WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali haijatoa maagizo ya kuwaondoa kazini walimu wa cheti, bali imewataka watumie mpango wa mafunzo endelevu kazini kwenda vyuoni kusoma.
Amesema serikali imefanya maboresho ya sera na mitaala ya elimu nchini, ambayo pamoja na mambo mengine, imeleta mabadiliko katika sifa za chini za mwalimu katika shule za msingi kuwa na stashahada (diploma).
“Pamoja na mabadiliko haya, serikali inatambua kuwa bado wapo walimu ambao hawajafikia sifa ya kuwa na stashahada au diploma na hakuna agizo la kuwataka waondolewe katika ajira,” amesema.
Alitoa kauli hiyo juzi Oktoba 11, mwaka huu, wakati akizungumza na mamia ya walimu na wadau walioshiriki maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani, yaliyofanyika kwenye uwanja wa mpira wa shule ya sekondari Ushirombo, wilayani Bukombe, mkoani Geita.
Alisema walimu wote ambao hawana sifa ya stashahada au diploma watumie fursa ya mpango wa mafunzo endelevu kazini kwenda vyuoni kusoma, ili kupata sifa ya diploma au kujiendeleza kupitia moduli kwa mfumo wa LMs - Learning Management System chini ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE).
“Kupitia mfumo huu, serikali imeingia makubaliano na kampuni ya simu ya Airtel, kwa walimu wenye vishikwambi na wanatumia mtandao wa Airtel kupakua moduli bure kwa ajili ya kujiendeleza," alisema.
Waziri Mkuu pia aliagiza TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, taasisi za elimu, sekta binafsi na wadau wa sekta ya elimu nchini, wahakikishe walimu wanajengewa mazingira bora ya kazi, ili watimize majukumu yao kwa ufanisi.
Pia aliwataka waimarishe programu za mafunzo kwa walimu, ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, huku akiwataka waajiri kuwapa mafunzo walimu pamoja na taasisi zinazohusika na udhibiti wa ubora waendelee kutimiza majukumu yao.
Katika kuboresha sekta ya elimu nchini, Waziri Mkuu alisema serikali imeendelea kuboresha na kusimamia miundo ya watumishi wakiwamo walimu.
“Serikali imeboresha stahiki za msingi za watumishi kwa kupandisha madaraja na kuhakikisha wanapata nyongeza ya mishahara yao kwa wakati," alisema Majaliwa.
Akiainisha maboresho mengine, Waziri Mkuu alisema: “Serikali imeimarisha miundombinu mahali pa kufanyia kazi, ikiwamo kuhakikisha kuna madarasa, maabara, mabweni, majengo ya utawala na sasa tumeingia kwenye ujenzi wa nyumba za walimu pamoja na kuimarisha ajira zao.”
Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari, kupitia miradi mbalimbali kama vile Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), Mradi wa Kuimarisha na Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), Mradi wa Huduma za Maji, Elimu ya Afya na Usafi wa Mazingira (SWASH), Programu ya Uboreshaji Kada ya Ualimu (GPE-TSP) na Programu ya Kutekeleza Elimu kwa Matokeo (EP4R).
Akielezea kuhusu upandishaji madaraja kwa walimu, alisema: “Kati ya Machi, 2021 na Agosti, 2024, walimu 601,698 nchi nzima wamepandishwa madaraja na serikali imetumia Sh. trilioni 1.3 kuwalipa. Na niwatake maofisa elimu kuwatembelea walimu vijijini na kusikiliza kero zao,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Alisema katika kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi sasa, serikali imebadilisha kada/miundo jumla ya watumishi 36,768 kwa gharama ya sh. 3,090,476,931.00 na imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 144,356 ya Sh. milioni 229.9.
Akimkaribisha Waziri Mkuu, kuzungumza na hadhara hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko aliwashukuru walimu wa Tanzania, kwa kuendelea kuiheshimisha taaluma yao na kuwa chanzo cha maarifa kwao, hivyo wailinde kwa wivu mkubwa taaluma hiyo.
Dk. Biteko alisema mwaka 2015 wakati anachaguliwa kuwa mbunge, wilaya yake ilikuwa ikishika nafasi ya mwisho katika mitihani ya taifa.
“Nilizungumza na walimu kuhusu matokeo mabaya na wakasema tusiwaache walimu nyuma, hivyo tulianza kukutana na kufanya tathimini na sasa tunafanya vizuri," alisema.
Alisema viwango vya ufaulu vimekuwa vikiongezeka kila mwaka, huku akitolea mfano wa matokeo ya mwaka jana kwamba darasa la saba ya wilaya hiyo ilishika nafasi ya pili katika mkoa huo, darasa la nne ilipata wastani wa asilimia 78 na kuwa nafasi ya pili kimkoa.
“Kidato cha pili tulikuwa na ufaulu wa asilimia 98, kidato cha nne ufaulu ulikuwa asilimia 96, kidato cha sita ulikuwa asilimia 100 na hizi zote tulikuwa wa kwanza. Katika mitihani ya ‘mock’ ya kanda ambayo ilijumuisha mikoa mitano yenye Halmashauri 37, Wilaya ya Bukombe tumeshika nafasi ya tatu, tukiwa nyuma ya Ilemela na Nyamagana. Hivyo, niliona tutenge siku moja ya kusema asante mwalimu," alisema.
Aidha, Dk. Biteko amesema kuwa walimu nchini wasivunjike moyo, waendelee kufanya kazi yao na kwamba maisha yao ni kielelezo cha mafanikio katika taifa na kuwa wao ni nyota inayoangaza na yeye ataendelea kushirikiana nao.
Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Mkoa wa Geita, Pauline Tinda, alisema tangu mwaka 2019, Wilaya Bukombe imekuwa ikiadhimisha Siku ya Mwalimu ambayo inalenga kutekeleza maelekezo ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kuwatambua na kutoa tuzo za umahiri, kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wanaofundisha masomo ya kusoma, kuandika na kuhesabu.
Aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha utendaji kazi kwa walimu ma ustawi wa walimu kwa kufanya jitihada mbalimbali, ikiwamo kuwapandisha madaraja. Pia alimshukuru Dk. Biteko kwa kuendelea kuthamini mchango wao katika jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema kuwa benki hiyo inatambua umuhimu wa walimu nchini na kuwa watu wengi wamefanikiwa kutokana na mchango wao.
“Sisi tunawapongeza walimu wote nchini. Tumeendelea kuunga jitihada nzuri zinazofanywa, ili mwalimu awe na mazingira mazuri ya kufanya kazi. Hadi sasa tumetoa zaidi ya shilingi bilioni moja, ili kununua madawati na leo (jana) tunachangia madawati 545 na magodoro 88 kwa shule mbalimbali za wilaya hii, ili kusaidia elimu ya Tanzania iwe bora zaidi,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED