Wananchi tutumie vyema mvua zilizopo

16May 2017
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wananchi tutumie vyema mvua zilizopo

HIVI sasa katika maeneo mbalimbali nchini, vijijini na hata mijini, kuna mvua. Hivyo, ni vyema wananchi wakazitumia kupanda mazao, ili kuondokana na njaa.

Mvua hizo zinazonyesha usiku na mchana, nadiriki kuzieleza zimekuja kwa wakati muafaka, kwa kuwa nchi ilikuwa imekumbwa na uhaba wa chakula, uliosababishwa na uwepo wa jua kali linalozaa ukame.

Miezi michache iliyopita, baadhi ya maeneo nchini, yalidaiwa kukumbwa na njaa. Ni hali iliyobabishwa na kutonyesha mvua kwa muda mrefu.

Wilaya nyingi na mikoani, kulisikika vilio vya wananchi walioomba msaada wa chakula kutoka serikalini, kutokana na mazao waliyopanda kukaushwa na jua.

Nasema, Mungu amesikia kilio cha wananchi hao kwa kuleta mvua ambazo tangu zianze kunyesha maeneo mbalimbali hapa nchini, hadi sasa ni takribani mwezi mmoja.

Kukosekana kwa mvua kulisababisha maeneo mengi kukumbwa na ukame, shida ya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, mifugo na kilimo katika tafsiri yake pana. Lakini mvua zinavyonyesha, zimeongeza upatikanaji wa maji ya matumizi ya nyumbani na hata shambani.

Niwaombe Watanzania wenzangu kuwa makini, kwa kuzitumia mvua hizi kwa manufaa ya kushiriki katika kampeni binafsi za kupanda mazao, ambayo hayachukui muda mrefu kukua, ili waweze kupata chakula cha kutosha na kuondokana na baa la njaa.

Pia, katika namna ya kipekee niwaombe wananchi wanaoishi vijijini, kuzitumia mvua vyema katika kipindi hiki, kupanda mazao ya biashara kama vile pamba, kahawa, korosho ili waweze kujipatia kiipato mwisho wa msimu.

Si hivyo tu, pia ni jukumu la serikali kupitia wenyeviti wa vijiji na serikali za mitaa, kuwahamasisha wananchi wao wapande mazao ya chakula, hususani ambayo ni ya muda mfupi, kama vile mahindi na mpunga.

Aidha, nazikumbusha mamlaka za kiserikali kusaidia kwa wananchi wake kwa ukaribu, sambamba na kushusha bei za mbegu na pembejeo kutoka vyanzo vya kiserikali, lengo ni kuwawezesha wakulima kununua kwa wingi na kwenda kuzipanda shambani.

Mbali na kutumia mvua zilizopo katika kilimo, pia wananchi wanaweza kuzitumia katika upandaji miti, ili nchi iondokane na ukame ulioanza kunyemelea katika baadhi ya mikoa, chanzo kikiwa ni jua lililowaka kwa muda mrefu.

Ni ukweli usiopingika kwamba, hakuna kiumbe kinachoweza kuishi salama, pasipo na mazingira salama, ambayo ni yale yaliyotunzwa kupitia miti inayopendezesha eneo husika ikinyonya hewa chafu na kutoa safi inayotumiwa na binadamu.

Kukosekana mvua, kumesababisha maeneo mengi kuwa na ukame, shida ya maji kwa matumizi ya nyumbani, mifugo na kilimo. Lakini, mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa, zitaongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shambani.

Tanzania ni kati ya nchi zilizoathirika sana na uharibifu wa mazingira, kwa vile watu wanakata miti bila kupanda mingine, kuziba nafasi ya iliyovunwa.

Hiyo inafanya suala la kupanda miti katika kipindi kilichopo, ni suala muhimu na kwa kiwango kikubwa itasaidia kupunguza uhaba wa miti, unaosababisha kuwapo ongezeko la joto na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Hivyo basi, kuna haja ya kila mwananchi aone haja ya kupanda miti, hasa katika msimu huu wa mvua, kwa kuwa kutawezesha miti hiyo kushika ardhini na kuendelea kustawi hata msimu ambao hauna mvua.

Rai yangu kwa Watanzania, ni kwamba watumia mvua zilizopo kwa manufaa ya kushiriki kampeni binafsi ya kupanda miti. Kila anapaswa apande mti na kufuatilia ukuaji wake kila hatua, kwa maana ni wajibu wetu wote, kutunza mazingira. Tuitikie kwa vitendo kaulimbiu ya “kata mti panda miti,” ili kuhakikisha tunayafurahia maisha wakati wote.

Hakuna namna tunayoweza kulisaidia taifa letu kuondokana na jangwa, kadhalika katika utunzaji wa mazingira, bila ya kupanda miti kwa wingi, ambayo itaondoa athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Vikundi mbalimbali navyo vinapaswa kushiriki katika upandaji miti na kufuatilia maendeleo yake, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wengi washiriki kwenye kampeni hiyo.

Miti ina faida nyingi, ikiwamo kutoa matunda mbalimbali, kivuli, kuhifadhi vyanzo vya maji, kusafisha hewa, kupendezesha maeneo. Hivyo, tutafanikiwa kuyafurahia hayo, iwapo kila mmoja kwa nafasi yake, atapanda miti na kufuatilia ukuaji wake.

Wapo wanaoungana kwenye vikundi na kupanda miti, lakini hakuna ufuatiliaji wake bado una kasoro, mtazamo wa ‘bora liende’ umetawala.

Ni vyema viongozi kuanzia serikali za mitaa waonyeshe mfano, kwa kuanzia kwenye ofisi zao na nyumbani, pia kuwahamasisha wananchi kuzitumia mvua kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Hata wahenga washasema ‘miti ni uhai.’