MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali itaendelea kuimarisha sekta ya uwekezaji na shughuli za biashara ili kukuza uchumi na kuongeza fursa nyingi za ajira kwa vijana.
Amesema tayari serikali imesajili na kutenga zaidi ya miradi 330 yenye thamani ya mtaji wa USD bilioni 5.4 ili kuzalisha ajira zaidi ya 18,000 kwa sekta mbalimbali zikiwamo, utalii yenye miradi 112, biashara ya majengo 56, viwanda 36 na sekta nyingine.
Dk. Mwinyi ambaye pia ni rais wa Zanzibar aliyasema hayo jana katika viwanja vya Gombani, Kaskazini Pemba, alipozindua Kampeni ya Kijana Kijani Pemba ikiwa ni shamrashamra za kupongeza miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane, anayoiongoza.
Alisema serikali imetoa vifaa vya uzalishaji kwa vijana vyenye thamani ya Sh. milioni 985.503 kwa vikundi 420 pamoja na ruzuku ya Sh. milioni 338.611 kwa vikundi 395 vya vijana ili kuwainua na kuwawesha kiuchumi.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata mitaji ya kuendesha shughuli zao, Rais Dk. Mwinyi alisema, hadi kufikia mwezi Machi, mwaka huu, kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, serikali imetoa zaidi ya Sh. bilioni 31.8 kwa wajasiliamali wadogo wadogo Unguja na Pemba, ambapo asilimia 40 ya wanufaika ni vijana wa umri kati ya miaka 18- 35.
Rais Mwinyi pia alisema kujengwa kwa vituo vya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo kwa kila wilaya ni kuwawezesha wananchi wa Zanzibar kwa kuwapa maeneo mazuri ya kufanya shughuli zao na kuzalisha fursa za ajira.
Akizungumzia nia ya serikali kuendeleza juhudi ya kuifungua Pemba kimaendeleo, Rais Mwinyi alisema serikali imeendeleza kazi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kuu na za vijijini, kutengeneza bandari za mkoani na Shumba na kuanza matayarisho ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba.
Alisema serikali inaendelea kuimarisha eneo la uwekezaji la Micheweni na eneo la viwanda Chamanangwe kwa kuyawekea miundombinu na kuongeza kuwa, tayari kuna wawekezaji waliojitokeza kuwekeza maeneo hayo, hatua aliyoieleza kwamba, itaongeza fursa za ajira kwa vijana.
Akizungumzia kuhusu kuimarisha shughuli za biashara na ujasiriamali kwa vijana, Rais Mwinyi alisema mafanikio ya Serikali ya Awamu ya nane ya ujenzi wa masoko makubwa ya kisasa likiwamo Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini ambayo mawili tayari yashafunguliwa.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alisema wananchi wa Pemba wanafahamu thamani ya maendeleo na kuona juhudi za Rais Mwinyi na Wanzanzibar wanaupenda uongozi wa serikali.
Aliwasihi wananchi wa Zanzibar kujihusisha na siasa ni maendeleo sio ugomvi.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, UVCCM na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Joketi Mwegelo, alisema CCM itashinda kwa ushawishi na imani kubwa kwa viongozi wao.
Alisema CCM hakiyumbishwi kwa chokochoko na majungu ya uvunjifu wa amani, bali misimamo ya viongozi wa kuu wa nchi wanaohubiri na kusisitiza umoja, utulivu, msikamamo na uthubutu.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Masoud, akiwawakilisha wananchi wa mikoa miwili ya Pemba Kusini na Kaskazini, alipongeza juhudi kubwa ya maendeleo iliyofanywa ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Mwinyi.
Pia alisifu hatua ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kujenga madarasa 661 kwa mikoa yote ya Pemba skuli za ghorofa 13, ajira za walimu 1,500 kutolewa vibali vya ajira za walimu, 600 ujenzi wa vyoo 953 kwa skuli mbalimbali na ujenzi wa hospitali kwa wilaya tatu za Pemba.
Kadhalika ukarabati mkubwa kwa hospitali ya Abdalla Mzee, kuongezwa kwa chumba cha ICU na uchunguzi na ajira 468 sekta ya afya na huduma nyingine za jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED