Waliopokea mgawo Escrow waige hatua iliyochukuliwa na Ngeleja

12Jul 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Waliopokea mgawo Escrow waige hatua iliyochukuliwa na Ngeleja

WAZIRI wa zamani wa Nishati na Madini, ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema mkoani Mwanza, William Ngeleja, amerejesha rasmi Serikalini fedha alizozipokea kutoka kwa James Rugemalila, February 12, 2014.

Hizo ni fedha kutoka kwenye mgawo wa Escrow, ambazo ni kiasi cha Sh. Milioni 40.4 akiwa na dhamira ya kukwepa kuendelea kuandamwa na kashfa hiyo.

Kwa kauli yake Ngeleja amenukuliwa akisema kwamba; “Nimeamua kurejesha fedha hizi hata kama aliyenipa msaada bado ni mtuhumiwa tu, kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya kashfa au tuhuma hizo.”

Ngeleja alisema hayo juzi wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari ambapo pia alidai ana zaidi ya miaka 12 akiwa kiongozi wa umma na hajawahi kukumbwa na kashfa ya rushwa au ufisadi.

“Kwa vile sasa imedhihirika kwamba aliyenipa msaada huu anatuhumiwa kwenye kashfa ya akaunti ya Escrow, nimeamua kuchukua hatua. Kupokea msaada ni jambo la kawaida, ila ikibainika kuna harufu ya uchafu hata kama haujathibitishwa na vyombo husika ni vyema kujiepusha nao,” akasema.

Akafafanua kuwa amerudisha fedha hizo ili kulinda maslahi ya nchi yake na heshima ya chama chake, serikali, wana Sengerema, familia yake na heshima yake na kwamba amepima, kutafakari, na kuamua kwa hiari yake mwenyewe, kurejesha fedha hizo serikalini.

Ni hatua nzuri aliyoichukua hasa kwa kuzingatia kwamba amekuwa mtu wa kwanza kufanya hivyo.

Amekuwa ni mtu wa kwanza kufanya hivyo kwa karibu kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa tokea Bunge lije na maazimio juu ya swala hilo, ikizingatiwa kuwa upepo unavyovuma kwa sasa si mzuri baada ya wahusika wakuu wa sakata hilo kupelekwa mahakamani.

Wahusika hao wakuu ni wafanyabiashara Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira ambao wamefunguliwa mashtaka katika Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 12.

Miongoni mwa mashataka hayo 12 ya uhujumu uchumi, yamo mashataka matano ya kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya USD 22, 198, 544.60 na Sh.309, 461, 300, 158. 27.

Wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujihususisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kuisababishia Serikali hasara na kutakatisha fedha.

Bunge lilikuwa na maazimio nane, ambapo la saba lilimgusa Ngeleja na wengine waliokuwa wametajwa kwenye mgawo wa fedha za Escrow, likitaka wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.

Mjadala unaona kimsingi kwamba, kitendo cha Ngeleja kurudisha fedha kina fundisho kwa wanasiasa na watu wengine waliohusishwa na kashfa hii na nionavyo mimi hawana budi kuiga kile alichokifanya.

Wanapaswa kurudisha mgawo waliopewa kupitia akaunti hii ya Escrow ili zitumike kwa shughuli za maendeleo ya wananchi.

Miongoni mwao wapo waliokuwa mawaziri kama Ngeleja na watumishi wengine wa umma.

Aidha, katika watu walioshiriki kwa namna moja au nyingine kwenye kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow pia wamo waliokuwa viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge.

Kila mmoja kwa nafasi yake kama alipata mgawo wa pesa ni vyema akaurejesha hata kama uamuzi huo pengine inawezekana usiweze kumuondoa kwenye mkondo wa sheria, lakini hatua ya aina hiyo inalinda heshima yake.

Ikumbukwe kuwa Maazimio ya Bunge yalikubaliwa pia na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ambaye aliipongeza Kamati ya Bunge chini ya Zitto Kabwe na Deo Filikunjombe kwa kazi nzuri walioifanya.

Ilikuwa Desemba 22, mwaka 2014 wakati akizungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam ambako aliwapongeza wabunge kwa moyo waliouonyesha wa kuchukia maovu na kutaka yashughulikiwe ipasavyo na akawahakikishia kuwa yuko pamoja nao katika maazimio waliyoyafikia.

Lililo kubwa zaidi na ambalo mjadala huu unaliona ni kwamba waliotuhumiwa katika kashfa hii ni vyema wakasoma ishara za nyakati na kuchukua hatua sasa.

Hatua za kurudisha fedha kama alivyofanya Ngeleja badala ya kukaa kimya kana kwamba hakuna mgawo waliopokea kutoka kwenye akaunti hii ya Escrow.