RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar ni nchi salama kwa utalii wa mikutano na makongamano ya kimataifa.
Alhajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana, wakati wa kongamano la kwanza la Kiislam la kimataifa lililowakutanisha pamoja mashehe mbalimbali kutoka mataifa 18 duniani kwenye viwanja vya New Amani Complex, wilaya ya Mjini, mkoa wa Mjini Magharibi.
Dk. Mwinyi alisema Zanzibar ina fursa kubwa ya kukuza utalii wa maadili ‘Halal Tourism’ kama chanzo cha mapato na ajira kwa watu wake, kupitia kongamano hilo la Kiislamu la kimataifa, limetoa mwangaza kwa nchi kama sehemu ya utalii wa Maadili hasa kwa wageni wanaofika kuitembelea, sio tu kujifunza dini lakini kufurahia uzuri wa mandhari na haiba ya nchi, mila, silka, utamaduni na ukarimu wa watu wake.
Akizungumzia faida za kongamano hilo, Alhajj Dk. Mwinyi alibainisha kuwa haziko za kiimani pekee, bali pia kuna manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Taifa.
Pia alieleza mafanikio ya tukio hilo muhimu kwa Zanzibar, ni ufunguo adhimu wa kuitangaza kwa utalii wa maadili “Halal Tourism”, ambao watu kutoka sehemu mbalimbali duniani huja kushiriki mikusanyiko ya kidini na matukio yenye uhusiano na tamaduni za dini.
Alisema ni jambo la kujivunia na kumshukuru Mwenyezi Mungu kuona wageni wengi kutoka mataifa tofauti duniani, wameungana kupitia mitandao ya kijamii kuangalia moja kwa moja kongamano hilo muhimu.
Alhajj Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa mikusanyiko kama hiyo na kuunga mkono jitihada za taasisi binafsi, ikiwamo kukuza uchumi na maadili ya nchi, ili kupatikane jamii yenye maadili na kuiweka nchi kwenye hadhi ya utalii wa maadili ambao hivi sasa umeshika kasi duniani.
Aliiasa jamii kuendelea kudumisha maadili kwenye maisha yao ya kila siku, ili kujenga taifa lenye maelewano, amani, heshima na ushirikiano kwa wote. Hatua hiyo akisema ina mchango muhimu katika kupatikana kwa mafanikio duniani na kesho mbele ya haki.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alisifu amani iliyopo nchini na kueleza utulivu wa watu wake kutokana na ukarimu na maadili haya walivyoonesha kwenye kongamano hilo.
Akihadhir mbele ya zaidi ya waumini wa Kiislam na waananchi wa Zanzibar 20,000 waliofika viwanja vya New Amani Complex, kumshuhudia Mufti Mkuu wa Zimbabwe, Ismael Menki, alisema maendeleo kwa taifa lolote duniani hayatimii pasi na kuwapo ustawi wa amani na usalama kwa nchi na watu wake kwa kuendeleza, kudumisha umoja, upendo na kuheshimiana miongoni mwa jamii.
Mufti Menki alisisitiza mshikamano miongoni mwa jamii na kuwasihi waendelee kufungamana kwa Imani, heshima na upendo sio kufarakana kwa tofauti za mitazamo ya dini na siasa.
Pia aliwasisitiza waislamu kuzingatia zaidi utulivu wanapokuwa kwenye sala zao kwani kufanya hivyo ni kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu (S.W), vilevile alipongeza maendeleo makubwa yaliyofikiwa Zanzibar akitoa ushuhuda wa tofauti ilivyo sasa na miaka 10 iliyopita, ikiwa mara ya kwanza kufika Zanzibar wakati huo.
Wakizungumza kwenye Kongamano hilo, Sheikh Ali Hamuuda Ali kutoka Uingereza, Sheikh Wael Ibrahim kutoka Australia na Dk. Muhammad Salah, Sheikh kutoka Misri, walisisitiza wananchi wa Zanzibar kuendelea kutunza amani na usalama kwa ustawi wa nchi yao, hasa katika kuzifikia ndoto za maendeleo ya taifa lao.
Walieleza uwapo wa amani na utulivu wa nchi husaidia hufanikisha mazuri yasiyowezekana, kuwezekana kwa usatawi mzima wa jamii.
Aidha, mashehe hao pia walihimiza kuhusu kuzikimbia dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kutofanya matendo yatakayomkosea Allah (S.W) pamoja na kujiepusha na anasa zinazomchukiza, Mwenyezi Mungu.
Eneo lingine waliloligusia masheikh hao ni kusisitiza waislamu kusalimiana kwa upendo na kushirikiana kwa hata wasiokua waislam, ili kujenga jamii moja yenye usawa, upendo, kuheshimiana kwenye kujenga maendeleo ya nchi yao, pamoja na kuwahimiza kudumisha sala za usiku katika kujitakasa na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (S.W), ili kujiepusha na maovu yanayotokana na sheitwani na kujitakasa kwa Allah (S.W).
Mwenyekiti wa Taasisi ya "Light upon light" (Noor alaan Noor) Sheikh Nadir Mahfoudh, alimshukuru Rais Alhaji Dk. Mwinyi na Serikali kupitia Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais na Ofisi ya Rais - Utawala Bora chini ya uratibu wa Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, kwa kusimamia kongamano hilo hadi kufanikiwa kwake.
Hii ni mara ya kwanza kwa historia ya Zanzibar, kufanya kongamano kubwa la kidini la kimataifa lililojumuisha wahadhiri na mashekhe mbalimbali maarufu kutoka nje ya nchi.
Kongamano hilo liliandaliwa na kuratibiwa na Taasisi ya ‘Light upon light’ kwa ushirikiano na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, lililofuatiliwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari vya ndani na mitandao ya jamii liliangaliwa na zaidi ya watu bilioni 1.3 duniani kote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED