Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amesema uwapo wa soko la Machinga Complex jijini Dodoma limesaidia wafanyabiashara wadogo kufanya biashara zao kwa utulivu na kuwahamasisha kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri.
Aidha, aliwataka mgambo wa Jiji hilo kuacha kutumia mabavu makubwa wanaposhughulika na wafanyabiashara wadogo ili biashara zao ziwe na tija.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa soko hilo, Mavunde aliupongeza uongozi wa soko kwa kuandaa mkutano wa kusikiliza kero za wafanyabiashara na kueleza kuwa soko hilo la kisasa limewasaidia kuondokana na kukimbizana na mgambo barabarani.
Alichangia Sh.Milioni 10 kwa ajili ya kutunisha mfuko wa soko huku akiwahamasisha kuchangamkia mikopo kwa wafanyabiashara hao kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji na kuwaunganisha na Taasisi za Fedha.
Naye, Kaimu Mwenyekiti wa Machinga Complex Lucas Kingamkono aliishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga soko hilo ambalo limerahisisha ufanyaji wa biashara kwa wafanyabiashara hao wadogo ambao awali walikuwa maeneo ambayo hayakuwa rasmi na hivyo kufanya biashara kwa mashaka.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED