Taka zizolewe mitaani bila ya kutoa visingizio

18May 2017
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Taka zizolewe mitaani bila ya kutoa visingizio

UZOAJI wa taka baada ya mvua mfululizo kwa kipindi cha wiki karibu tatu jijini Dar es Salaam, unasuasua kwa mitaa kadhaa unakabiliwa na hali hiyo.

Achilia mbali maeneo ya sokoni ambako taka zinazalishwa zaidi tena zikiwamo taka ngumu hali ni mbaya iwapo zitapita siku tatu tu bila taka kuondolewa.

Baadhi ya maeneo ikiwamo Tegeta, Kunduchi, Bunju kwenye makazi ya watu, hali ni hiyo, taka zimejaa haziondolewi, na kibaya zaidi wakazi wake hawana pa kwenda kuuliza.

Licha ya wakazi hao kuendelea kulipia ada ya uzoaji taka katika kila kaya kiasi cha Sh. 5,000 hadi 10,000 kwa mwezi, bado taka hazibebwi kwa wakati mwafaka.

Wakati mamlaka zilizopewa kazi ya usimamizi wa mazingira na wao kutoa tenda kwa wazabuni ndio wanaoondosha taka mtaani, lakini kuna malalamiko kuhusu mwenendo wake.

Mvua zinazoendelea kunyesha, imekuwa kisingizio kwamba magari yanakuwa na changamoto kubwa, hasa katika barabara ya kuelekea dampo, lililopo Pugu. Kwamba huko, njia hazipitiki na kusababisha magari ya ubebaji taka kukwama.

Hii ni hatari, kwa afya za wakazi wa maeneo hayo na jiji kwa ujumla, kwa kusababisha magonjwa ya tumbo, kipindupindu huku hospitali zikiwatibu kisha watu hao wakirudi mtaani ni kuchafu, inakua haina maana.

Mwaka jana watendaji, wakurugenzi wa halmashauri katika mikoa na wilaya nchini, waliagizwa kuhakikisha usafi na uondoshaji wa taka katika maeneo yao unafanyika kabla ya kuchukuliwa hatua.

Walitakiwa kuvunja mikataba kati yao na kampuni za uzoaji taka, ambazo hazitekelezi majukumu yake na kusababisha ongezeko kubwa la taka mijini.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina alitoa agizo hilo hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Ifahamike kuwa asilimia 80 hadi 90 ya taka zinazozalishwa katika majiji nchini, hazikusanywi na mamlaka za halmashauri.

Anaeleza kuwa, halmashauri hasa za miji mikubwa zimeendelea kutoa visingizio ili kuhakikisha taka zinaondolewa kwa wakati, huku wakikusanya mapato makubwa kutoka kwa wazalishaji wa taka hizo.

Anasema watendaji wanaotoa sababu za kutozoa taka, watachukuliwa hatua, mikataba ya wazabuni walioingia nao mikataba hawafanyi kazi ivunjwe, wao wanafahamu kuwa hawana vifaa, lakini wanawapa kazi.

Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 kifungu cha 104 na 139 kinazitaka mamlaka husika kuondolewa taka, hivyo uzembe hauhitajiki.

Wakati msisitizo wa ufanyaji usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ukififia, hali ya uchafu imeanza kurejea jijini.

Ni wakati wa halmashauripamoja na watendaji wa mitaa kuchukua hatua na kuhakikisha usafi unafanyika katika maeneo yao, kwa kuwa nao pia ni wakazi wa mitaa hiyo.

Iwapo uondoshaji wa magari umekuwa changamoto urejeshwe utaratibu ambao baadhi ya wakazi waliwatumia wabeba taka wanaokokota mikokoteni na kuingia kila nyumba na kuzibeba na kuzifikisha mahali husika kisha kujipatia riziki.