Wapiga dili za pembejeo wasome alama za nyakati

13Jul 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Wapiga dili za pembejeo wasome alama za nyakati

MOJA ya changamoto ambazo wakulima walikuwa wakiilalamikia kwa muda mrefu ni kutopelekwa kwa wakati pembejeo za kilimo hata kujikuta wakishindwa kuzalisha mazao mengi hivyo kujikuta wakipata hasara kinyume na matarajio yao.

Licha ya kushindwa kupata pembejeo kwa wakati, changamoto nyingine ilikuwa ni kushindwa kupata mbolea kulingana na mahitaji yao.

Yaani wakati mwingine badala ya kupata mifuko mitatu baadhi walijikuta wanaambulia mfuko mmoja kinyume na mkataba kama wanavyotakiwa bila kufahamishwa na mamlaka husika kwa nini mambo yako hivyo.

Baadhi yao wamekuwa wakitamka wazi kuwa, serikali ina lengo zuri kwao lakini wanaokwamisha nia hiyo nzuri ni baadhi ya watendaji wa kata na vijiji wakishirikiana na baadhi ya kamati za vocha za vijiji au kata kwa kuwaibia wananchi huku wakimhusisha wakala aliyepewa dhamana ya kusambaza pembejeo.

Baadhi ya wakulima katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ni miongoni mwa waliokumbwa na changamoto hizo msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017. Taarifa ilionyesha kuwa, ilitumia pembejeo zipatazo 27,813 kati ya 32,145 zilizopelekwa katika manispaa hiyo.

Taarifa ya Kaimu Ofisa Kilimo Manispaa ya Mpanda, Said Hemed iliyotolewa na Ofisa habari wa Manispaa ya Mpanda, Donald Pius ilionyesha kuwa, matumizi ya pembejeo katika msimu huo hayakutumika ipasavyo na kwa wakati, kwa madai kuwa, Wizara ya Kilimo ilichelewesha pembejeo hizo.

Kama hiyo haitoshi, walisema licha ya kucheleweshewa mbolea na mbegu, bei ya pembejeo hizo ilikuwa kubwa ukilinganishwa na uwezo wa mkulima. Walitolea mfano bei ya mbolea CAN na UREA kwamba iliuzwa kwa Sh.58,000.

Kufuatia tuhuma hizo, mawakala wasambazaji wa pembejeo za ruzuku waliokuwa wakilalamikiwa na wakulima wakajibu lawama hizo na kubainisha kuwa, tatizo la kuchelewa kwa pembejeo siyo lao, na kuinyooshea kidole serikali kwamba inachelewa kuwakabidhi mbolea kwa muda muafaka .

Katika mlolongo huo wa malalamiko, baadhi ya wakulima walidai kuwa, badala ya mbolea walikuwa wakiuziwa kitu kingine kisicho mbolea hivyo kujikuta watumiaji wakishindwa kupata tija katika kilimo chao hata kuathiri maendeleo na ukuaji wa uchumi kwa ujumla

Katika mlolongo huo wa ukwamishaji wakulima kupitia pembejeo, kuna baadhi ya maofisa kilimo waliowahi kukamatwa na vyombo vya dola wakituhumiwa kwa upotevu wa vocha za pembejeo za ruzuku wakati wakizisafirisha kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mikoani.

Kwa ujumla ni kwamba, wakulima wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi zikiwamo hizo nilizozitaja, ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia kukwamisha maendeleo yao katika kilimo.

Nimegusa changamoto hizo zinazowakabili wakulima kwa lengo la kutaka kuchangia kile ambacho Rais John Magufuli amekisema hivi karibuni kuhusu ufisadi na ubadhirifu uliofanyika kwenye matumizi ya fedha za pembejeo.

Dk Magufuli alieleza kuwa, katika mikoa takribani 11 iliyokaguliwa imebainika kuwepo tofauti kubwa ya kilichoandikwa kwenye ripoti na uhalisia wa mambo.

Inaonyesha kwamba, kiasi halisi cha pembejeo kilichotolewa kina thamani ya Sh. Bilioni nane na zaidi.Lakini madai kwa ajili ya malipo yaliyowasilishwa serikalini ni zaidi ya Sh. Bilioni 50 na zaidi.

Hali hiyo ilimshangaza Rais kuona jinsi serikali inavyojitahidi kuhakikisha kuwa, wakulima wanapata unafuu kwa kupewa vocha za pembejeo, lakini kumbe kuna wajanja wachache wanafanya dili hata kusababisha hasara kwa serikali na wakulima!

"Tunafanya uhakiki wa pembejeo za kilimo. Tumegundua hadi sasa madai ya pembejeo ya Sh. Bilioni 50 zilizowasilishwa serikali ni sh bilioni nane ndio madai halali baada ya kufanyiwa uhakiki," akasema Rais .

Dk Magufuli akatoa wito kwa wakuu wa wilaya na mikoa nchi nzima kuwa makini katika matumizi ya fedha za serikali." Hapa Chato fedha za pembejeo zimeliwa zaidi ya Sh. Bilioni moja.Mchezo huu, upo kila mahali, tunafanya ukaguzi wa nchi nzima. Serikali haiwezi kufanya biashara na maskini kuwaacha matajiri wawasumbua maskini," akasema.

Kwa mwendo wa serikali ya awamu ya tano ni wazi kwamba, wale ambao wamekuwa wakiwafanyia uhuni wakulima kuwacheleweshea pembejeo kwa sababu wanazozijua wao ni bora sasa wasome ishara za nyakati.

Watambue kwamba, serikali hii haiwezi kuwachekea ndiyo maana rais amewaumbua wacheza dili baada ya kubaini kuwa, wanaiongezea mzigo wa deni badala ya kiasi halisi ambacho inadaiwa.

Maana yake ni kwamba fedha hizo za ziada walitaka waweke mifukoni mwao na hivyo kuendelea kuiumiza serikali na wakulima, ambao hujikuta hawapati pembejeo kwa wakati hivyo kushindwa kuzalisha mazao mengi.

Sasa kwa vile serikali imeshtukia mchezo huo, nina imani kwamba kila mhusika hataurudia na badala yake afanye kazi yake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria na dhamana aliyokabidhiwa na kuhakikisha kuwa, wakulima wanapata pembejeo kama inavyotakiwa.

Lengo zuri la kuhakikisha kuwa nchi inazalisha chakula cha kutosha na mazao ya bishara ya kutosha kwa ajili ya kuuza ili kupata fedha za kigeni ambazo tunazihitaji sana kwa ajili ya kununulia mashine, mitambo, dawa na mambo mengine muhimu ambayo hayazalishwi nchini.

Ni muhimu kila mtu katika eneo lake kuhakikisha kuwa anafanya kila awezalo ili pembejeo halisi na sio feki zifike kwa wakati na kwa bei halali kuhakikisha kuwa, uzalishaji wa mazao unaongezeka na hivyo kuchangia kuboresha maisha ya wakulima na walaji kwa ujumla