Mgema akisifiwa, tembo hulitia maji

15Jul 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mgema akisifiwa, tembo hulitia maji

KWA kawaida mgema apewapo sifa kutokana na tembo (pombe ya mnazi) lake badala ya kutengeneza tembo zuri hulitia maji akaliharibu.

Ni methali ya kutumiwa kuwanasihi watu wasimsifu mtu mno asije akafura kichwa na kuharibika. Pia yaweza kutumiwa kwa mtu ambaye asifiwapo huishia kujivuna.

Chunguza sana utakubaliana nami kuwa wachezaji wa Simba na Yanga pamoja na vilabu vyao hupotoshwa na magazeti ya michezo. Magazeti huandika propaganda ili yanunuliwe, na kuwafanya wachezaji wanaosifiwa wajione bora kuliko wenzao kumbe si kweli.

Hata hivyo hajatokea wala hatatokea mchezaji bora chini ya jua awezaye kucheza peke yake uwanjani dhidi ya wachezaji 11 wa timu pinzani. Wanaosifiwa sana ni sawa na kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa kwani mwishowe hushindwa kuthibitisha sifa walizopewa.

Aidha, nionavyo kuna namna fulani ya uchonganishi unaofanywa na magazeti ya michezo. Soma vichwa vya habari vilivyoandikwa kwa herufi kubwa kwenye magazeti hayo na baadaye kufahamika kuwa si kweli!

Moja: “Mama amrudisha Niyonzima Yanga.” Ingawa ilisemekana kuwa mama mzazi wa Niyonzima alimsihi mwanawe asiiache Yanga mwishowe ikajulikana kajiunga na Simba!

Mbili: Gazeti hilohilo likaandika: “Ngoma aitosa rasmi Yanga” ikifuatiwa na habari kuwa: “Ukisema Simba na Yanga zimeingia chaka utakuwa sahihi na hii ni baada ya timu hizo zote mbili kushindwa kuinasa saini ya straika Mzimbabwe Donald Ngoma, ambaye taarifa zinadai kuwa amejiunga na timu ya Polokwane City ya nchini Afrika Kusini.”

Tatu: Kesho yake, gazeti dada la hilo likaandika: “Ngoma aitosa rasmi Simba – asaini Yanga kwa Sh. Mil. 132.” Kichwa hicho kilipambwa na picha ya Ngoma akisaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo.

Jana yake, gazeti dada ya hilo kutoka nyumba hiyo hiyo ya habari liliandika juu ya Ngoma kuitosa rasmi Yanga.

Nne: “Huyu ndiye mwenye hadhi ya Yanga: Ni fundi wa Lesotho mwenye mbavu za mmbwa, mkali wa mashuti, chenga aliyewatesa kinoma Muzamir, Banda, Mao.”
Wakati ikiandikwa hivyo, bado mchezaji huyo aliyeandikwa kuwa ni fundi wa Lesotho mwenye sifa kemkem hakuwa amesajiliwa!.

Tano: Kuna mchezaji wa Zambia aliyesifiwa mno mpaka akapewa jina la ‘mkata umeme’ hata kabla ya kusajiliwa na Yanga. Aliposajiliwa na kuichezea Yanga, hakuwa ‘mkata umeme’ wala ‘mkata waya!’ Leo yu’wapi ‘mkata umeme? Sifa za magazeti yetu ya michezo ndizo zinazoziharibu Simba, Yanga na wachezaji wao.

Sita: “Hilo tizi la Yanga acha” kwenye ukurasa wa mbele. Ukurasa wa pili: “Maandalizi … Tizi la Yanga usipime.” Sijui mazoezi (ambayo waandishi huyaita ‘tizi’) hupimwaje! Kwa mizani, rula au kamba?

Saba: Paragrafu ya kwanza ikaandikwa: “Kocha wa Yanga, George Lwandamina, hataki masihara kabisa katika maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Klabu Bingwa Afrika, baada ya kukipigisha tizi la kufa mtu kikosi chake.”

Huwa najiuliza mara kwa mara bila kupata majibu sahihi. Kama kocha anawapa wachezaji wake mazoezi ya ‘kufa’ ina maana aliwahi ‘kufa’ kisha akafufuka na sasa anawapa wachezaji mbinu za ‘kufa’ kama ‘alivyokufa’ yeye na baadaye ‘akafufuka’? Wachezaji nao hukubali kufanya mazoezi ya ‘kufa’? Kwani dunia imewachosha?

Nane: “Kiungo mpya Yanga mtamu bwana! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema, baada ya kiungo huyo kufanya vitu adimu na tamu katika mazoezi ya Yanga yaliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.”

Tisa: Soma vichwa vifuatavyo: “Kotei asaini, Simba ya ubingwa yatimia” na “Mido huyu akitua tu Yanga, Simba imeumia.” Uchochezi mtupu!

Hili ndilo tatizo kubwa la magazeti yetu ya michezo kuwasifu wachezaji wa kigeni hata kabla hawajatua nchini wala kusajiliwa!

Wakati mwingine wachezaji wetu hujimaliza wenyewe kwa tamaa ya hela. Wewe watakiwa kujisajili Simba au Yanga lakini nafasi yako kule ina wachezaji wawili mpaka watatu walio ‘hirizi’ ya timu hizo. Hujifikirii kuwa utawekwa akiba na mwishowe kupelekwa kwingine kwa mkopo?

Kwa upande mwingine, Simba na Yanga ndizo zinazoua vipaji vya wachezaji wetu kwa kushindana kusajili wachezaji weengi wasiochezeshwa.

Hudhani wanakomoana kumbe wanajikomoa wenyewe na kuharibu viwango vya wachezaji wanaowasajili bila mpangilio. Matokeo yake huwalipa wachezaji fedha ambazo zingetumika kufanyia shughuli zingine za vilabu.

Hebu waambie wanachama na mashabiki wa vilabu hivyo vifanye usajili wa wachezaji wa msimu mmoja tu na kuwalipa mishahara.

Thubutuu … ila ni hodari wa kuchonga! Kwa hilo nawapa kongole.
[email protected]
0715/0784 33 40 96