Maofisa serikalini badilikeni

29Dec 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Maofisa serikalini badilikeni

MOJA ya misemo maarufu nchini ya kuitafadhalisha jamii na raia kwa ujumla wake ni msemo uliwahi kutolewa na aliyekuwa rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Mzee Mwinyi, katika misemo yake mingi ya kuwaelekeza wananchi wenzake aliyoitoa ili wawe na maamuzi yenye tija katika mazingira mbalimbali ni ule usemao ‘kila zama zina kitabu chake.’

 

Kwa tafsiri ya kawaida ni kuwa mzee Mwinyi ni kama alikuwa anaasa wananchi wenzake wawe waangalifu kila mara katika shughuli zao za kimaisha na wabadilike kufuatana na hali ilivyo kwa wakati huo.

 

Yaani wasifanye kazi zao kwa mazoea, kwani wakiendekeza utamaduni huo wa kufanya kazi ama shughuli zao mbalimbali kwa mazoea, wanaweza kujikuta wakiumia au wakapata hasara ambayo kumbe ingeweza kuzuilika.

 

Ingeweza kuzuilika iwapo wangeng’amua mapema mantiki ya msemo huo wa kuwa kila zama zina kitabu chake na hivyo wakabadilika kufuatana na mazingira yaliyopo kwa wakati husika, sawa na kinyonga anavyobadilika rangi kufuatana na mazingira alipo.

 

Muungwana ameanza na ufafanuzi wa msemo huo wa Mzee Mwinyi, maarufu kama ‘Mzee wa Ruksa’ ili kuwa katika nafasi nzuri ya kukidadavua anachokilenga leo ambacho kimsingi kinawalenga maofisa wa serikali.

 

Maofisa wa serikali na wa umma walio katika nafasi za utendaji.

 

Muungwana anaona baadhi ya maofisa hawa watendaji bado hawajaamka, bado wanadhani kwamba wanaishi katika zama zile za enzi na enzi na hivyo kuendeleza utendaji wa kimazoea.

 

Kwamba bado hawajagutuka kuwa hii ni awamu ya tano na ina kitabu chake, kitabu kinachoongozwa na utumishi kwa wananchi pamoja na falsafa ya ‘Hapa kazi tu’ inayowataka watoe huduma bora kwa raia na tena kwa wakati.

 

Kwamba ile ‘blah blah’ ya njoo kesho haina nafasi tena katika zama hizi za uongozi wa Dk. John Pombe Magufuli anayelenga kuifanya nchi isonge mbele katika dhima nzima ya kujiletea maendeleo na hivyo kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2015.

 

Pengine nitoe mifano hai ya jinsi baadhi ya watendaji serikalini na katika ofisi za umma ambavyo bado hawajagutuka, wakidhani bado muda ni wa mawio na matokeo yake wanasababisha mambo kwenda mrama.

 

Akizindua nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Arusha, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwaijia juu maofisa wa serikali walio chini yake.

 

Lukuvi aliwajia juu maofisa wa ardhi wa jiji kwa kitendo chao cha kuchelewesha utoaji wa vibali vya ujenzi, kitendo ambacho kimesababisha ujenzi wa makazi holela katika miji na majiji nchini.

 

Lukuvi akasema kuwa wakazi waliojenga makazi holela yaliyotapakaa kwenye miji na majiji nchini hawakufanya jinai yoyote, lakini hiyo imetokana kwa sehemu na kitendo cha maofisa na watendaji wa ardhi cha kushindwa kutoa vibali kwa wakati.

 

Akasema kwa kitendo chao hicho, kinawafanya wawe mizigo kwa wananchi kutokana na ukiritimba wao usio na nafasi katika zama hizi.

 

Mfano mwingine ni ule uliojitokeza kwenye ziara mkoani Tanga ya Rais Magufuli katika Kiwanda cha Tanga Fresh ambapo hati ya umiliki wa kiwanda hicho ilikuwa imezuiwa na ofisi za serikali kwa kuwa mmiliki wake wa awali alikuwa akidaiwa kodi ya mtaji ya shilingi bilioni 1.2.

 

Kitendo hicho cha kuzuiwa kwa hati ya umiliki kilisababisa benki ambazo zilikuwa zimekubali kukipatia mkopo wa shilingi bilioni 12 kwa ajili ya upanuzi wake zisite.

 

Ni amri ya Rais Magufuli ya kutaka kiwanda hicho kirudishiwe hati hiyo ndiyo iliyookoa jahazi.

 

Ni rai basi ya Muungwana kwa maofisa watendaji serikalini na katika ofisi za umma kubadilika kwa ustawi wa taifa kwani zama hizi zina kitabu kingine.