Yanga itumie vema nafasi ya mwisho michuano Caf

20Mar 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Yanga itumie vema nafasi ya mwisho michuano Caf

KAMA ilivyokuwa msimu uliopita, wawakilishi wa Tanzania kimataifa, Yanga wametolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na kuangukia Kombe la Shirikisho.

Ni baada ya kulazimishwa suluhu ya bila mabao ugenini dhidi ya wenyeji, Zanaco ya Zambia.

Kilichoiondoa Yanga kwenye michuano hiyo ni sare ya bao 1-1 iliyoipata nyumbani, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya timu hiyo.

Kwa kanuni za soka, Yanga imeondolewa kwa goli la ugenini ambalo walilipata Zanaco kwenye mechi ya awali, kwani huhesabika mawili kama timu zitaonekana ziko sawa kimatokeo ya mechi zote mbili.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Yanga kutolewa kwenye michuano hiyo. Msimu uliopita ilitolewa na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 3-2.

Ililazimishwa sare ya bao 1-1 nchini na kufungwa mabao 2-1 huko Misri.

Baada ya hapo ikaangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho. Droo ilipopangwa, iliangukia kwa Sagrada Esperanca ya Angola.

Katika mechi ya kwanza nchini, Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 na kwenda kufungwa bao 1-0 ugenini, matokeo ambayo yaliifanya kusonga mbele na kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, ikiwa na timu ya Mo Bejaia ya Algeria, TP Mazembe ya Congo DR na Medeama ya Ghana.

Tofauti pekee iliyokuwapo msimu uliopita na huu ni kwamba, njia ya kwenda hatua ya makundi imerahisishwa zaidi.

Kama Yanga ingeshinda dhidi ya Zanaco moja kwa moja ingetinga hatua ya makundi, ikiwa imecheza mechi mbili tu, dhidi ya Ngaya ya Comoro na Wazambia hao tu.

Ni tofauti na msimu uliopita, Yanga ilipolazimika kucheza mechi tatu. Ya awali ilicheza dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius na kuitoa kwa jumla ya mabao 3-0, kabla ya kuivaa APR ya Rwanda na kuiondoa kwa jumla ya mabao 3-2 na hatimaye ikaavana na Al Ahly.

Kama mfumo huu ungewekwa msimu uliopita, ina maana Yanga ingeingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipoitoa tu APR.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limebadilisha mfumo ili kuipa msisimko mkubwa michuano hii mikubwa ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho barani Afrika.

Nadhani hata suala la wadhamini na matangazo ya biashara inaweza pia ikawa imehusika kuifanyia marekebisho michuano hii.

Kwa sasa makundi yote ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho yatakuwa na timu 16 kila moja, badala ya timu nane.

Kila kundi awali lilikuwa na timu nane, sawa na makundi mawili tu kwenye Ligi ya Mabingwa, pia Shirikisho.

Kwa sasa Ligi ya Mabingwa itakuwa na makundi manne, pia Shirikisho.

Ina maana kwa sasa kumekuwa na wigo mpaka. Kinachotakiwa sasa ni timu zetu za Tanzania kuacha kufanya usajili kwa ajili ya Ligi Kuu tu au kumfunga mtani.

Kusajili wachezaji ambao wanaona watawasaidia kwenye michuano hiyo.

Hata wale wa kimataifa, wale ambao wana faida kwenye timu na si wa kukaa benchi.

Kwa miaka ya hivi karibuni, nimegundua kuwa timu nyingi za Kiafrika kwa sasa hazitofautiani sana kwa uwezo wa soka uwanjani.

Ni makosa madogo ya mchezaji mmoja mmoja na mfumo, ndiyo yanayosababisha timu zitolewe, lakini pia ni uwezo wa baadhi ya wachezaji wenye vipaji, pamoja na nidhamu ya maelekezo ya benchi la ufundi ndiyo inayosababisha timu zishinde.

Zamani ilionekana kabisa kuwa kuna baadhi ya timu zilikuwa na uwezo mkubwa kuliko nyingine zinazocheza nazo, lakini kwa Afrika kwa sasa limepungua sana.

Kwa maana hiyo kama timu za Tanzania zikisimama, kukomaa na kujipanga sawasawa kwa mfumo huu mpya, zinaweza kabisa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho kila msimu, labda tu itokee bahati mbaya.

Mfano Yanga, imetolewa kwa mbinde na Zanaco iliyonufaika kwa goli la ugenini, lakini imejikuta ipo kwenye Kombe la Shirikisho.

Hii sasa ni nafasi ya mwisho kwa Yanga, kwani kama itafanya vizuri itarudia rekodi yake ya msimu uliopita na kutinga hatua ya makundi.

Kinachotakiwa kwa viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wa Yanga si kukata tamaa.

Timu hiyo kwa sasa inapitia kwenye kipindi kigumu ikiwamo ukata, lakini si kigezo na kuanza kutupiana lawama.

Maana kuna baadhi ya wanachama na mashabiki wameshaanza kumtupia lawama kocha George Lwandamina, wengine wanawalaumu wachezaji kama Haruna Niyonzima, Vicent Bossou, Donald Ngoma na wengineo.

Huu ni wakati wa kushikana na kuwa kitu kimoja ili kuweza kuvuka kwenye hatua hiyo.