Vijana watumia ‘unga’ wasaidiwe kuondoka waliko

12Jan 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vijana watumia ‘unga’ wasaidiwe kuondoka waliko

SENSA ya mwisho ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa idadi ya Watanzania ni milioni 44.9, Tanzania Bara ikiwa na watu milioni 43. 6 na Zanzibar milioni 1.3, pamoja na mchanganuo mbalimbali ukiwamo wa umri na jinsia.

Mchanganuo huo unaonyesha kuwa katika idadi hiyo ya watu milioni 44.9, vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 wapo milioni 15.1, ambao kimsingi ndiyo wanaoitwa taifa la kesho.

Lakini bahati mbaya, wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi, ambazo kama hazitapatiwa ufumbuzi haraka, vijana hao huenda wasiwe na manufaa kwa taifa lao kutokana na matendo wanayofanya.

Dhana ya vijana ni taifa la kesho maana yake ni kwamba wanaandaliwa kwa lengo la kushika madaraka baadaye, lakini inasikitisha kuona baadhi yao wakijikita kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Ikumbukwe kuwa, viongozi wa sasa ambao ni watu wazima waliandaliwa wakiwa vijana ili kuwa viongozi wa sasa, hivyo vijana wa sasa wasaidiwe ili waachane na dawa hizo, ambazo ni hatari kwa maisha yao.

Ninasema hivyo, kwa sababu tatizo la matumizi ya dawa za kulevya nchini ni kubwa na utafiti unaonyesha kuwa watu 50,000 wameathirika kwa kujidunga sindano na wengine kwa njia ya uvutaji.

Haya yanathibitishwa na daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Kassian Nyandindi na kufafanua kuwa utafiti uliofanywa mwaka 2014 unaonyesha hali hiyo.

Dk. Nyandindi alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa, idadi hiyo ni kwa wale wanaotumia dawa aina ya heroin na cocaine, lakini kuna wengine wanaopatiwa huduma katika kliniki zao wanaotumia bangi, mirungi na pombe.

Anasema, ingawa idadi ya watu walioathiriwa na dawa za kulevya nchini kwa sasa ni 25,000 na waliojitokeza kupatiwa huduma katika kliniki nne zinazotoa huduma hiyo ni 3,500 tu na kuongeza kuwa kiwango cha HIV kwa kundi hilo ni kati ya asilimia 20 na 50.

Kwa mazingira haya, ni kwamba taifa linapoteza nguvu kazi kwa kuwa vijana ambao wanategemewa kuwa taifa la kesho ndiyo wanabobea kwenye ulevi na dawa za kulevya, wanakuwa legelege, hawana msaada hata kwenye familia zao na taifa kwa jumla.

Kuna wakati hata kama walikuwa na kazi, hupoteza ufanisi na kujikuta wakitumia muda mwingi kwa ulevi na ndiyo maana baadhi ya vijana waliovuma kwenye sanaa wamebaki kuwa 'mateja' na hawana faida tena katika jamii.

Maana yake ni kwamba kijana huwa, anabadilika tabia na kama alikuwa na uwezo wa kifedha, huziharibu na kugeuka kuwa mwizi ama ombaomba ili angalau apate japo pesa kidogo za kununulia dawa za kulevya.

Wapo wale ambao huuza vitu vyao kidogo kidogo na hatimaye kumaliza vyote na kujikuta wakiwa hawana kitu kabisa na kubaki wakishinda mitaani ama kwenye vijiwe kwa sababu tu ya kutumia dawa za kulevya.

Baadhi ya vijana wanaotumia dawa hizo wanasema wazi kuwa wamejitahidi kuziacha wameshindwa, hivyo wameona ni bora waendelee kutumia tu. Kama kila anayetumia akisema hivyo maana yake ni kwamba taifa la kesho litakuwa na kundi kubwa la ‘mateja.’

Ingawa inaelezwa kuwa, biashara ya dawa za kulevya ni vigumu kuidhibiti kwa kuwa mtandao wake ni mpana na wa kificho na wadau wake ni watu wazito, bado juhudi zinahitajika kuokoa taifa la kesho, badala ya kuliacha liendelee kuangamia.

Wataalamu wa mambo ya afya wanasema kuwa dawa za kulevya na pombe kali, zinaua taratibu bila ya mtu kujitambua na inawezekana ndiyo maana, vijana wamekuwa wakivichangamkia na mwisho wake wanakuwa hawafai tena katika jamii.

Kila Mtanzania ana sehemu yake katika vita hiyo, ikiwamo kutoa taarifa kwa mamlaka husika inabainika kuwa kuna watu wako sehemu fulani wanauza dawa hizo, vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya.

Inasikitisha kuona, baadhi ya vijana wanaotumia dawa hizo wakipelekwa kwenye vituo maalumu vya kuwarekebisha, lakini wanatoroka na kurudi mitaani kuendelea kutumia dawa hizo, kana kwamba zina faida katika maisha yao.