Tutegemee nini kwa Yanga leo?

15Apr 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Uchambuzi
Tutegemee nini kwa Yanga leo?

‘UADUI’ ni hali ya watu kuchukiana na kutendeana maovu; uhasama. Ndivyo zilivyo Simba na Yanga kwani hakuna moja inayotaka kuona maendeleo ya nyingine ingawa wote wapo mkoa mmoja katika nchi moja --Tanzania!

‘Utani’ ni maneno au vitendo vya dhihaka; mzaha. Tabia ya watu kufanyiana masihara kwa lengo la kuambiana kweli au kuimarisha uhusiano wao. Sivyo walivyo wanachama na mashabiki wa Simba na Yanga. Kile kiitwacho ‘watani wa jadi’ hakipo abadan.

Timu hizi huombeana mabaya, hufanyiana hiana (tabia ya uchoyo) na kuoneana gere (choyo kinachotokana na husuda). Hakuna moja inayopenda kuona mafanikio ya nyingine ila hufurahia sana maanguko ya nyingine!

Zafaa kuitwa ‘mahasimu wa jadi’ badala ya watani wa jadi kwani utani haupo ila chuki na kuhasimiana kila uchao. Zapeana zamu tu -- leo Msimbazi, kesho Jangwani -- katika kile kilichosemwa na wahenga kuwa “Akumulikaye mchana usiku atakuchoma.”

Ni methali ya kutumiwa kuwatahadharisha binadamu dhidi ya watu waliowahi kuwatendea uovu kuwa wakipata nafasi wanaweza kuwaangamiza. Katika hili, kwa Simba na Yanga si ajabu kwani ni jambo la kawaida kabisa.

Kisha twasema kandanda la Tanzania linakua?
Simba ilikwenda Kagera kucheza na timu ya kampuni ya kiwanda cha sukari, Kagera Sugar FC kwenye duru la pili la Ligi Kuu ya Vodacom. Bila kutazamiwa, Simba ikafungwa mabao 2-1.

Hata hivyo Simba ililalamika kuwa Kagera ilimchezesha mchezaji Mohammed Fakhi aliyeonyeshwa kadi tatu za njano katika michezo iliyopita, hivyo kuomba ushindi wa alama tatu na mabao matatu kama ilivyo sheria.

Kabla ya kamati husika haijatoa uamuzi wa madai ya Simba, uongozi wa Yanga ukasimama kidete (yenye kuwa imara katika kufanya au kusimamia ufanyaji wa jambo) kupinga madai ya Simba!

Madai ya uongozi wa Yanga ni kwamba eti (neno la kuonyesha shaka ya jambo au kutokuwapo uwezekano) Kamati ya Saa 72 isikubali kuwapa Simba ushindi, kwani ikifanya hivyo itaiathiri Yanga kutetea ubingwa wao!

Timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ni 16. Simba na Yanga ni timu mbili kati ya hizo. Hata kama zikitoka, zitabaki timu 14 na Ligi Kuu itaendelea bila wasiwasi. Kama ni kutikisa kibiriti kwa Kamati ya Saa 72, tutaona kama njiti zimejaa au la.

Pamoja na ukweli huo, eti Yanga yasema Simba ikipewa ushindi dhidi ya Kagera, itaathiri utetezi wa ‘ubingwa wao!’ He! Ishakuwa ubingwa ‘wao’ wakati ubingwa waweza kutwaliwa na timu yoyote kati ya nne zinazoongoza kati ya 16 zinazoshindania ubingwa huo?

Simba nao wanapoona Yanga ipo kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa huifanyia visa alimradi isifanikiwe kukamilisha malengo yake. Ni kufanyiana ubaya ubaya tu yaani ‘kutesa kwa zamu’ kama wasemavyo vijana wa mjini.

Nilipata kuandika kuwa hata vilabu vya soka nchini vyapaswa kulaumiwa kwa kutoweka kumbukumbu ya mambo yanayotendeka viwanjani. Kadi za njano na nyekundu wanazooneshwa wachezaji wao na idadi ya wachezaji wanaotolewa nnje ya uwanja kwa mchezo m-baya.

Hufika mahali nikajiuliza: wale wanaoitwa ‘benchi la ufundi’ huwa na kazi gani viwanjani? Huenda kushangilia timu zao tu bila kutazama makosa wanayofanya wachezaji wao na kuyaweka katika kumbukumbu ili baada ya mechi wazungumzie makosa hayo?
Vilabu vyetu vya kandanda huchukulia mambo kwa wepesi sana. Viongozi wengi wanaochaguliwa kuviongoza vilabu hawana wajualo katika uongozi wa vilabu ila wanachojali ni ushindi na hela tu basi.

Nadhani sasa ni wakati muafaka viongozi wanaogombea nafasi hizo kwenye vilabu vya kandanda nchini wawe na CV (maelezo binafsi ya mtu kuhusu elimu, ujuzi, uzoefu n.k.) ya nafasi wanazoomba.

Wengi hukimbilia kuomba nafasi hizo ili kujinufaisha kwa hela zinazoingia vilabuni na wakati huohuo kujitafutia umaarufu miongoni mwa jamii ya wapenda kandanda.

Katika mambo mengine, makala kabla Yanga haijacheza na timu ya MC Alger ya Algeria Uwanja wa Taifa, niliwatahadharisha wachezaji kuwa makini. Niliwataka wafunge mabao yasiyopungua matatu ili kuwarahisishia kwenye mechi ya marudiano kule Algeria.

Papara walizofanya Uwanja wa Taifa ziliwakosesha mabao mengi na kuambulia moja tu baada ya kukosa mabao yasiyopungua matano ya wazi kwa kutokuwa watulivu.

Leo huko Algeria, wenyeji watashambulia tangu mwanzo na kuwatia Yanga kiwewe. Hiyo itawafanya Yanga warudi kulinda lango lao na itakuwa hatari. Wenyeji wakipata bao la kusawazisha, itakuwa vigumu kwa Yanga kusonga mbele. Mwamuzi ni dakika 90 za mchezo.
[email protected]
0715/0784 33 40 96