Mkuranga, Kibiti, Rufiji zifanywe Kanda Maalum

12May 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mkuranga, Kibiti, Rufiji zifanywe Kanda Maalum

NIANZE kwa kuwapa pole wakazi wa wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, kwa matukio mbalimbali ya mauaji ambayo wamekuwa wakikumbana nayo yanayosababisha wapoteze ndugu, jamaa na marafiki zao.

Ninaamini kwamba kila raia mwema wa nchi hii atakuwa anaguswa na kuumizwa na matukio hayo ya kusikitisha ambayo yameendelea kupoteza maisha ya Watanzania wenzetu kwa sababu ambazo hazieleweki.

Mbali na matukio ya nyuma, hivi karibuni askari polisi nane waliuawa mpakani mwa wilaya za Rufiji na Kibiti na sasa limetokea tukio lingine lililoripotiwa na vyombo vya habari la mgambo kuuawa wilayani Rufiji.

Ninadhani kuna umuhimu sasa wa kuja na mbinu zaidi za kukomesha mauaji hayo.

Tanzania ni nchi huru, lakini inasikitisha na kushangaza kuona baadhi ya maeneo nchini, wananchi wakiishi kwa hofu namna hii.

Ni vyema serikali ikapandisha kiwango cha ulinzi hasa kwenye maeneo yote ya ukanda wa Pwani na ikiwezekana wilaya hizi ziwe Kanda Maalum kama ambavyo ilifanyika kwenye wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara na sasa angalau kuna unafuu, kwani matukio ya mauaji siyo mengi kama ilivyokuwa huko nyuma.

Nakumbuka Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo ambaye kiutaratibu ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema kuna haja ya kuanzisha Kanda Maalum ya Polisi yenye kikosi kipya ili kupambana na watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

Muungwana anadhani ni wakati mwafaka wa kutimiza haraka kile ambacho mkuu huyo wa mkoa alikisema.

Ninasema hivyo kwa sababu kama askari wenye dhamana ya kulinda raia na mali zao wanauawa kirahisi hivi usalama wetu uko wapi?

Waswahili wanasema kuwa ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji, leo wahalifu hao wanaua polisi na viongozi wa serikali, kesho watatugeukia sisi raia kwani hatujui lengo lao ni nini.

Kwa hali hiyo hatua madhubuti inapaswa kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kanda Maalum ya Polisi.

Baadhi ya wakazi wa wilaya hizo na hasa vijana wanaoendesha bodaboda wanadai kuwa wanashindwa kufanya shughuli za kujiletea maendeleo kutokana na masharti yaliyoanzishwa ya kutoendesha vyombo hivyo vya moto wakati wa usiku.

Wakati hao wakitoa madai hayo, abiria nao wanaotumia usafiri wa bodaboda wanadai kuwa wanalazimika kutafuta sehemu ya kulala iwapo watachelewa kutoka kwenye shughuli zao za kila siku.

Wengine wamekuwa wakihusisha mauaji hayo na mambo ya ugaidi, lakini ninashauri tusifike huko kwanza bali uchunguzi wa kina ufanyike kubaini kinachosababisha hayo yote na kuchukua hatua stahiki.

Pamoja na hayo, huu siyo muda wa kulaumiana, kila mtu afanye sehemu yake, kwa maana ya askari, huku wananchi nao wakitoa ushirikiano kama wana taarifa kuhusu wahusika wa mauaji hao.

Nina uhakika kwamba uchunguzi wa kina wa chanzo cha mauaji hayo ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na ushirikiano wa wananchi utarejesha amani kama zamani.

Inawezekana kuna kitu kimejificha, ambacho kinatakiwa kuwekwa wazi, kwani inashangaza ni kwa nini kuwe na mauaji ya mara kwa mara kwenye wilaya hizo tu kwenye mkoa wa Pwani?

Kuna wilaya za Mafia, Bagamoyo na Kisarawe ambazo ziko mkoani Pwani, wananchi wake wanaishi kwa amani,
lakini wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji zimekuwa ni majanga kwa nini?

Sina maana kwamba Mafia, Bagamoyo na Kisarawe kuwe na mauaji, hapana, bali ninatamani utulivu na amani virejee katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji ili wananchi waishi na kufanya shughuli za maendeleo bila hofu.