Mayowe ya wabunge utekaji yafanyiwe kazi

16Apr 2017
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
UPEPO WA ZANZIBAR
Mayowe ya wabunge utekaji yafanyiwe kazi

MAISHA ya watu wa visiwani maeneo mengi duniani hutegemea zaidi uvuvi, ufundi na kilimo huku wakitumia usafiri wa majahazi, madau, meli, ngalawa na mitumbwi kufika masafa mafupi na marefu

Kuishi visiwani kuna utamu wake na kunahitaji mazoea, kufuata kanuni, sheria na kuheshimu mila, silka na utamaduni. Watu wa visiwani, kwa kawaida huwa ni wapole na wakarimu. Hata hivyo, huonekana wakorofi, watukutu na machachari sana wanapolengwa kwa kubughudhiwa, kuvurugwa, kudharauliwa au kuwaletea tafrani ya aina yoyote ile.

Kwa sababu hiyo, wakitaka jambo na kuafiki kitu chao hukubali moja kwa moja, kichwakichwa na kuridhia mia kwa mia ila wanapokataa, kugomea na kupinga jambo hakuna namna ya kuwageuza. Hawakubali na wala hawasikilizi, hata kama utawasemesha kwa misamiati ya lugha wanayoifahamu kwa kina.

Kwa mfano, usafiri wa baharini una kanuni na sheria zake. Jahazini hakuna neno kamba. Kamba, kwa Zanizbar, ni aina ya samaki wa baharini na pia kifaa cha kufungia. Kila kamba uionayo kwenye jahazi ina kazi maalum na jina lake.

Kuna iitwayo sharti, enza, demani, joshi na hayari. Kila moja ina kazi yake, tena kwa wakati wake kadri nahodha atakavyoelekeza na kuwataka mabaharia wafanye au kutekeleza wajibu wao.

Mjumuiko wa majina ya kamba zote hizo hupandisha tanga juu ya foramali, tanga bovu huwa halihimili upepo mkali uvumao bahari. Nahodha na mabaharia kabla ya safari hutazama uzima na uimara wa tanga. Ikiwa limetoboka , kuchanika au kufumka, mabaharia hulishona kwa weledi ili wanaposafiri lisiwaletee tafrani na kuwapa hofu.

Katika safari ya meli au jahazi kunahitajika dhana ya umoja, upendo, mshikamano na ushirikiano mkubwa.Maisha ya mabaharia aghalab hutawaliwa na masikhara mengi, utani, matusi, vicheko na hadithi za kupendeza.

Maisha ya baharini yanaongozwa kwa taratibu husika ambazo hazikiukwi. Katika meli au jahazi unapokosekana umoja, ushirikiano na mashauriano, jahazi huweza kwenda kombo, mrama na mambo yakawa arijojo. Hakutakiwi sauti na amri ya kila baharia ifuatwe. Amri na maelekezo hutolewa na nahodha mmoja pekee huku mabaharia wote wakitakiwa kutekekeza, kutii na kufuata.

Bungeni mjini Dodoma hivi sasa yamezuka mayowe yanayopigwa na wabunge wakiwamo wale wa upinzani na wa chama tawala. Kwa kawaida kelele za wabunge hutolewa kwa kwa nguvu ya hoja.

Mayowe, malalamiko na hofu sasa ziko pande zote mbili. Wabunge wa upinzani na wa chama tawala, CCM wote wanalalalama, wanapaza sauti zao juu. Hawakubaliani na mambo yanavyokwenda ikiwamo kuzuka wimbi la baadhi ya watu kutekwa na wengine kutofahamika mahali walipo.

Wapo wabunge wanaosema kwa kupaza sauti zao wakipinga utamaduni uliozuka ghafla wa watu kutekwa na kupotea kiholela. Wanasema huo si mwenendo na utamaduni ulioachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na hiyo si Tanzania wanayoijua.

Nimekuwa nikijiuliza, hivi kimetokea nini huko Dodoma? Hofu na mshawasha ulionijaa ni kitendo cha kuona wabunge hao, bila kujali na kuzihusisha itikadi za vyama vyao, wanavyoonekana kuwa hawakubaliani na mambo mapya yaliojiri na vile yalivyo.

Baadhi yao wanataka iundwe tume huru itakayochunguza kuchomoza kwa vitendo hivyo. Kwamba kamati hiyo ije na majibu ya kina ili kujua kina nani wanaohusika, wametumwa na nani na kwa nini wafanye hivyo.

Wasiwasi wao ni kuhusiana na utekaji watu.
Wabunge wengine wanasema wamepata taarifa ya kuwapo mpango hatari wa kutekwa wabunge kumi na moja na mbunge mtoa hoja hiyo akidai yu miongoni mwa hao walengwa. Amelalamika kwamba amekuwa akikamatwa mara kadhaa, kuhojiwa na kuteswa na watu wa usalama.

Mbunge mwingine anataka Serikali isikubali mpango wowote ambao utaichafua machoni mwa wananchi.

Yupo mbunge mmoja naye amesimama bungeni akisema tokea atishwe jijini Dar es Salaam, hadi sasa anaogopa kulikanyaga jiji hilo akihofia usalama wake.

Pia yupo mbunge aliyesema haiwezekani mambo ya kuogofya yatokee katika nchi na serikali iendelee kukaa kimya kama haipo au haioni mambo yanavyokwenda na wananchi wakijenga hofu na wasiwasi katika fikra na mioyoni mwao.

Mbunge mwingine wa chama tawala alieleza huku akishangaa, kwamba iweje katika mkutano wa msanii anayedai kutekwa akizungumza na waandishi wa habari uhudhuriwe na waziri.

Amehoji kuwa je, akitokea mtu akisema iliyomteka ni serikali atakwepa?
Kama nilivyoeleza hapo awali kwamba, kawaida ya safari ya meli na jahazi hakutakiwi itokee na kushamiri mikwaruzano, mivutano au misuguano kati ya mabaharia na nahodha wao.
Mabishano, mivutano na kupingana wenyewe kwa wenyewe ikiwa kutachukua nafasi, jahazi si hasha likawa halina safari, halitafika mahali popote. Litakwama au kuzuka hamkani.

Ukiona manahodha au mabaharia wanagombea usukani baharini, jua safari hiyo ina walakin, imejaa dosari na pengine ina wingi wa kasoro zinazoweza kukifanya chombo wanachosafiria kikagonga mwamba.

Kwenye jahazi maji hujaa ngamani, mabaharia hulazimika kutoa maji na kumwaga baharini, maji yakiachwa yaingie chomboni bila kumwagwa chombo kitaelemewa.

Kikielemewa na iwapo kitapigwa na upepo mkali hakitasonga mbele na kujikuta kikizama
Je, viongozi wa CCM wanayaona mambo hayo? Na wanayachukuliaje? Maana yanaweza kuichafua serikali iliyoingia madarakani kwa tiketi ya chama hicho.

Kwa kadri ya upepo huu toka Zanzibar unaovyoyasukuma na kupiga mawimbi katika mwambao wa Pwani ya Tanzania na visiwa vyake, kwakweli unahitaji tahadhari na tafakuri ya kutosha kwani ni mayowe ya wabunge hawa wa kila itikadi hayapaswi kupuuzwa. Wazee wetu walituonya kwa kutuambia kuwa mdharau mwiba mguu wake huota tende .