Tuwe wazalendo ili fursa za kiuchumi zinufaishe taifa

22Nov 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tuwe wazalendo ili fursa za kiuchumi zinufaishe taifa

TAFSIRI au maana ya neno uzalendo inaelezwa na wataalamu wa lugha ya Kiswahili kuwa ni tabia ya kuipenda sana nchi hata kuifia na kwamba sio kila raia katika nchi au taifa anaweza kuwa mzalendo.

Wanafafanua kuwa mtu ambaye ni mzalendo kamwe hawezi kusaliti nchi yake, bali atajitahidi kuijenga, kuilinda na kuitumikia kwa uaminifu hadi kufa kwa manufaa ya nchi yake hiyo.

Kwa maana nyingine ni kwamba kukosekana kwa uzalendo husababisha watu mbalimbali katika jamii kutenda mambo ambayo hushangaza na kuacha wengi wakijiuliza kama mtu fulani anaipenda nchi yake!

Baadhi ya matendo, ambayo yanatajwa kwamba yanachangiwa na ukosefu wa uzalendo ni utoaji rushwa, upokeaji rushwa, upoteaji wa tamaduni, mtu kutojiamini kama Mtanzania na mengine mengine ya aina hiyo.

Ukosefu wa uzalendo unaelezwa kuwa unaweza kusababisha umaskini katika nchi nyingi na hasa za Kiafrika, ambazo wananchi wake wanadaiwa kukumbatia matendo ambayo sio ya kizalendo.

Ikumbukwe kuwa tabia ya uzalendo ina athari kubwa katika kuchochea maendeleo ya mtu binafsi na nchi yake kwa ujumla na humsukuma mtu kuithamini na kuionea fahari nchi yake, vitu ambavyo ni chachu na muhimu kwa maendeleo na pia uzalendo humfanya mtu kuitakia mema nchi yake.

Bahati nzuri viongozi wa nchi hii wamekuwa wakihimiza uzalendo kwa sababu wanajua kuwa wapo baadhi ya watu, ambao wanashirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kufanya udanganyifu katika biashara kwa kuwauzia wananchi bidhaa zilizo chini ya kiwango cha ubora, kuwapunja katika mizani au kuwauzia kwa bei ya juu kupita kiasi.

Wanasahau au hawajui kwamba kuipenda nchi ni kufanya kila jambo ambalo kwa namna moja au nyingine litakuwa ni sababu ya kuletea maendeleo, heshima, kuilinda dhidi ya maadui wake, kuhifadhi, rasilimali zake kwa faida ya kizazi hiki kilichopo na kijacho.

Nimeona nizungumzie uzalendo kutokana na yale yanayoendelea kuibuliwa na serikali yakidaiwa kufanywa na watu ambao wameaminiwa na serikali, kwa sababu yameonyesha kuwa wahusika hawana uzalendo kwa nchi yao.

Kuna baadhi ya watu walioaminiwa na kupewa dhamana kubwa ya kusimamia taasisi mbalimbali zikiwamo za serikali, ambao sasa wamekuwa wakitumbuliwa kwa makosa, ambayo yanaonyesha kwamba hawana uzalendo.

Mimi ukiniuliza jambo langu ambalo ninalipa kipaumbele nitakuambia kuwa ni uzalendo, uzalendo, uzalendo, kwa sababu ninaamini kuwa unaweza kusaidia nchi kwenda vizuri na tena iwapo kila mmoja atakuwa nao.

Hivi karibuni akiwa nchini Canada, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka Watanzania waishio nchini humo wadumishe mshikamano wao na wawe na uzalendo kwa taifa lao.

Majaliwa akasema kuwa kila Mtanzania anapaswa ahubiri utaifa wake na pia wakati wote waringie nchi yao na wanapotakiwa kuisemea nchi yao waisemee vizuri kama ambavyo wengine wanavyosemea vizuri nchi zao.

Akawakumbusha kuwa serikali inawasisitiza wananchi wake hasa waishio nje ya nchi, wawe wazalendo na washirikiane kuhakikisha wanazitumia fursa za kimaendeleo vizuri kwa ajili ya manufaa ya nchi yao.

Wito huu unafaa pia kwa kila mmoja wetu hasa kwa kuzingatia kwamba wapo waliofanikiwa kupata fursa na kuzitumia kwa manufaa yao wenyewe ikiwa ni hata kwa kuiba au kuingiza bidhaa bandia, ili mradi wafaidike tu bila kujali afya za wengine.

Kwa ujumla, mtu mwenye tabia za aina hiyo sio mzalendo, kwani ni wajibu wa kila Mtanzania kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo kwenda mbele, hakuna mtu mwingine wa kufanya kazi hiyo bali ni Watanzania wenyewe.

Kama nilivyosema awali, kwa wafanyabiashara wazalendo katika biashara zao hawawezi kufanya udanganyifu kwa kuwauzia wananchi wenzao bidhaa zilizo chini ya kiwango cha ubora, hawapunji katika mizani, hawauzi kwa bei ya juu kupita kiasi.