Serikali iwaajiri waliofaulu ualimu

13Apr 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali iwaajiri waliofaulu ualimu

KATIKA jitihada za kufungua fursa za kukua kwa uchumi wa nchi na kuchochea ustawi wa maisha bora kwa Watanzania, serikali ya Awamu ya Nne, chini ya uongozi wa Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, ilikuja na Mpango wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa.

Mpango huo ambao kwa Kimombo ulijulikana kama Big Results Now (BRN), ulichagua sekta sita kwa minajili ya kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kitaifa katika dhana nzima ya kufikia Matokeo Makubwa Sasa.

Moja ya sekta iliyochaguliwa na serikali katika kufikia malengo ya BRN, ilikuwa ni ya elimu.
Sekta zingine zilikuwa ni nishati, Maji, Miundombinu, Kilimo na Fedha.

Sababu kubwa ya kuchaguliwa kwa sekta hizo kuwa za kwanza miongoni mwa zingine, ilitokana na ukweli kwamba ndizo zinazobeba ndoto ya Wananchi.

Ndoto ya kufungua fursa za uchumi na ustawi bora wa wananchi.

Katika hotuba yake ya Uzinduzi wa Utekelezaji wa Mikakati ya BRN, kwenye sekta ya elimu, aliyekuwa Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakati huo, Dk. Shukuru Kawambwa alisema, wizara yake ilikutanisha washiriki 34 kutoka taasisi 31 za serikali na zisizo za serikali.

Lakini pia washirika na wadau wa maendeleo ambao walikutana katika mfumo wa maabara kwa kipindi cha wiki sita kutafakari kwa kina changamoto zinazoathiri sekta ya elimu.

Changamoto kadhaa zilibainishwa na mojawapo ya changamoto hizo ambayo kwa leo inaangaziwa na safu hii ilikuwa ni ya uhaba wa walimu kwa shule za msingi na sekondari.

Changamoto zingine zilizobainishwa ni pamoja na uwezo mdogo wa walimu kufundisha, motisha kwa walimu, uwajibikaji wa walimu na watumishi wa sekta ya elimu, upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na zingine.

Japokuwa suala la BRN halizungumzwi sana katika zama hizi za serikali ya Dk. John Pombe Magufuli, lakini suala la uhaba wa walimu nchini bado lipo.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu nchini (CWT), Ezekiel Oluoch, alinukuliwa mwanzoni mwa mwaka huu na moja ya chombo cha habari nchini akikiri hilo la upungufu wa walimu.

Oluoch alisema upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari unafikia takribani walimu 150,000.

Lakini hata Waziri wa sasa wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, anakiri hilo la upungufu wa elimu.

Wakati akijibu swali la Mbunge wa Buyungu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kasuku Bilago mwaka jana, alikiri uwapo wa uhaba wa walimu 22, 460 wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwenye shule za sekondari.

Sasa wakati uhaba wa walimu ni changamoto iliyoanishwa toka kuzinduliwa kwa BRN, mwaka 2013, na hata wadau wa elimu na serikali iliyopo madarakani ikiliungama hilo, bado serikali haijaajiri walimu waliomaliza mafunzo yao kwa karibu miaka mitatu sasa!

Uchunguzi wa Muungwana unaonyesha kwamba serikali ina vyuo vya ualimu na vyuo vikuu vinavyofundisha ualimu takribani 40, ambavyo vina uwezo wa kuzalisha karibu walimu 12,000 kwa mwaka.

Ni kwa mtazamo huu ndipo Muungwana anapoona kuna ulazima wa serikali kuwaajiri walimu hao ambao kwa sasa wako mtaani ili wakasaidie kupunguza changamoto ya uhaba uliopo wa walimu, kwa maslahi ya kuongeza ubora wa elimu nchini, lakini pia katika dhima nzima ya kufikia malengo ya BRN kwenye sekta ya elimu.