WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka vijana nchini kutojihusisha na mikopo yenye masharti magumu, maarufu kama ‘kausha damu’ kwa kuwa itawafanya waishi maisha magumu na hatimaye kushindwa kutimiza malengo yao.
Majaliwa alisema hayo juzi wakati akifungua Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, yaliyofanyika jijini hapa, huku akisema haiwezekani taasisi kutoa mikopo kwa asilimia 100 na ikitakiwa kurejeshewa ndani ya muda mfupi.
Alisema ukopeshaji wa namna hiyo hautakiwi kufuatwa na vijana wala watu wa aina yoyote, kwa kuwa hakuna maendeleo bali ni maumivu kwa mkopaji.
"Nawasihi sana msiende kwenye mifuko ya ukopeshaji inaitwa kausha damu, wana mashari#ti magumu. Eti anakukopesha leo Ijumaa (juzi) anakwambia Ijumaa ijayo zote zirudi, halafu ukirudi anataka kama hiyo hiyo uliyoikopa. Hii haiwezekani.
“Asilimia 100 haiwezekani hata benki walitaka watoe asilimia 15 tuliwaambia ni ngumu kwa Watanzania. Hawa wananchi wa kawaida, sasa hivi wameshuka wako kwenye nane, saba, sita na tunaendelea ikiwezekana waende kwenye tano, nne hata moja,” alisema Majaliwa.
Pia alisema katika kukabiliana na suala hilo, serikali imeweka utaratibu maalum wa kupata mikopo kwa masharti nafuu kupitia Programu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alisema katika program hiyo iliyoko chini ya Kurugenzi ya Uwezeshaji Kiuchumi, umefanyika uwekezaji wa miradi ya zaidi ya Sh. bilioni 1.6 inayowanufaisha zaidi ya wananchi milioni 3.7.
Waziri mkuu alisema wanufaika katika uwezeshaji huo, ni vikundi mbalimbali kwa kuelimishwa na kupata fedha zenye masharti nafuu na pia ipo mikopo ya halmashauri ya asilimia 10 iliyoanza kutolewa mwezi huu, baada ya kufungwa kwa muda, ili kupata njia sahihi ya utoaji huduma hiyo.
Pia alisema serikali inatambua juhudi na uwapo wa vijana na kuwataka kutobaki nyuma katika mabadiliko ya sayansi na teknolojia, bali waungane na wengine kwa kuwa yana mchango muhimu katika kusaidia kufanya uamuzi wenye tija katika shughuli mbalimbali.
"Kila mmoja ajikite kwenye eneo hili la teknolojia, ili turahisishe utendaji kazi nchini na sisi tunaendelea kunyoosha fursa za vijana, ili kila mmoja azione na kushiriki ipasavyo kujipatia mafao kwenye maisha yake,” alisema.
Majaliwa pia alisema serikali inatambua na kuheshimu mchango wa vijana nchini na mikakati mbalimbali imeendelea kutekelezwa na taifa, ili kuhakikisha kila kijana anapata fursa kwa ajili ya maendeleo yake binafsi na taifa.
Kuhusu ajira, Majaliwa alisema Tanzania ni moja ya nchi zinazokabiliwa na tatizo hilo duniani na kwamba, juhudi mbalimbali zimeendelea kufanyika ikiwa ni kuzalisha ajira takribani 162,968, zikiwamo 112,572 katika ujenzi na 21,445 sekta ya madini.
“Tukisemea ajira watu wanawaza kupata kwenye ofisi za halmashauri, mkuu wa mkoa na wizarani na Tanzania nzima, tuna watumishi wasiozidi milioni mbili na nchi nzima tuko zaidi ya milioni 62.
Hiyo ni ngumu na si kwetu tu ni duniani kote na serikali inachokifanya ni kufungua milango ya ajira serikalini na sekta binafsi na zile shughuli mbalimbali za kujipatia pato binafsi,” alisema.
Alisema kupitia programu iliyoanzishwa mwaka 2001 wanaratibu programu inayogharamiwa na serikali kwa miezi sita, ili kuwaimarisha vijana katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi kwa lengo la kuwapa ujuzi na wakitoka huko wajiajiri na kuwa na sifa za kuajiriwa.
Alisema wanaimarisha fursa za upatikanaji wa elimu kuanzia awali mpaka kidato cha sita bure na vyuo vikuu, ambako kuna utaratibu wa kuchangia.
Alisema mikopo hiyo imeendelea kupanda kutoka Sh. bilioni 400 hadi 700 na kwamba, serikali imeendelea kufungua milango ya ajira katika sekta mbalimbali za binafsi na serikalini kwa wazawa, ili vijana wapate fursa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED