WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), umeanza kutumia teknolojia ya mifumo ya kufuatilia viashiria na matukio ya moto, kwa njia ya mtandao kupitia satelaiti.
Mifumo hiyo itawawezesha wahifadhi kuchukua hatua za haraka katika matukio hayo na kuyadhibiti, kwa kushirikina na wadau wengine .
Ofisa Uhifadhi Mwandamizi wa TFS, Rodgers Nyinondi, alisema hayo juzi wakati wa mafunzo kwa wahifadhi kutoka Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani hapa.
Nyinondi ambaye ni mtaalamu wa ufuatiliaji na matukio ya moto msituni, alisema lengo la kujengewa uwezo huo ni wahifadhi kupata ujumbe wa matukio ya moto, kwenye maeneo wanayoyasimamia kupitia simu janja.
Alisema kuyapata kwa uharaka matukio hayo na kubaini viashiria vya moto, kutawarahisishia kudhibiti na kuyafikia matukio hayo kwa haraka zaidi na kuuzima.
Kwa mujibu wa Nyinondi, mafunzo hayo ni sehemu ya kwanza ya mpango wa muda mrefu, ambayo watapewa wahifadhi wote wa TFS nchini, ili kuwawezesha kukabiliana na matukio ya moto na kubaini viashiria vyake, kwenye maeneo yao. Hivyo kuchukua hatua za udhibiti.
“ Hii ni sehemu ya kwanza ya mafunzo kutolewa na TFS kwa wahifadhi wa wilaya, mashamba ya miti na hifadhi ya msitu asilia wa Kanda ya Mashariki, lakini baadaye yataendelea maeneo mengine ya nchi,” alisema.
Nyinondi alisema lengo kubwa la mafunzo hayo ni kuhakikisha matukio ya moto yanadhibitiwa pale yanapotokea na pia katika kufuatilia viashiria vya moto, kabla hayajijatokea na kuchukua tahadhari.
Alisema mfumo huo wa kidigitali unatumia sateleiti zinazodhaminiwa na mashirika ya anga ya Marekani na nchi nyingine za Ulaya.
“Huu ni mfumo wenye kuleta tija, kwa haraka na pia ni mfumo rafiki. Kinachotakiwa ni kuwa na simu janja na kutumia mtandao na kungia na kuona matukio ya moto maeneo mbalimbali, ili kama uko jirani kuchukua tahadhari mapema,” alisema.
Pia alisema teknolojia hiyo ilivyo, TFS itaendelea kuwafundisha wataalamu wake ambao nao watawafikia wananchi na kuwafundisha mifumo hiyo, ambayo itawasaidia watu kuchukua tahadhari ya baadaye .
Naye Ofisa Mhifadhi, Zarina Shaweji, kutoka Hifadhi ya Mazingira ya Asili Uluguru, alisema mafunzo waliyopata ya kutumia satelaiti kwa kutumia mtandao ya kutambua au kupata vashiria vya moto unaotokea msituni, yamekuwa ya muhimu.
Alisema njia hiyo inawezesha wahifadhi hata wanapokuwa nje ya misitu kutambua moto unaotokea ndani ya msitu, kwa kupata ujumbe katika simu.
Kaimu Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, Matthew Ntilicha, aliwataka wananchi kuwa mabalozi katika masuala ya udhibiti wa moto katika misitu ya asili na hifadhi .
Ntilicha alisema TFS imeandaa programu ya kupita kwenye shule mbalimbali ndani ya kanda hiyo, ili kuzungumza wanafunzi baada ya kubaini nyakati za likizo wanafunzi kwa baadhi ya maeneo wanashiriki kwenye suala la moto bila ya wao kuwa na uelewa.
Alisema program hiyo, itaanza kutekelezwa katika shule zilizoko kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi na itakuwa chachu kwa wanafunzi kushiriki mapambano dhidi ya moto na kuchangia kudhibiti viashiria vya moto, kwenye maeneo ya hifadhi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED