Ushabiki uliopitiliza haufai

07Jan 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ushabiki uliopitiliza haufai

SHABIKI au mshabiki ni mtu mwenye mapenzi na hamasa kubwa juu ya jambo au kitu fulani. Kwa hiyo ‘shabikia’ ni kitendo cha kuunga mkono jambo au mtu kwa moyo mmoja.

‘Ushabiki’ ni hali au tabia ya kupenda sana jambo au kitu fulani, hali ya kuwa shabiki, tendo la kushabikia. ‘Ushabaki’ ni hali ya kupenda ugomvi, hali ya kuwa shabaki.

Nimeanza ufafanuzi wa maneno hayo ili tuweze kuwafahamu vizuri wanaoshabikia mchezo wa kandanda. Ingawa ushabiki upo duniani kote, huu wetu wa Tanzania umekithiri (kitendo cha kitu, jambo au matendo kupita kiasi; pindukia).

Mashabiki wetu wa kandanda nchini hunishangaza sana. Hawana habari kuwa kandanda ni mchezo wa makosa na bahati. Timu inayoitwa ‘kubwa’ yaweza kufungwa na timu inayodharauliwa hata kuitwa ‘vibonde’ kama isemwavyo na mashabiki.

Hawa ni watu wasiojua kwamba katika mchezo kuna kushinda na kushindwa. Hawajui kuwa timu inayodharauliwa ikutanapo na timu inayosifiwa, wachezaji wa timu inayodharauliwa hutaka kuuonesha umma kuwa wao ni bora kuliko baadhi ya wachezaji wa timu wa timu zinazosifiwa.s

Wachezaji hupeana majukumu ya kupambana kufa au kupona ili kuwavunjia heshima wachezaji nyota. Huambizana kuwakaba wachezaji nyota ili wasiweze kuleta madhara. Kwa mkakati huo, wachezaji mahiri hubanwa kiasi cha kuonekana si lolote.

Itokeapo hivyo, mashabiki, bila kupima hali ya mchezo, huwalaumu wachezaji wao nyota kuwa wanacheza chini ya viwango kumbe wamebanwa na kukabwa vilivyo na wachezaji wa timu inayodharauliwa!

Mara nyingine wachezaji mahiri wanaponyimwa nafasi ya kuchezea mpira kama watakavyo, hughadhibika na kucheza rafu dhidi ya timu inayodharauliwa. Mwishowe haishangazi kuona au kusikia timu yenye wachezaji mahiri imefungwa na timu isiyotarajiwa.

Kwa nini? Ni kwa sababu wachezaji wa timu isiyotarajiwa huwekeana nadhiri ya kucheza kwa bidii bila woga ili kuvunja umaarufu wa wachezaji wanaothaminiwa.

Matokeo yake wachezaji wanaozisumbua na kuzifunga Simba na Yanga, hushawishiwa kwa fedha ili wasajiliwe na timu hizo; nao bila ajizi hunasa kwenye ulimbo. Wachezaji wengi wanaosajiliwa na Simba na Yanga ni wale wanaozisumbua mno.

Karibuni hapa Yanga ilimsajili Emmanuel Martin kutoka timu ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) ya Zanzibar. Alikuwa lulu alipoifunga Yanga kwa mguu wake mabao 2-0 kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Yasemwa “Fedha ilivunja nguu, milima ikalala.” Pesa zina uwezo wa kuivunja milima na vilima. Ni methali ya kutumiwa kupigia mfano uwezo wa fedha. Mtu akiwa na fedha aweza kufanikiwa kufanya mambo ambayo asingeweza kuyafanya wala kudhania kuyafanya.

Sasa tuje kwa mashabiki. Watu hawa wanachotaka kuona na kusikia ni timu zao kushinda tu basi. Ni kweli hakuna anayependa kuona au kusikia timu yake kushindwa. Hata hivyo nakuwa mgumu kukubaliana na mashabiki wanaoshangilia ushindi wa timu yao hata kama inacheza kibabe tena kwa mfumo usioeleweka wala kuridhisha.

Nitashangiliaje bao la mkono au la kuotea ama upendeleo wa dhahiri unaofanywa na waamuzi wasiofuata sheria za kandanda ?

Nitashiriki vipi matusi ya mashabiki wahuni wanaozusha rabsha uwanjani timu zao zinapofungwa kihalali?

Timu inaposhindwa, vifaa vya uwanjani vinavyoharibiwa na mashabiki huhusishwa vipi na hali hiyo? Kama viti vimewekwa ili kukufanya wewe shabiki uangalie mchezo ukiwa umeketi, kwa nini timu yako inapofungwa unag’oa viti na kuvirusha huko na kule? Kwa nini upigane na mashabiki wenzako wa timu pinzani?

Kwani hawajui kuwa “hasira hasara?” Nani asiyejua kuwa hasira huleta hasara? Tusijiruhusu kutwaliwa na hasira au kufanya mambo tunapokuwa tumekasirika kwa kuwa matokeo yake huwa hasara.

Hakuna timu inayoingia uwanjani ili ifungwe. Katika mchezo wowote kuna kushinda na kushindwa kwa hiyo tuwe wavumilivu na waungwana tukubali tunaposhindwa kwani asiyekubali kushindwa si mshindani.

[email protected]
0715 33 40 96