Mkataa kwao ni mtumwa

02Jan 2018
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Mkataa kwao ni mtumwa

“MTU anayekataa kwao huwa mtumwa mahali anapoishi. Methali hii yatukumbusha umuhimu wa kuzikumbuka asili zetu au tutokako. Twapaswa kuwaonea fahari wazazi wetu au hata mataifa yetu.

‘Asili’ni chimbuko la mtu, kitu au jambo; chanzo. Pia –a mwanzo; kabisa!, asilani!, abadan! Kwa muktadha (hali, wakati jambo linapofanyika au panapohusika) huu, nazungumzia lugha yetu ya taifa – Kiswahili.

Kiswahili ni ‘krioli’ yaani lugha ya awali ya wazungumzaji iliyoibuka kutokana na mchanganyiko wa lugha nyingi. Ni kisalia cha lugha mbili au zaidi ambacho hutumiwa na wazungumzaji kama lugha yao ya awali ya mawasiliano.

Ni kawaida kwa Mswahili anapozungumza na wenzake kuipamba lugha yake kwa kutumia tamathali mbalimbali za usemi kama vile tashbihi, tashihisi, istiara, jazanda, methali, misemo au nahau ambazo humjengea uwezo wa kuwa fasaha wa matumizi ya lugha katika mawasiliano yake.

‘Tashbihi’ pia ‘tashbiha’ni usemi unaofananisha kitu kimoja na kingine /chengine kwa kutumia maneno k.v. kama, mithili au sawa.

‘Tashihisi’ ni usemi wenye kukipa sifa ya uhai kitu kisichokuwa na sifa ya uhai. ‘Istiara’ ni matumizi ya neno kwa maana isiyokuwa ile ya msingi; tamathali ya semi inayofananisha viumbe viwili kwa kutumia sifa wanayoweza kuwa nayo.

‘Jazanda’ ni taswira yaani picha ya jambo inayomjia mtu akilini mwake anaposoma au anaposikiliza maelezo; umbo linalofanana na kiumbe kingine/chengine lililochongwa, lililochorwa au lililofinyangwa.

‘Methali’ ni misemo au nahau ambazo humjengea mtu uwezo wa kuwa fasaha wa matumizi ya lugha katika mawasiliano yake. Ni maneno ya kiufundi ambayo yamerithiwa tangu na tangu katika jamii, yanayosadikiwa kuwa na ukweli, na hutumika kutolea mfano au kufumbia. Maneno haya yanabeba ujumbe mpana zaidi kimaana kuliko maneno yenyewe yalivyo.

Kwa maelezo na ufafanuzi zaidi, soma Kamusi la Kiswahili Fasaha la Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) ukurasa wa K 476.

Pamoja na ukweli huo, Watanzania tunaendelea kudharau lugha yetu ya Taifa ama kwa kuchanganya na maneno ya Kiingereza au ya mitaani yasiyokuwamo kwenye msamiati (jumla ya maneno yaliyo katika lugha fulani) wa Kiswahili!

Wazungumzaji, waandishi wa vyombo vya habari wakiwemo watangazaji wa redio na runinga hawakosi kupenyeza maneno ya Kiingereza katika kazi zao! ‘

Yashangaza kwani hata wahariri wameshindwa kukemea tabia hiyo. Au wanakubaliana na waandishi wao? Huenda ndio maana wanaodurusu habari na makala huogopa kusahihisha!

Sikushangaa wakati washiriki wa mkutano wa kimataifa kujadili lugha ya Kiswahili waliokutana Zanzibar walisema bila kumumunya* kwamba lugha ya Kiswahili inaharibiwa na Watanzania wenyewe!

*Mumunya ni fyonza kitu taratibu kwa kukiweka baina ya ulimi na kaakaa* ;guruguza. *Kaakaa ni paa la kinywa linaloanzia kwenye ufizi wa meno ya juu hadi sehemu laini ya nyuma karibu na koromeo.

Ni vigumu kuwasikia viongozi wetu, watangazaji na wazungumzaji wa ofisini na mitaani kuzungumza Kiswahili bila kuchanganya Kiingereza ingawa cha kubabaisha! Matokeo yake, hata kuzungumza Kiswahili fasaha wanashindwa na kuishia maneno ya mitaani ambayo hayamo kwenye msamiati wa Kiswahili.

Vilevile waandishi hushindwa kuandika mtiririko mzuri wa habari/makala kutokana na matumizi yanayopewa tafsiri tofauti ya maana halisi.

Magazeti ya michezo yamekubuhu (kitendo cha mtu kukithiri katika jambo maalumu hasa lisilopendeza) kwa kupotosha maana ya maneno. Nimejaribu kuongea na baadhi yao lakini wanadai kuwa ni ‘ukuaji wa lugha ya Kiswahili!’

Majuzi nilipigiwa simu na mmoja wa waandishi wa habari za michezo akisema maneno ya vijiweni wanayotumia ndiyo yanayouza magazeti. Nilichoka! Nikamwuliza maana ya neno ‘hekalu’akaniambia ni nyumba ya ibada.

Nilipomwuliza tena kama ‘hekalu’ ni nyumba ya kufanyia ibada, kwa nini magazeti huandika kiongozi fulani amejenga hekalu akimaanisha ‘jumba kubwa,’ akashindwa kunijibu!

Kwa hakika ‘hekalu’ ni nyumba maalumu inayotumiwa na Mayahudi na Mabaniani kufanyia ibada.

Biblia Takatifu yaeleza Hekalu la Selemani lilikuwa jumba la mstatili lenye sehemu tatu: Ukumbi, Hekalu au patakatifu, chumba kikubwa cha ibada ya hadhara; na tatu, Patakatifu pa patakatifu, sehemu takatifu kabisa (Soma 1Fal.6:1 n.k.). Humo liliwekwa Sanduku la Agano (1Fal. 6: 19).

Soma kichwa hiki cha gazeti la michezo: “Wamekula shavu la Sportpesa.” Chini ya kichwa hicho iliandikwa: “Promosheni ya ‘Shinda na SportPesa’ inazidi kushika kasi na tayari wateja kadhaa wa kampuni hiyo ya michezo ya kubeti wamekula shavu kwa kubeba Bajaji katika droo tofauti zinazoendelea kuchezwa.”

‘Shavu’ ni minofu iliyoko upande wa kulia na kushoto kwenye uso wa mtu; pia ni kiungo anachotumia samaki kuvutia pumzi. Hilo ‘shavu’ la Sportpesa likoje?

Imeandikwa “ … wamekula shavu kwa kubeba Bajaji …” He! Nani hao ‘waliobeba’ Bajaji? ‘Beba’ni kitendo cha kuchukua kitu mgongoni au begani.

Nawatakia wasomaji wangu wote wa safu hii Heri ya Mwaka Mpya 2018.

Methali: Wagombea ndizi mgomba si wao!

[email protected]

0715 334 096 / 0622 750 243