Tusibweteke, ajira iko shambani

06Jan 2017
Halfani Chusi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tusibweteke, ajira iko shambani

KILIMO kimegawanyika katika sehemu kuu mbili. Kilimo cha mazao ya biashara ambacho ni cha kipato cha fedha na kile cha chakula,kwa ajili ya lishe ya kila siku.

Aina ya kilimo ambacho mtu analima kwa lengo la kujipatia kipato, inaweza kuzalisha vitu visivyoliwa, kama vile tumbaku na bidhaa zinazoliwa kama vile vitunguu na nyanya na mboga.

Nikisema katika lugha nyepesi, ni sehemu ya ajira inakotoa fursa kwa Watanzania wengi, wanaoweza kunufaika na kilimo, katika sura ya ujasiriamali, uwakala au kujihusisha moja kwa moja na uzalishaji shambani. Ni sekta inayoajiri katika sura pana.

Kwa kurejea kinachoendelea katika maisha ya kila siku, kuna baadhi ya watu wanaolia wakilalama kuhusu ugumu wa maisha ya kila siku, kwamba hawana ajira na hasa sehemu za mijini.

Wanakuwa wakilalama na kubakia tegemezi kwa jamaa zao na taifa kwa jumla.

Sababu kubwa inayowafanya watu hao kukaa bila ya kazi mjini, ni kwamba wengi wanashindwa kujihusisha na masuala ya kilimo.

Kisa? Baadhi uvivu ni asili yao na wengine hawajui wakitawaliwa na dhana hawaelewi ni wapi pa kuanzia, katika kujihusisha na kilimo, hususani cha mazao ya biashara ambayoyanaweza kumpatia mtu kipato.

Wataalamu wa kilimo cha mazao ya biashara, wanasema zao la kitunguu ni kati ya zenye gharama nafuukatika kulizalisha, wakati katika upande mwingine, lina thamani kubwa.

Inaelezwa kuwa, linapokuwa sokoni, zao hilo linachukua muda wa takribani miezi miwili na nusu tu kukomaa, tangu linapopandwa
Kuna baadhi ya hatua ambazo wataalamu wanaziainisha zifuatwe kwa mtu mwenye mawazo ya kulima zao la biashara kama kitunguu.

Kuandaa shamba ni hatua ya kwanza, ambayo mkulima wa kitunguu atatakiwa kuitumia kwa kuandaa shambalenye ardhi isiyo na mfinyanzi wala tifutifu.

Inadaiwa kuwa, udongo wa mfinyanzi na tifu tifu huchoma mizzi ya kitunguu wakati wa jua kali

Kuandaa miche ni hatua ya pili. Hapo wataalamu wanasema kuwa, kitungu hupandwa kwa mfumo kama wa zao la mpunga.

Mara baada ya miche inapokomaa, kutoka kwenye kitalu, miche hiyo huchukua takribani mwezi mmoja na 12 hadi kufikia kupandwa
Kuandaa vijaruba vya kupandia miche ndiyo hatua inayofuata.

Miche ya kitunguu ikishakomaa toka kwenye vitalu, hupandwa kwenye vijaruba vidogo na kuanza kupata matunzo hadi kukomaa, kufikia kupata kitunguu kamili

Tukumbuke kuwa, matunzo hayo ni pamoja na kumwagilia maji kila baada ya wiki mbili, kutia mbolea na kupiga dawa za wadudu,ukungu na kutu.

kama inavyofahamika, chochote kizuri kina hitaji matunzo

Hivi hapo naomba kuhoji, jamani kuna haja gani ya mtu kukaa bila ya kazi mjini, wakati vijijini kuna mashamba mazuri ya kulima mazao ya biashara na mtu akajipatia kipato?

Kwa mtazamo wangu, kilimo siyo kwa mtu asiye na kazi tu, bali hata kwa mtu mwenye ajira, anaweza kujihusisha na kilimo, kwani huyu tayari anakuwa na mtaji wa kumwezesha kufanya kilimo kirahisi.

Hivyo basi, ni bora kwa mtu mwenye kazi na asiye na kazi wote wajihusishe na kilimo, kwani kupitia kilimo kuna baadhi ya watu wamepata mafanikio makubwa.

Kitunguu kwa maelezo ya mtaalamu wa kilimo, mtu anaweza kupata pesa nyingi. Mpaka sasa, kuna mamilioni ya watu vijijini wainue mafanikio makubwa kupitia kilimo cha biashara na mazao mengine kama vile, mfano nyanya,bamia na mboga tofauti.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu:
+255 787879707