Majaliwa asema SDG msingi wa matumaini

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:41 AM Sep 29 2024
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia kwenye Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79) New York nchini Marekani, Septemba 27, 2024. Mheshimiwa Majaliwa amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo.
Picha:Mtandao
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia kwenye Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79) New York nchini Marekani, Septemba 27, 2024. Mheshimiwa Majaliwa amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amehutubia Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79) na kusema Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ni msingi wa matumaini katika kukabiliana na changamoto za kidunia.

Hii ni mara ya pili kwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mara ya kwanza ilikuwa Septemba 27, 2010 wakati Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo  Pinda, alipolihutubia Baraza la 65 (UNGA65). 

Majaliwa alisema hayo juzi wakati akihutubia kwenye mkutano huo ulioshirikisha wakuu mbalimbali wa nchi jijini New York, Marekani, anakomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan. 

Alisema chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imedhamiria kufanikisha malengo endelevu ya kiuchumi, ufugaji, uwekezaji katika miundombinu na mifumo ya kidijitali, uvuvi na nishati.

 “Lengo letu ni kufikia uhakika wa kupunguza umasikini, kutengeneza ajira mpya na kusukuma mbele maendeleo ya uchumi shirikishi katika nyanja mbalimbali. 

“Kuna shuhuda nyingi za taarifa za makuzi katika sekta hizo Tanzania zinazotokana na mikakati kama ya Kesho Iliyo Bora (BBT) unaohusu kilimo kwa Tanzania Bara na uwezeshaji wanawake wanaoshiriki kilimo cha mwani Zanzibar. 

Alisema Tanzania, kama yalivyo mataifa mengine, imekuwa ikipambana na changamoto kama za athari za UVIKO-19 kwenye sekta ya afya, mabadiliko ya tabianchi yanayojidhihirisha katika ongezeko la hali mbaya ya hewa kama mvua haribifu na ukame uliokithiri, pamoja na mambo mengine, vimeathiri ufikiwaji wa malengo endelevu. 

Majaliwa alizungumzia pia Sera ya Tanzania ya Mambo ya Nje kuhusu utu kwamba Desemba 14, 1961 wakati akiwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere alisema: “Msingi wa matendo yetu, ya ndani (ya nchi) na ya nje (nchi za nje) utakuwa ni kujaribu, kiungwana, kuheshimu utu wa mtu.” 

Alisema Tanzania imeendelea na msimamo huo katika mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi na kwamba kwa muktadha huo Tanzania ilikuwa ni mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi wa Bara la Afrika (OAU) ikiwaunga mkono wapigania uhuru wa mataifa mbalimbali ya Afrika. 

Alisema pamoja na kupatikana kwa uhuru, mataifa hayo bado yanakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi na mazingira hatarishi kwa utu yanayokwamisha upatikanaji wa maendeleo halisi. 

 “Kwa hiyo tunatoa wito watu wajitawale wale ambao bado katika mifumo ya ukoloni, na kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa kwa mataifa ya Cuba na mengineyo,” alisema.               

 Alitumia jukwaa hilo kuliarifu baraza hilo juu ya uwepo wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika nchini. 

 “Novemba, mwaka huu, Tanzania itafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kisha kufuatiwa na uchaguzi wa Rais na Wabunge Oktoba, 2025. Tunapojiandaa kwa matukio haya ya uchaguzi, ningependa kuliarifu baraza hili kuwa demokrasia, haki za binadamu, na utawala wa sheria vitaheshimiwa, sambamba na maono ya Rais Samia kama ilivyoelezwa katika falsafa ya 4R, ambazo ni upatanisho, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi upya,” alisema.