Riadha Afrika Mashariki sasa kufanyika Zanzibar

By Hawa Abdallah , Nipashe Jumapili
Published at 11:58 AM Apr 21 2024
Mashindano ya riadha.
PICHA: MAKTABA
Mashindano ya riadha.

MASHINDANO ya riadha ya Afrika Mashariki na Kati (EARA) sasa yatafanyika Zanzibar Aprili 26 na 27, mwaka huu badala ya Tanzania Bara kama ilivyotangazwa awali, imefahamika.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Zanzibar (ZAF),  Muhidini Yassin, amesema mashindano hayo yatashirikisha timu za taifa za wanariadha wenye umri chini ya miaka 18 na miaka 20.

Yassin amesema wanachama wa nchi zote 11 za ukanda huo wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo na wataanza kuwasili Visiwani hapa kuanzia April 24, mwaka huu.

Amesema wenyeji tayari wamejipanga kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ufanisi na kwa kufuata taratibu za michuano hiyo za kimataifa.

Kuhusu wanariadha wa Zanzibar, amesema tayari wameshachagua vijana 40 watakaounda timu mbili za taifa na wameshaanza maandalizi.

"Zanzibar kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kutatupa faida nyingi ikiwemo kuibua vipaji vya vijana na yatainua uchumi wananchi kwa sababu timu ambazo zitafika hapa zitalala katika mahoteli na kulipia kodi," amesema kiongozi huyo.

Ameongeza pia kuhamishia mashindano hayo Zanzibar kumetokana na ushirikiano uliopo na viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

"Wenzetu wa Tanzania Bara walipata changamoto ya uwanja, na kwa sababu viongozi tuna ushirikiano na umoja mzuri, hawakusita kuyaleta mashindano haya Zanzibar, tunatarajia kuwa na mashindano bora, maandalizi yake yako katika hatia za mwisho," ameongeza.