Waraka wangu kwa wanufaika wa IPTL

15Jul 2017
Nkwazi Mhango
Nipashe
Hekaya za Mlevi wa Canada
Waraka wangu kwa wanufaika wa IPTL

BAADA ya juzi kumshuhudia mnufaika mmoja wa mamilioni na mabilioni ya escrew na IpTL, ile kashfa ambapo baadhi ya wapigaji wa ndani na nje ya nchi na baadhi ya wanene kwenye lisirikali walipiga njuluku za walevi kwenye sandarusi,

nimeamua kuwatahadharisha wale wanaodhani wataendelea kufwaidi zile njuluku au fweeza za walevi wakati wanywa ulabu wakiendelea kunyotolewa roho na mikasa itokanayo na umaskini unaosababishwa na udokozi na wizi.

Hii ni baada ya walevi kunituma ninafanya hivyo kabla hawajakwenda wenyewe kugawana kila kitu wababe hawa wanachomilki bila kujali kuwa kinatokana na mshiko huu au mishemishe nyingine.

Katika wale waliolamba bingo kwenye njuluku hizi za walevi ni wakubwa kadhaa akiwamo Bil Gereza aliyeamua kuzitema juzi baada ya kuona joto la kuingia Keko likizidi kupanda huku serikali ikitaka majipu yajitumbue kabla hajayapasuliwa bila kujali yameota kwa vifito au vigogo, akaamua ateme mzigo.

Kwa kufanya hivyo, Bil ameanzisha ngwe nyingine ya kuona wenzake wakizitapika njuluku zetu ili tuzitumie la kupata kanywaji na huduma nyingine za kijamii.

Mshiko wa escrew umenufaisha wengi wakiwamo vigogo na wanasheria wanene wa lisirikali la zamani inaelezwa kiasi cha madufu 1.6 bilioni kilizama mifukoni kwa wabarikiwa.

Sambamba na wazee hao mabingwa wa Sheria au Masadukayo kama wanavyotajwa kwenye maandiko matakatifu , aliyekuwa waziri mmoja wa mambo ya mahekalu na makasiri mwenye cheo cha profwedheha alilamba kiasi hicho hicho.

Jamaa hakuishia hapo, aliwapa marafiki zake Pilato au majaji, makasisi, makuhani hata wafagiaji kutegemea na thamani na umuhimu wa mhusika.

Wapo walioambulia vijesenti kidogo vya kununulia mboga vikaitwa kuwa japo ni mamilioni vilikuwa ni vijisenti vya ugoro.

Kwa hivyo, waliolamba bingo wote walionekana kushabikia ugoro kiasi cha kuhitaji msaada wa jamaa huyu.

Kwa moyo wa huruma chonde chonde natawatahadharisha wote waliopokea mamilioni na mabilioni haya kurejesha mara moja huku wakijipeleka wenyewe lupango kabla ya kuzolewa mzobemzobe na kurundikwa kwenye karandinga na magereza.

Tena nitamshauri mnene awafungulie kesi za makosa ya ‘mauaji ya kukusudia’ kutokana na ukweli kuwa ujambazi huu umeua walevi wengi waliokosa huduma muhimu kama dawa, elimu na hata kufaidi maisha kwa ujumla.

Tukijrejea kwa wapendwa walioshikishwa mshiko napenda kumpongeza mwenzao aitwaye Bill aliyeamua kutema vijisenti vya ugoro.

Inaonekana jamaa kaachana na tabia ya kunusu au kubwia tumbaku hiyo. Je marafiki zangu mnaojijua mnangoja nini au hadi kinukishwe ndipo msituke baada ya kujikuta lupango? Pia nawafahamisha; kurejesha njuluku siyo mwisho wa stori.

Huu siyo wakati wa EPA ambapo mkuu wa nchi,aliwashauri watuhumiwa wa kashfa hii warejeshe mishiko halafu wasamehewe japo wapo waliosuasua kurejesha wakashitakiwa.

Tunajua kuwa jamaa huyu alifanya hivyo ili wasiumbuke waliopunyua njuluku hizi na kuzitumia kujipatia ulaji kisiasa. Mbona mauzauza na ujambazi huu yalianikwa na mwanasheria aitwaye Bhindika aliyesaini uhamishaji wa njuluku za EPA? Tena nichukue fursa hii kumkumbusha Munene atumbue na kufumua kashfa hii bila kumbakiza kiongozi wa genge hili Roast Tamu la Aziz.

Akimaliza hii aende pake UdA kampuni la walevi lililotwaliwa na jamaa mmoja ajiitaye Saimo ambaye hivi karibuni alikabidhiwa mradi mwingine mkali utokanao na njuluku za walevi wa DrT akajitwalie kama alivyofanya kwa UdA.

Nikirejea kwa wanufaika wa Escrew, mjue fika, chini ya utawala wa sasa, rejesheni–na kuonyesha wazi mlivyo mafisadi–halafu mjiandae kwenda lupango kunonihino kwenye mtondoo. Chini ya kanuni hii ya majibu kujitumbua yenyewe, wengi walionufaika na ujambazi huu watakwenda kuimba kwaya korokoroni. Inapendeza siyo?

Ngoma haiishii hapa. Lazima akina Bill na wenzake warejeshe njuluku zetu na interest juu. Maana walikaa nazo na kuzitumia kutengeneza utajiri kinyume cha sheria.

Kwa wale ambao wako kwenye ofisi za umma, kuanzia siasa, dini na magumashi yoyote waachie ngazi kwanza ndipo wapelekwe lupango.

Kwa wale ambao wameisharudisha namba, nitamuomba Mungu awaadhibu huko huko tena kwa nyongeza ya mateso. Natamani kumuona mzee wa vijisenti akimfuata mzee wa ugoro ili wakaimbe kwaya pamoja tena kwa kigabacholi huku kwaya man akiwa mgeni kutoka Asia. Bring back our escrew dosh as soon as possible.

Loo! Kumbe vitu vimepanda hadi ninaongea kimakonde! Tuonane wiki ijayo basi.