WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, amezipongeza hifadhi za Serengeti na Mlima Kilimanjaro, kwa kushinda tuzo za utalii za Bara la Afrika, huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kuendelea kuitangaza sekta ya utalii duniani kupitia Filamu ya Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hassan Abbasi, Taasisi ya Tuzo za Dunia za Utalii Kanda ya Afrika (World Travel Awards Africa - Gala), imeitangaza Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa kuwavutia watalii barani Afrika mwaka 2024 na Bodi ya Utalii Tanzania kuwa bodi inayoongoza Barani Afrika mwaka 2024.
Aidha, taasisi hiyo imezitangaza hifadhi mbili za Serengeti na Mlima Kilimanjaro, kuwa washindi kwenye kipengele cha Hifadhi na Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika mwaka 2024.
Hifadhi ya Taifa Serengeti imetangazwa kuwa mshindi katika kipengele cha Hifadhi Bora Barani Afrika (Africa’s Leading National Park 2024), wakati Mlima Kilimanjaro ikitangazwa Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika (African Leading Tourism Attraction 2024)
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serengeti imezishinda hifadhi zingine kwa ubora barani Afrika, ilizoshindanishwa nazo ambazo ni Maasai Mara ya Kenya, Kruger ya Afrika Kusini, Central Kalahari ya Botswana, Etosha ya Namibia na Kidepo Valley ya Uganda.
Mlima Kilimanjaro umevishinda vivutio vingine vya utalii ambavyo ni Hifadhi ya Ngorongoro, Hartbeespoort Aerial Cableway, V&A, Waterfront, Robben Island, Table Mountain zote za Afrika Kusini. Pia Ziwa Malawi, Okavango Delta ya Botswana na Pyramid of Giza ya Misri.
Taarifa hiyo pia ilisema Mlima Kilimanjaro umeshinda tuzo hiiyo ya kivutio Bora Barani Afrika mara sita, kuanzia mwaka 2013, 2015, 2016,2017, 2018 na sasa 2024 huku Hifadhi ya Serengeti nayo imeshinda mara sita mfululizo kuanzia mwaka 2019.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED