Tusibweteke na kuota kuajiriwa serikalini

18Apr 2017
Faraja Ezra
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tusibweteke na kuota kuajiriwa serikalini

LICHA ya serikali kuleta fursa nyingi za ajira nchini ikiwemo kupitia mlango wa pili, bado ukosefu wa ajira hizo umekuwa kilio kikubwa kwa vijana wengi, kwani njia mojawapo muhimu ya kujikwamua kiuchumi katika suala zima la maendeleo.

Ziko fursa nyingi za kazi, lakini kutokana na uelewa mdogo wa fikra, wanajamii kila siku tunailalamikia serikali kuhusiana na ukosefu huo wa ajira nchini.

Vijana wengi hivi sasa wapo mitaani wakisubiri kuajiriwa, hususan kwa wahitimu wa vyuo mbalimbali na hasa wasomo zaidi kutoka vyuo vikuu.

Kila wanapomaliza masomo, wanakiwa na mataarajio ya kupata kazi nzuri, jambo ambalo mara nyingi huwa kinyume, kwani wanajikuta wanasota mitaani.

Wengi wanaitupia lawama serikali katika suala la kuwatafutia fursa za kazi, pindi wanapomaliza masomo. Wanahitaji serikali ichukue jukumu la kutatua matatizo hayo na iwatimizie ndoto zao.

Wapo baadhi wamekuwa wakijishughulisha na kazi mbalimbali, katika kipindi wanasuburi ajira zao na wakati mwingine ajira zinachelewa kuwafikia na wanaishia na kupoteza kabisa matumaini yaliyopo ndani ya subira.

Kisichoeleweka kwa wengi ni kwamba, kukosa ajira hakumaanishi kwamba ni ulingo wa kukata tamaa ya maisha, hata wakaamua kukaa mtaani. Kimsingi, nasema kwa hilo wanalokumbana nalo, bado hakijaharibika kitu. Fursa zipo nyingi tu za kujiajiri, tofauti na kuajiriwa serikalini au kwingineko kunakofanana nako.

Mtu anaweza kujiajiri kwa namna nyingi, ili ajikwamue kiuchumi kupitia kujishughulisha na biashara za viwango na aina tofauti, hata kama ni biashara ndogo kama vile kununua na kuuza bidhaa za ujasiriamali.

Pia, kuna wengi wamejikita katika michezo, jambo ambalo liwanawapa pesa na katika ulimwengu wa sasa na ajira nyingine. Huko nako wananufaika na kuonekana kuwa na maisha bora.

Kujishughulisha na kilimo, pia ni fursa nyingine inayojitegemea, japo kuna ukweli kwamba vijana wengi hawakipendi sana kilimo, kwa hisia ni kazi ngumu, bado kuna ukweli kwamba, hiyo ni nguzo mojawapo ya uchumi wa dunia, hata kufikia hatua tulio nayo leo nchini.

Hivi sasa vijana wengi wanaonekana kukwepa kazi zinazoonekana ngumu kwao.

Wanakimbilia kazi nyepesi kulingana na uwezo wao, huku kuna kundi la wanaoshindwa kutokana na miili yao kuonekana minene au mikubwa zaidi, kuliko uhalisia wa umri walio nao kwa kuiendekeza.

Turejee kaulimbiu ya Rais Dk. John Magufuli ya ‘Hapa kazi tu’ kwamba imetoa hamasa  kubwa kwa Watanzania, kwamba serikali anayoiongoza ya awamu ya tano, imejikita zaidi katika ‘kuchapa  kazi.’ Kwa walio wavivu, hilo nalo linaonekana kuwakwaza.  

Inasadikika kuwa wapo wanaoshidwa kufanya kazi hizo, kwa kuwa na  miili minene inayosababishwa na aina ya vyakula wanavyokula, ikiwa na mafuta mengi yanayochanganyika na kemikali.

Pamoja na hayo, kuna kundi la vijana hasa wa kiume wanaokijihusisha na matumizi mabaya ya dawa za kulevya, sambamna na kuuza.

Kuna wanaokaa vijiweni kutwa nzima bila ya kuwa na kazi maalumu. Wapo wanaojitisa katika tabia ya aibu ya kuwa ‘Mashoga wakitetea mwenendo huo kwa dai “ni kwenda na wakati.’

Vilevile kuna vijana wa kike wanaofanya biashara haramu ya kijiuza miili yao, ili kujipatia pesa ya kujikimu kimaisha. Mwishowe wanapoteza nguvu ya taifa kwa vijana wengi  na kusababisha ongezeko la maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Kuepukana na matatizo hayo kwa kijana wa leo, anastahili kujishughulisha bila ya kuchagua kazi, ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuwa na maisha mazuri ya baadaye.

Serikali inapaswa kuwatafutia nafasi za ajira na hasa kwa wanaohitimu kutoka vyuo vikuu, ili kuwatimizia ndoto zao kwa kufanya hivyo, pia inatia hamasa hata kwa wengine wenye maono ya kufikia elimu ya juu.

Tusiwe na mtazamo mmoja wa kuajiriwa pekee serikalini kila tunapomaliza masomo, bali tupanue fikra ya kujiajiri unapofika wakati muafaka wa kujitegemea.

Ieleweke kuwa, matatizo hayo hayako kwa vijana tu, bali hata wa rika tofauti.

Hilo nalo kwao ni mtihani wa kimaisha, jambo linalowasukuma katika umaskini, kama lisipochukuliwa hatua sahihi.