Tuache siasa kwenye mambo ya msingi

12Jul 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tuache siasa kwenye mambo ya msingi

NENO siasa ni miongoni mwa maneno ambayo ni maarufu sana midomoni mwa watu kwa sababu kimsingi linagusa karibu katika kila nyanja ya maisha yao.

Na umaarufu wa hili neno kwa Watanzania huenda uko juu zaidi pengine karibu kuliko nchi nyingi zinazotuzunguka.

Hii ni kwa sababu kwa miongo mingi katika awamu zilizopita takribani kila kitu kilichukuliwa kuwa ni siasa ukiacha kipindi hiki cha serikali ya Awamu ya Tano ya Dk. John Magufuli.

Tafsiri potofu ya siasa ilisababisha mambo ya maendeleo yasisonge mbele.

Ndiyo maana hata miradi ya kujitolea au kuchangia ujenzi kama zahanati au darasa wakati mwingine ilikwama.

Ilikwama kwa sababu kuna watu walikuwa wakijitokeza na kuleta siasa za fitna wakiwaambia wananchi hawana sababu ya kuchangia ujenzi wa zahanati au darasa kwa sababu hiyo ni kazi ya serikali.

Siasa aina hiyo ndiyo iliyoleta maovu ya ufisadi na wizi karibu katika kila nyanja na idara za serikali.

Watumishi hewa, wanafunzi hewa, watumishi waliotumia vyeti visivyo vyao kupata ajira, vyeti vya kughushi na maovu mengine ni matokeo ya kuchukulia kila kitu kuwa ni siasa.

Kwamba badala ya tafsiri inayokubalika ya siasa kuwa njia ya kufanya maamuzi kutokea ngazi ya chini kwa maana ya kitongoji ama mtaa hadi ngazi ya taifa ama kimataifa, inatafsiriwa katika njia inayokwamisha kila lengo la kuboresha maisha ya watu.

Kwamba badala ya siasa kuchukuliwa kama sehemu muhimu ya majadiliano ya maendeleo na hoja kati ya watu mbalimbali, serikali na serikali au serikali na vyama vya upinzani kwa lengo la kupata ufumbuzi wa hoja iliyo mezani, inachukuliwa kama turufu ya kutafuta umaarufu wa kisiasa ambao wakati mwingine hauna mashiko.

Muungwana anaona awamu hii ya tano inathibitisha kwamba zama za siasa kuingizwa katika kila kitu hata kwa miradi yenye mashiko, zimepitwa na wakati.

Mojawapo ya eneo ambapo serikali ya Dk. Magufuli imeonyesha kwamba siasa hizo hazina mashiko tena ni kwenye mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa maji kwenye Maporomoko ya Stiegler yaliyo katika Hifadhi ya Taifa ya Selous.

Kama ilivyokuwa kwenye sakata la makinikia, kulijitokeza watu baada ya Dk. Magufuli kutamka hadharani kuwa serikali yake itauendesha mradi huo bila kuangalia ‘makunyanzi’ walioungana na wadau wa mazingira kuupinga.

Wanapinga kwa hoja kwamba mradi huo utaleta uharibifu wa mazingira kitu ambacho kitaathiri viumbe kwenye hifadhi hiyo.

Hata hivyo, pamoja na upinzani wa wanamazingira, Kituo cha Urithi wa Dunia, mojawapo ya taasisi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kimekubaliana na msimamo wa serikali kujenga mradi huo kwenye maporomoko hayo.

Kimekubali kubadili azimio lake la zamani la kuusimamisha moja kwa moja mradi huo baada ya majadiliano kiliyoyafanya na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.

Hiyo ni baada ya Tanzania kuwasilisha barua ya kuelezea msimamo wake juu ya mradi huo kwenye Mkutano wa 41 wa Kamati ya Urithi wa Dunia, unaoendelea jijini Krakow nchini Poland.

Katika barua hiyo, Tanzania iliweka wazi kuwa inapinga Rasimu ya Azimio Namba 41COM 7 A.17 aya ya (7) linalopiga marufuku kujengwa kwa bwawa la maji katika maporomoko hayo.

Ni kwa sababu hiyo Muungwana anatoa rai kwa Watanzania wote, wenye vyama na wasio na vyama kuacha siasa katika masuala yenye manufaa kwa wananchi kama ilivyo kwa mradi huu unaotarajiwa kujengwa ambapo wamejitokeza watu kuingiza siasa.

Tanzania ilieleza katika mkutano huo kwamba mpango wa kujenga bwawa hilo upo toka miaka ya 1960, na kwamba katika kipindi hiki ambapo imo katika kujenga Tanzania ya viwanda inahitaji kuwa na umeme wa kutosha.