Ukosefu ajira kwa vijana sharti utafutiwe ufumbuzi

18Apr 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Ukosefu ajira kwa vijana sharti utafutiwe ufumbuzi

WAKATI akiwasilisha hotuba bungeni kuhusu hali ya uchumi mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka wa Fedha wa 2015/2016, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema ni asilimia 9.6 pekee ya wakazi wa Dar es Salaam, ndio walio na ajira licha ya mkoa huo kuwa na viwanda 516.

Dk. Mpango akasema kuwa Dar es Salaam inamiliki asilimia 29.2 ya viwanda vyote vilivyopo nchini, ikifuatiwa na mkoa wa Arusha wenye viwanda 144 (asilimia 8.1), Shinyanga 101 asilimia 5.7, Kilimanjaro 96 (asilimia 5.4) na Mwanza 88 (asilimia tano).

Waziri huyo akanukuu utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa mwaka 2014 na kusema kuwa watu wenye ajira jijini Dar es Salaam walikuwa ni 1,927, 367, ambao ni sawa na asilimia 9.6 ya wakazi wote wa jiji hilo.

Akataja maeneo mengine ya mijini kuwa yana idadi ya watu wasio na ajira 5, 131, 422, sawa na asilimia 25.6.

Kwa upande wa maeneo ya vijijini, Dk. Mpango akasema kuwa watu 12, 971, 350, sawa na asilimia 64.8, hawana ajira.

Waziri alisema hayo huku takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) za mwaka 2014 zikionyesha watu milioni 200 miongoni mwa wakazi wa nchi za Afrika ni vijana wa umri kati ya miaka 15 na 24, na idadi ya vijana wasio na ajira barani humu ni mara mbili zaidi ya watu wazima.

Hizi ni takwimu zilizotolewa kwenye Kongamano la Ukosefu wa Ajira na Madhara yake Barani Afrika lililofanyika jijini Dakar nchini Senegal, likishirikisha maafisa kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika.

UN inasema kuwa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana unawafanya washawishike kujiunga na makundi yenye misimamo mikali.

Na ukatolea mfano wa hali hiyo kama unavyoshuhudiwa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Nigeria na Mali.

Kwamba vijana wasio na ajira huwa wanashawishiwa kujiunga na makundi hayo kwa kulipwa, lakini pia kitendo cha kukosa matumaini ya kuboreshwa hali ya kiuchumi ya vijana na utendaji mbovu wa serikali ndio sababu kuu ya kujiunga na makundi hayo.

UN ikabaini idadi kubwa ya vijana barani humu ambao hawana kazi ni hatari kubwa kwa amani na utulivu na kuonya kwa kuzitaka nchi husika zitafute njia za kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

Ikashauri kuwa vijana wasaidiwe sambamba na kubadilisha hali ya sasa kwa kuandaliwa mustakabali mzuri zaidi, na ikazitaka serikali kulipa kipaumbele tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Nimejaribu kueleza kwa kirefu changamoto hii ya ajira kwa vijana kwa vile ni bomu iwapo halitapatiwa ufumbuzi utakaowezesha vijana kuajiriwa ama kujiajiri.

Hizi ni takwimu zilizowasilishwa bungeni na Dk. Mpango kuhusu Hali ya Uchumi Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka wa Fedha wa 2015/2016.

Kwa upande wa Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa watu milioni 20 hawana ajira, hali ambayo imekuwa ikisemwa kuwa hilo ni bomu ambalo linatakiwa kuteguliwa mapema kabla halijalipuka.

Hivyo ni bora uwepo mpango mahsusi wa kukabili tatizo la ukosefu wa ajira.

Baadhi ya vijana wamekuwa wakiilaumu serikali kuwasahau na kuwaacha bila ya shughuli za kufanya.

Mpango mahsusi utasaidia kuwaepusha kushinda vijiweni au kujiingiza katika makundi yenye misimamo mikali.

Ninajua serikali ilishatoa takwimu zinazoonyesha kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana nchini Tanzania umepungua kwa asilimia mbili, kutoka asilimia 13.7 mwaka 2012 mpaka asilimia 11.7.

Binafsi ninaamini hatua ya kuwa na mpango mahsusi ikitekelezwa kwa vitendo itasaidia.

Aidha kuna umuhimu wa kuwaelimisha vijana watambue kuwa ajira zipo za aina nyingi, na si lazima mtu aajiriwe serikalini, kwenye mashirika ya umma au sekta binafsi, bali kijana anaweza kujiajiri mwenyewe.

Ninasema hivyo kwa sababu wapo baadhi ambao hudhani kwamba ajira ni lazima iwe ni katika maeneo hayo tu.

Kumbe mtu anaweza kuwezeshwa akajiajiri na kuendesha maisha yake vizuri.

.