Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko ameipongeza Wizara ya Madini kuanzisha na kusukuma uwapo wa akiba ya Dhahabu kupitia Benki kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
Akifungua maonesho ya saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yenye kauli mbiu ya 'Matumizi ya Teknolojia sahihi ya Nishati safi katika sekta ya Madini kwa maendeleo endelevu' yanayofanyika mkoani Geita, Biteko amesema utajiri wa madini ikiwamo Dhahabu, lazima uwe na chachu katika ukuaji wa uchumi.
Naye, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameeleza kwamba kwa sasa baada ya kukaa pamoja baina ya serikali na wadau wamefikia muafaka na hakuna mgomo tena wa kutoiuzia Dhahabu BoT baada ya ufafanuzi wa baadhi ya hoja na elimu kutolewa ikiwa ni sehemu ya falsafa ya maridhiano inayohubiriwa kwa nguvu na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mavunde ametoa rai kwa wadau wote kushirikiana na serikali katika mpango huo wa upatikanaji wa akiba ya dhahabu kupitia BoT na kuahidi kutoa ushirikiano katika kushughulikia changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.
Awali, Rais wa Shirikisho la Vyama cha Wachimbaji Madini(FEMATA), John Bina ameipongeza Wizara hiyo kwa usikivu na majadiliano ya mara kwa mara pindi changamoto zinapojitokeza na kuahidi kwamba baada ya kikao cha pamoja wadau wameridhia mpango wa serikali wa ununuzi wa dhahabu kupitia BoT.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED