Usafi uzingatiwe kwa wauzaji wa pweza

21Apr 2017
Jenifer Julius
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Usafi uzingatiwe kwa wauzaji wa pweza

ULAJI wa samaki aina ya Pweza umeongezeka kwa kasi jijini Dar es Salaam. Ukitembelea katika vituo vingi vya daladala, utakutana na meza zilizojaa samaki hao pamoja na ngisi, ikiwa imezungukwa na watu wa rika tofauti wanaotafuna kila mmoja kulingana na uwezo wake, kwa vigezo vya hamu na mifuko yao

Mvuto huo unatokana na faida kadha wa kadha kutoka samaki huyo, ikianzia na ladha, pia virutubisho vinavyosaidia mwili kujikinga dhidi ya maradhi kama vile saratani, pumu na kuusaidia mwili kufanya kazi yake vizuri.

Hapo ninamaanisha mambo kama vile kumeng’enya chakula, upumuaji na hata mzunguko wa chakula mwilini.

Mbali na faida hizo za kiafya, pia uuzwaji wa pweza unasaidia kutoa ajira kwa watu katika namna mbalimbali na kuwezesha ongezeko la kipato cha muuzaji anayeweza kujihudumia vyema pamoja na familia yake.

Manufaa hayo yanaenda mbali, hata kwa wote waliosababisha mchakato wa pweza huyo kufika mahali hapo, biashara kufanyika na hata akaliwa na wateja.
Pamoja na faida hizo, lakini katika mantiki ya kiafya, mazingira ya uandaaji wa samaki huyo hadi kufika kwenye kinywa cha mlaji, bado si salama.

Iwapo mtu akibahatika kutembelea kwenye meza zinazouzwa pweza na kulinganisha na msingi wa hoja yangu, ataelewa kwa kina zaidi mantiki ya hicho ninachokizungumzia.

Meza hizo huwa zipo pembezoni mwa barabara au maegesho ya wafanyabiashara za usafiri wa pikipiki, maarufu kama bodaboda. Licha ya kuwa sehemu za wazi, lakini chakula hicho kipo wazi kwa saa zote ambazo kinauzwa.

Mara nyingi wauzaji husika, wanafika na kuwapanga samaki hao kuanzia saa 10.00 jioni na wanafunga biashara zao majira ya mpaka saa nne usiku, kulingana na mahali soko lilipo.

Ukiachilia mbali namna chakula hicho zinavyoachwa wazi na kuingiwa na vumbi litokanalo na nyendo za vyombo vya moto kama magari na bodaboda zipitazo jirani, pia ulaji wake si wa kistaarabu. Mteja anachukua kijiti na kuchagua samaki ampendaye, kisha anachomvya kwenye bakuli lenye pilipili na kumla.

Ni aina ya hatua anazofanya kila mteja, kupitia hatua au nyendo hizo hizo. Yaani bakuli la pilipili lipo moja tu na kila mteja anaingiza kijiti chake humo.

Pia wauzaji wanapokuwa wanawakata samaki hao, huwa wanawashika kwa mikono yao, pasipo kunawa kwanza au kuvaa kitu kinachomkinga katika maadili ya usafi na afya.

Kwa hali hii, ni rahisi kwa wateja kuambukizana maradhi hasa yatokanayo na vivywa kama vile fangasi pamoja na kuharisha na kutapika.

Faida zote hizo nilizoziorodhesha hazitokuwa na maana kama usafi hautozingatiwa kuanzia kwenye hatua ya kuwaandaa, hadi wanapokuwa mezani kwa ajili ya mauzo.

Nasema hivi, kwa sababu kama walaji wakila pweza ambao hawajaandaliwa katika mazingira salama, maradhi yanakuwa jirani nao , hivyo virutubisho vinavyopatikana katika samaki hao havitokuwa na maana katika miili yao.

Ni heri walaji wasitumie kabisa samaki huyo na kukosa virutubisho vyake na wabaki na virutubisho vinavyopatikana katika chakula salama, kuliko kula samaki hao kisha wakapata maradhi kama vile kuharisha, kutapika na kipindupindu na kujikuta wanapoteza kabisa hata virutubisho walivyokuwa navyo kabla.

Shime kwa wafanyabiashara wa chakula hicho,kuzingatia usafi kwenye chakula wanachokiandaa ili kiwe salama kwa walaji.