Uchaguzi CCM usihusishe wanachama hewa, kadi feki

19Apr 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uchaguzi CCM usihusishe wanachama hewa, kadi feki

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kilitarajia kuanza uchaguzi wa viongozi wake kwenye ngazi ya shina, ambao ni maarufu kama wajumbe wa nyumba kumi, Jumatatu wiki hii na kisha utafuatia wa ngazi niyngine.

Uchaguzi huo wa nchi nzima utaendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu na utafuatia wa ngazi ya tawi mwezi ujao na kisha zitafuata ngazi nyingine hadi zikiwamo za kata, wilaya hadi taifa.

CCM inafanya uchaguzi wa viongozi wake huku kukiwa na angalizo ambalo lilitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais John Magufuli kwamba hataki utawaliwe na 'figisufigisu'.

Mwenyekiti huyo alishasema kuwa hataki mwanachama apate uongozi kwa kutoa rushwa bali apate kwa uwezo wake wa kuongoza na kwamba watakaokiuka maelekezo hayo hata kama watashinda watavuliwa uongozi.

Kikubwa ambacho wanachama wanatakiwa kuzingatia kauli mbiu ya 'CCM Mpya, Tanzania Mpya', ambayo wenye chama wanasema kuwa inalenga kuleta mabadiliko si ndani ya CCM tu bali pia kwenye maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama kuwapo kwa wanachama hewa na kadi feki za CCM na kusababisha kuwapo makundi ya chama hicho tawala.

Baadhi ya wanachama walikuwa wakidai kuwa wapo wenzao wenye pesa ambao walikuwa wakisaka uongozi hata kwa kununua wanachama hewa na kadi feki ili wafanikishe ushindi.

Mara baada ya wanachama hewa wakiwamo wa vyama vya upinzani kupiga kura inasemekana walikuwa wakichana ama kutupa kadi hizo za CCM (feki) kwa vile zilikuwa umuhimu tena kwao.

Lakini ninaamini kwamba kwa CCM hii wenye mchezo wa aina hiyo hawatakuwa na nafasi kwani mianya hiyo ni kama imezibwa na mwenyekiti wa chama, ambaye tayari ameshatoa maelekezo ya kupata viongozi bora.

Kinachotakiwa sasa ni wenye mchezo huo kukubaliana na hali halisi ili wasije wakaukumbuka kwenye uchaguzi huo hasa kiuanzia ngazi ya matawi na kuendelea, kwani huku kweye mashina hakuna changamoto kama hizo.

Mimi ninaamini kwamba uchaguzi ndani ya CCM bila 'figisufigisu' inawezekana iwapo wahusika watazingatia maelekezo ambayo tayari wameshapewa kwani lengo ni kurudisha chama kwenye hadhi yake ya zamani.

Wakati akiongoza Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kilichofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli alitaja mambo kumi ambayo angeanza nayo kama mwenyekiti wa chama.

Miongoni mwa hayo ni vita dhidi ya rushwa, kuwa CCM ni miongoni mwa taasisi zinazotuhumiwa kwa mianya ya rushwa hasa kipindi cha uchaguzi ndani ya chama au serikali.

Kwamba atahakikisha hakuna kiongozi atakayechaguliwa kwa kutoa rushwa.

Kati ya mambo hayo kumi lilikuwamo la usaliti ambalo limeshashughulikiwa na tayari wapo makada waliovuliwa uanachama, wengine kuonywa kwa vitendo hivyo ndani ya chama.

Alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwapo kwa wanachama wasio waaminifu ndani ya chama, ambao hatari, hivyo akachukua hatua hizo ili kubaki na wanachama wa kweli.

Akasisitiza kwamba anataka chama kinachoongoza wananchama na si wananchama au mwanachama anyeongoza chama na kufafanua kuwa mwanachama ndiye anapaswa kukifuata chama na si chama kumfuata mwanachama au wanachama wachache.

Kwa maana hiyo ni kwamba wale ambao walikuwa wamezoea kutoa chochote ili wachaguliwe na wasipochaguliwa wanahama ili wafuatwe na wapambe wao hawana nafasi tena katika CCM ya sasa.

Kimsingi alichokisema ni sahihi kwa sababu kuwa na wanachama wa aina hiyo ni kuyumbisha chama, hivyo watakaochaguliwa wawe ni wale ambao wamekidhi vigezo ambavyo havihusiani na pesa zao.

Chama imara ni kile chenye mizizi kuanzia ngazi za chini, lakini viongozi wake wakiwa ni wale ambao hawatokani ya rushwa bali wachaguliwe kutokana na sifa zinazotakiwa ukiwamo uwezo wa kuongoza.

Hayo yakizingatiwa ni lazima CCM itakuwa imara kuanzia ngazi za shina, tawi, kata, wilaya, mkoa hadi taifa, hivyo niwatakie CCM uchaguzi mwema viongozi unaoendelea sasa ili wapatikane wale wanaotakiwa.