SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema itaendelea kukuza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji na kuweka mkazo wa kurahisisha michakato, kuimarisha mifumo ya udhibiti na kutoa motisha za kuvutia uwekezaji.
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo alipofungua Maonesho ya Utalii na Uwekezaji Zanzibar, viwanja vya maonesho ya Biashara Nyamanzi, wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni mwendelezo wa kupongeza mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya nane anayoiongoza.
Alisema Zanzibar imefungua milango wazi kwa fursa za biashara na uwekezaji na tayari imewakaribisha wadau mbalimbali, kushirikiana nao kwenye maono ya ukuaji wa Uuchumi endelevu na ustawi wa utalii wa muda mrefu.
Dk. Mwinyi alisema maonesho hayo yamedhihirisha thamani ya ushirikiano baina ya wadau wa utalii nchini, Sekta ya Umma na Kibinafsi (PPP) na kwamba ushirikiano wao ni njia muhimu za kufikia malengo ya pamoja.
Rais Dk. Mwinyi aliwashauri wadau wa utalii kuendeleza utamaduni na shauku ya kufanya Maonesho ya Utalii na Uwekezaji si kwa mnasaba wa Zanzibar pekee, bali kwa Afrika Mashariki na medani za kimataifa, ili kuendelea kuitangaza nchi na vivutio vyake duniani kote.
Alisema hatua hiyo itaiwezesha Zanzibar kuwa kituo bora cha ushindani kwa utalii kwenye ramani ya dunia.
Pia alisema maonesho hayo ni fursa nzuri za kubadilishana uzoefu, kuweka harambee, misingi ya miradi ya kuleta mabadiliko kwenye sekta ya utalii nchini na kuwahimiza wadau wa utalii kushiriki kikamilifu na kuchangia katika kuunda mustakabali wa utalii na uwekezaji Zanzibar.
Alisema maonesho hayo yanaashiria mwanzo wa mashirikiano mapya na wa kudumu na ubunifu tu si dhamira ya utalii na uwekezaji peke bali ari ya pamoja ya kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa kinara wa ukuaji endelevu, uhifadhi wa utamaduni na maendeleo ya kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi alisema sekta ya utalii licha ya kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi, bado inaakisi nadharia nzima ya maisha ya Wazanzibari, elimu kwa vizazi vilivyopo pamoja na kuhifadhi utamaduni wa utambulisho wa taifa.
Dk. Mwinyi alibainisha kwamba faida za utalii na uwekezaji zinufaishe visiwa vyote vya Unguja na Pemba, kwa kutengeneza fursa kwa watu wote.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga, alipongeza juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais. Mwinyi kwamba mafanikio makubwa yaliyopo kwenye sekta ya utalii ni kazi kubwa inayofanywa na kiongozi huyo.
Pia alisema miaka minne ya mafaniko kwenye uongozi wa Dk. Mwinyi, imeakisi maendeleo endelevu ya sekta ya utalii na kukuza biashara na uwekezaji nchini.
Maonesho hayo ya Utalii na uwekezaji Zanzibar, 2024 yameandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kamisheni ya Utalii na sekta binafsi.
Katika hafla hiyo pia kulitiwa saini makubaliano ya ushirikiano baina ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji na Vitegauchumi Zanzibar (ZIPA) katika kuendeleza kazi za utalii na kurahisisha uwekezaji kwa kuendeleza vivutio vipya kwa maeneo ya utalii nchini.
Aidha, yalitiwa saini makubaliano baina ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Baraza la Sanaa Zanzibar katika kuondosha changamoto zinazotokana na utalii, hususan eneo muziki, sanaa na burudani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED