Yanga yaendeleza ubabe kwa Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 11:22 AM Apr 21 2024
Azizi  Ki akishangilia goli alilofunga katika mchezo wa jana dhidi ya Simba.
PICHA: YANGA
Azizi Ki akishangilia goli alilofunga katika mchezo wa jana dhidi ya Simba.

MABAO yaliyofungwa na nyota ambaye yuko katika kiwango cha juu, Stephane Aziz Ki na Joseph Guede yaliipa Yanga ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wapinzani wao wa jadi Simba katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam jana.

Yanga imeweka rekodi ya kushinda mechi mbili kwa msimu mmoja baada ya misimu minane kupita.

Mara ya mwisho kati ya timu hizo mbili kushinda katika mechi ya dabi ilikuwa ni msimu wa 2015/16, ambapo Yanga iliifunga Simba mabao 2-0 katika mechi zote mbili katika msimu huo.

Mechi ya mzunguko wa kwanza Yanga ilishinda mabao 2-0, yaliyowekwa wavuni na Amissi Tambwe na Malimi Busungu na mzunguko wa pili ilishinda idadi hiyo hiyo ya magoli yaliyofungwa na Donald Ngoma na Tambwe.

Imejirudia tena msimu huu, katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika  Novemba 5, mwaka jana mabingwa hao watetezi walipata ushindi mnono wa mabao 5-1.

Kocha Mkuu wa Yanga, raia wa Argentina, Miguel Gamondi, naye anaingia katika  kitabu cha kumbukumbu cha mwalimu  aliyeiongoza timu hiyo kushinda dabi mbili kwa msimu mmoja, huku Abdelhak Benchikha, ikiwa ni dabi yake ya kwanza, ambayo ameanza kwa kipigo.

Ushindi wa jana umeifanya Yanga kufikisha pointi 58 na kuukaribia ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo huku Simba ikibakia na pointi 46, lakini imecheza mechi moja pungufu ukilinganisha na vinara hao.

Simba itabidi ijilaumu kwa kukosa mabao mengi ya wazi kwa sababu wao ndio walianza kufika katika lango la Yanga dakika ya pili tu kupitia, Saido Ntibazonkiza, alipopata mpira kwenye wingi ya kulia peke yake, baada ya Joyce Lomalisa kuteleza, lakini alikuwa na papara, badala ya kuangalia wenzake akapiga krosi fyongo iliyodakwa kwa urahisi na kipa, Djigui Diarra.

Yanga ilijibu shambulio hilo dakika moja baadaye, kwa Aziz Ki, kupiga mpira wa mbali kiasi cha mita 40 hivi, baada ya kuona kipa wa Simba, Ayoub Lakred, amesogea mbele ya lango, lakini mpira huo ulitoka juu ya lango.

Sadio Kanoute kama angekuwa makini angeweza kuipatia Simba bao dakika ya sita kufuatia krosi ya Israel Mwenda iliyotua kichwani kwake, akashindwa kuchagua engo sahihi, badala yake akapiga mpira uliodakwa kirahisi na Diarra.

Kwa mara nyingine tena, Kanoute alikosa bao akiwa yeye na wavu, dakika ya saba, akipiga mpira pembeni ambao ulirudishwa kimakosa na mabeki wa Yanga.

Moja ya tukio ambalo si la kawaida ni wachezaji wawili wa timu zote mbili, ambao ni raia wa Jamhuri ya Kidemkokrasi ya Congo (DRC),  kushindwa kuendelea na mechi kutokana na kuumia.

Lomalisa, beki wa kushoto, aliumia dakika ya sita kwa upande wa Yanga, nafasi yake ikachukuliwa na Nickson Kibabage, na dakika tano baadaye, Henock Inonga, wa Simba, naye alipatwa na tatizo la misuli kama mwenzake, akatoka na nafasi yake ikachukuliwa na Hussein Kazi, ambaye ndiye aliyesababisha penalti iliyozaa bao la kwanza kwa Yanga.

Awali aliokoa mpira ambao ulimbabua Aziz Ki, aliyeuchukua kumfungasha 'tela', kabla ya kucheza madhambi ndani ya eneo la hatari.

Penalti hiyo iliwekwa wavuni na Aziz Ki mwenyewe dakika ya 19, licha ya Lakred kuruka upande sahihi, lakini mpira ulikuwa na kasi zaidi kuliko yeye na kutinga wavuni.

Simba ilikosa tena bao la wazi dakika ya 35, pale Saido alipopata mpira ndani ya eneo la 18, akapiga shuti lililowababatiza mabeki wa Yanga, ukamrudia Kibu Denis aliyepiga shuti lililotoka nje ya lango.

Dakika mbili baadaye, Yanga iliifundisha Simba jinsi ya kutumia nafasi ilipopachika bao la pili, likifungwa na Guede, ambaye  akipokea mpira mrefu uliopigwa kutoka katikati ya uwanja, akaumiliki na kuwaacha mabeki wa Simba walidhania ameotea, akampiga chenga Lakred kabla ya kuujaza wavuni.

Kipindi cha pili, angalau Simba ilionekana kutulia na kusukuma mashambulizi katika lango la Yanga ambao sasa walitegemea zaidi mashambulizi ya kushtukiza.

Alikuwa ni nyota kutoka Ivory Coast, Freddy Michael, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Saido, aliyepachika bao la kufutia machozi dakika ya 73, akiitendea haki pasi ya Clatous Chama.

Aliwahadaa kwa chenga, Ibrahim hamad 'Bacca' na Bakari Mwamnyeto, kabla ya kuukwamisha wavuni.

Lakred alifanya kazi ya ziada dakika ya 78, alipookoa Simba isifungwe bao la tatu na Kennedy Musonda aliyeingia kuchukua nafasi ya Clement Mzize.