Rais John Magufuli, endelea kutembea juu ya kauli yako

29Dec 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Rais John Magufuli, endelea kutembea juu ya kauli yako

VITENDO vya rushwa, ufisadi na kila aina ya uozo serikalini na ndani ya CCM ni miongoni mwa vitendo ambavyo Rais wa sasa John Magufuli aliahidi kupambana navyo alipokua akijinadi kwa Watanzania kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Magufuli alitoa ahadi hiyo kwenye mikoa mbalimbali nchini kwa vile aliamini kwamba vitendo hivyo ndivyo vinavyochangia kukwamisha maendeleo ya Mtanzania mmoja mmoja na nchi kwa ujumla, huku watu wachache ndio wakineemeka.

 

Hata hivyo, wapo wale ambao walikuwa wanambeza wakisema kuwa ni kawaida ya wanasiasa ya kuahidi mambo lakini mwisho wa siku wakishachaguliwa wanashindwa kuyatekeleza.

 

Waliamini kwamba hana ubavu wa kupambana na vitendo hivyo, kwa madai vimeota mizizi.

 

Hata hivyo, mwenyewe alijibu kuwa alichoahidi sio nguvu ya soda bali alikuwa na dhamira ya kweli kushughulikia vitendo hivyo.

 

Hata soda yenyewe ikichanganywa na gongo huwa inakuwa kali.’ Ndivyo alivyosema akimaanisha kwamba hawezi kukatishwa tamaa na wale waliokuwa wakimbeza wakidhani hana ubavu wa kuwashughulikia 'waovu'.

 

Hata wakati akizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano mwishoni mwa mwaka juzi, alirejea mambo aliyoyaahidi wakati wa kampeni zake za urais huku akijipa jukumu aliloliita la kutumbua majipu.

 

Kwa wale wanaofuatilia utendaji wake watakubali kuwa amefanikiwa kuziba mianya iliyokuwa ikitumika kuiba mali ya umma na anaendelea kukabiliana na kila aina wizi ikiwamo kuwabana watumishi hewa na wengine wanaojitafutia utajiri kwa njia zisizo halali.

 

Mwenyewe amekuwa akisema kuwa nchi hii ni tajiri, lakini wapo watu wachache waliokuwa wakifaidi utajiri huo, hivyo ameamua ‘kulala nao mbele’ ili kuhakikisha kwamba kila mtu anafaidi matunda ya utajiri wa Tanzania.

 

Inawezekana bado kuna mianya mingi, lakini kwa ujumla ni kwamba Rais Magufuli na timu yake wanafanya kazi kubwa na kusababisha baadhi ya watu kulalamika kuwa ‘vyuma vinakaza.’

 

Katika utendaji wake wapo baadhi ya Watanzania ambao wamekuwa wakiulaumu na kuukosoa, lakini ni ukweli ni kwamba katika maisha mtu hawezi kufanya jambo likafurahiwa na watu wote.

 

Kwa mtazamo wangu ni kwamba aendelee na kazi ya kuibua uozo huo kwa sababu nchi ilikuwa imefika pabaya na hakuna aliyekuwa anashtuka, hivyo hatua yake ya kuirudisha kwenye mstari haina budi kuungwa mkono.

 

Imekuwa ni kawaida yake kukumbushia kile alichoahidi na kufafanua kuwa hakutoa ahadi ili apigiwe kura bali atahakikisha yote aliyoahidi anayatekeleza, kwa sababu anatambua kuwa ahadi ni deni.

 

Hatua hii inaonyesha ni jinsi gani anavyotembea juu ya kauli yake kwani anapokemea jambo anaonyesha wazi kwamba kile anachokisema kinatoka moyoni, anaonyesha kukerwa na mambo ambayo anaona yanafanywa ndivyo sivyo.

 

Hivyo ndivyo kiongozi anatakiwa kuonyesha kutoka moyoni kwamba anachukia jambo ambalo anaamini halina manufaa kwa wananchi anaowaongoza badala ya maneno matupu.

 

Mimi ninaamini kwamba mwendo huu wa serikali ya awamu ya tano utawafanya kila Mtanzania kuishi kulingana na kipato chake na sio mwenye nacho kuendelea kuongezewa huku mnyonge akiteseka.

 

Kinachotakiwa ni kila mmoja wetu kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali hii na pia kutoa ushauri pale ambapo inaonekana kuna tatizo, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mmoja wetu anafaidi keki ya taifa.

 

Ninajua kila hatua zina changamoto zake na inawezekana kabisa wapo wale ambao wakajikuta mirija yao imezibwa wanaiona serikali kama haina mwelekeo na kumbe inawezekana wao ndio wamekosa mwelekeo baada kubanwa.

 

Kwa hali ilivyo sasa ni kwamba wale ambao walizoea vya kunyonga wataendelea kulaumu, lakini ukweli utabaki pale pale kwamba Rais Magufuli amekuja kuirudisha nchi kwenye mstari.