TFF kumbukeni kuheshimu kanuni na sheria

17Apr 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe
Uchambuzi soka
TFF kumbukeni kuheshimu kanuni na sheria

HUKU Ligi Kuu Soka Tanzania Bara ikielekea ukingoni, hali imekuwa si shwari au kwa maana nyingine naweza kusema upepo umechafuka katika dakika hizi za lala salama ambapo mbio za kumpata bingwa wa ligi hiyo ya juu hapa nchini zimeanza kuonekana.

Ligi hiyo ndiyo inayotoa mwakilishi wa Bara kwenye mashindano yanayofanyika kila mwaka ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mpaka sasa vita ya kuwania taji hilo inaonekana inawaniwa na timu kongwe mbili, Simba na Yanga lakini lolote linaweza kutokea kwa Azam FC naye akafanikiwa kunyakua ubingwa huo.

Kwa nini nasema upepo umechafuka, hii ni kutokana na hali ya mazoea ambayo imekuwa ikionekana kuwa ni tabia kwa baadhi ya mashauri mbalimbali yanayowasilishwa na kutakiwa kutolewa uamuzi ama na Kamati zilizoundwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au shirikisho lenyewe.

Huku malalamiko kadhaa yamewahi kuchukua muda mrefu kuamuliwa huku mengine hadi sasa yakiwa yamewekwa 'viporo' kwa kutojadiliwa baadhi yake yamekuwa yakiamuliwa kwa mtindo wa 'mwendokasi'.

Hii inatoa mwanya wa kuonekana kuna upendeleo au dalili zozote za upangaji wa matokeo. Au kubariki madai ya wale ambao kila mara wanasisitiza kuwa bingwa wa Ligi Kuu hupangwa na msimu huu wamekuwa wazi wakiitaja Simba ndiyo amelengwa.

Kwa nini nasema upepo umechafuka, hii ni kufuatia kikao cha Kamati ya Saa 72 ya Usimamizi wa Ligi kilichokutana Alhamisi iliyopita na kuamua kuipa Simba pointi tatu baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya Kagera Sugar ambao ilimchezesha Mohammed Fakhi ambaye alikuwa na kadi tatu za njano.

Utata ulianza hapa kwa mara ya kwanza kikao hicho kuita waamuzi na kamshina wa mchezo kuwahoji na hatimaye kutoa uamuzi, hiyo haijawahi kutokea katika maamuzi yake mbalimbali ambayo ilifanya katika kusimamia ligi hiyo, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.

Kitendo cha kuita maofisa walioshiriki katika mechi hiyo, ndiyo kilianza kutia shaka uhakika wa taarifa ambazo ziliwasilishwa na waamuzi pamoja na kamisaa wa mchezo huo kuwa huenda ni tofauti za zile zilizoko kwenye ofisi ya Bodi ya Ligi.

Je endapo Simba ingeshinda mechi ile dhidi ya Kagera Sugar na isingekata rufaa, bodi au kamati hiyo ingekaa kimya au ingetoa tamko lolote wakati haina uhakika wa taarifa zilizoko mezani kwake? Jibu rahisi hapana, kwa sababu kitendo cha kuwahoji maafisa waliochezesha mchezo huo ili kuthibitisha taarifa walizoziwasilisha katika muda muafaka ni dhahiri hapa kuna mapungufu kwenye utunzaji au upokeaji wa takwimu.

Wakati kabla na baada ya uamuzi wa kuipa Simba pointi tatu kufanyika, tayari baadhi ya wadau ambao wanapinga mfumo wa pointi za mezani kuendelea, viongozi wa Yanga ambao hawakuona ni vyema kuweka nguvu zaidi kwenye mchezo kati ya timu yao dhidi ya MC Algeria, waliitisha mkutano na kueleza hawako tayari kuona hilo linafanyika na watajipanga kwenda hadi mahakamani kusimamisha ligi.

Hili nalo likiwa halijatekelezwa kutokana na uwapo wa sikukuu na hivyo mahakama hazifanyi kazi, juzi TFF imeandika barua ya wito kwa wajumbe kuhudhuria kikao cha Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Waehezaji ambacho kitafanyika kesho jijini, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmad Yahaya, alisema wakati akitangaza kuipa Simba pointi tatu na mabao matatu kuwa uamuzi unaotolewa na Kamati ya Saa 72 huwa haukatiwi rufaa na ni wa mwisho, je hiki kikao kinachotarajiwa kufanyika kesho kina mamlaka gani? Tunajua Kamati ya Utendaji ya TFF ndiyo yenye mamlaka ya juu kwa mujibu wa katiba.

Muda huu mbio za ubingwa zikiwa zimekolea, viongozi wa TFF mnatakiwa kuwa makini na kukumbuka pia na mbio za uchaguzi ambazo ziko mbele yenu zisiharibu mazuri ambayo mmeyafanya kwa faida ya soka la Tanzania.

Ni vyema kuendelea na utaratibu wa kutoingilia maamuzi ya kamati ambazo mmeziunda wenyewe.Kila la kheri Tanzania, Mungu Ibariki Tanzania.

[email protected]