Wakati viwanda vikianzishwa, tupende kununua bidhaa zetu

02Jan 2018
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Mjadala
Wakati viwanda vikianzishwa, tupende kununua bidhaa zetu

MOJAWAPO ya kipaumbele cha Serikali hii ya Awamu ya Tano ni cha Tanzania ya viwanda.

Kwamba serikali ya Rais John Magufuli imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda katika dhima yake ya kustawisha maisha ya Watanzania kwa ujumla wake na kuhakikisha kwamba lengo la kuifanya Tanania nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025 linafikiwa kama ilivyopangwa.

Kimsingi, uwepo wa viwanda utatoa fursa mbalimbali kwa wananchi kama ile ya ajira, changamoto ambayo bado inaendelea kuwa kubwa hadi sasa.

Lakini si ajira tu, bali viwanda vinatarajiwa pia kuwa soko la mazao ya wakulima na ndiyo maana serikali inalenga zaidi kuwa na viwanda vinavyotumia malighafi inayopatikana nchini.

Yaani viwanda vinavyotumia mazao kama pamba, kahawa, korosho, katani, tumbaku na mengineo mengi yanayozalishwa katika sehemu mbalimbali za nchi yetu.

Na kwa kutoa soko kwa mazao yanayozalishwa nchini moja kwa moja kunaboresha kilimo kinachoajiri takribani asilimia 70 ya Watanzania.

Lakini vilevile kwa kuwa na viwanda, serikali inapata kodi inayoihitaji kwa udi na uvumba kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.

Miradi inayohusu huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji, miundombinu, nishati na mingine yenye tija kwa ustawi wa taifa.

Wengi wameunga mkono nia hiyo ya Rais Magufuli na katika kipindi kifupi cha kukaa kwake madarakani, viwanda mbalimbali vimeanzishwa na mashirika, taasisi na watu binafsi.

Mfano hai wa kuitikia wito huo wa Dk. Magufuli kuifanya Tanzania nchi ya viwanda, umeonyeshwa na wadau mbalimbali.

Wadau hao ni pamoja na Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania (TSSA) ambao unakusudia kufufua viwanda 25 vilivyoshindwa kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 baada ya serikali kuvibinafsisha.

Hatua hiyo inalenga mbali na kukuza uchumi wa nchi lakini pia kuibua ajira.

Na ndiyo maana Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF kwa mfano umeweza kufufua vinu vya kusindika nafaka vya Shirika la Taifa la Usagishaji (NMC) vya Iringa, Dodoma na Mwanza vitakavyotoa ajira 30,000.

Lakini si hivyo, ukienda katika mkoa wa Pwani kwa mfano kuna zaidi ya viwanda 300 ambavyo vimejengwa na wadau mbalimbali hadi sasa kwa nia hiyo hiyo ya kuitikia wito wa Rais Magufuli wa kuifanya Tanzania ya viwanda.

Hata hivyo, mjadala unaona kuna suala la msingi ambalo lisiposisitizwa sambamba na kasi hii ya ujenzi wa viwanda, kazi yote hiyo itakuwa na mapungufu.

Na hili pia lilibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Sunshine, Leo Lee, alipokuwa anazindua mafuta mapya ya kula ya Taty Pure Sunflower Oil yanayozalishwa na kampuni hiyo juzi, mafuta ambayo tayari yako sokoni kwa sasa.

Nalo ni la Watanzania kutopenda vya kwao, vinavyozalishwa ndani ya nchi yao.

Mjadala unaungana na mkurugenzi huyo kuwaasa Watanzania kuwa na moyo wa kununua bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyao, badala ya utamaduni wa enzi na enzi walionao wa kupenda vya nje.

Kama alivyowaasa Lee, mjadala pia unaona kwamba kwa kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini, kutasaidia kuimarisha viwanda vya ndani na kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumzia kuhusu mafuta hayo mapya aina ya Taty, Lee alisema yanatengenezwa na Alizeti inayolimwa nchini na yamethibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) baada ya kukidhi vigezo vya ubora kwa afya ya binadamu.

Na kwa kuwa mafuta hayo yaliyo na vitamin A na E yanatengenezwa kutokana na alizeti inayozalishwa nchini, tayari soko la Alizeti yetu inayozalishwa zaidi katika mikoa ya Singida na Dodoma linazidi kuwa la uhakika.

Ni kwa msingi huo mjadala unatoa rai kwa Watanzania, tujenge utamaduni wa kupenda bidhaa zinazolishwa na viwanda vyetu na ambavyo vinaendelea kujengwa, badala ya kupenda vya nje.

Majirani zetu kama Kenya wameliona hili kwa muda sasa na ndiyo maana wanapenda bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyao tofauti na sisi.

Mjadala unaona kwamba wakati Rais Magufuli anapigania uanzishwaji wa viwanda, basi wananchi tupende vinavyozalishwa na viwanda hivyo.