Maeneo yenye tija ikiwa utawekeza fedha zako

21Apr 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Maeneo yenye tija ikiwa utawekeza fedha zako

MMOJA wa wasomaji wa safu hii kutoka jijini Mbeya alinipigia simu mwanzoni mwa wiki hii akitaka kujua maeneo ambayo anaweza akawekeza fedha zake ili zimzalishie zaidi, lakini pia ziendelee kuwa salama.

Kadri nilivyomuelewa msomaji wa safu hii ya Mtazamo Kibiashara ni kwamba, ana fedha tayari, lakini hana uhakika wa eneo la kuwekeza fedha zake.

Kama tulivyoona wakati tunazitalii kanuni za fedha, moja ya kanuni ambayo kimsingi inaweza kuwa jibu ya swali la msomaji ni kanuni ya tatu.
Hii inazungumzia namna ya kuifanya fedha yako ikuzalishie zaidi kwa kuiwekeza kwenye maeneo yanayolipa.

Kwa maana hiyo, mtu anapaswa kuwa mwangalifu katika kufanya uchaguzi wa wapi anataka kwenda kuwekeza.

Kuna maeneo mengi yenye tija ambayo mtu anaweza kupeleka fedha zake, ili yamzalishie zaidi.

Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na kuongeza mtaji kwenye biashara uliyonayo na hivyo kuifanya ipanuke na kutengeneza faida zaidi.

Eneo lingine unaloweza kuwekeza na ukawa na uhakika wa faida, ni lile la mali zisizohamishika kwa maana ya ardhi kama vile mashamba na ujenzi wa nyumba.

Na katika siku za hivi karibuni, kumeibuka eneo la uwekezaji lenye uhakika, na waliobahatika kulibaini na kuitumia fursa katika kuwekeza fedha zao huko, wamefaidika sana na wanaendelea kufaidika kila siku.

Eneo hili ni la kuwekeza kwenye masoko ya fedha kwa njia mbalimbali.

Katika hili mfanyabiashara anaweza akanunua hisa kutoka kwenye kampuni zilizojisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Ni juu ya mfanyabiashara ama mtu yeyote kama huyo msomaji wangu kupata taarifa sahihi ya kampuni zinazofanya vizuri zaidi na kununua hisa zake.

Hii ni njia ya uhakika ya kutunza fedha na kupata faida kwa sababu mhusika atakuwa na uhakika na usalama wa fedha yake, lakini pia atapata faida kupitia gawio la hisa zake.

Lakini kwenye masoko ya fedha, kuna fursa pia ya kununua dhamana ama hati fungani zilizoko sokoni kwa hivi sasa.

Kwa mfano serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inauza hatifungani ama dhamana za serikali za muda mfupi, na za muda mrefu.
Mwekezaji hapa atakuwa na uhakika wa usalama wa fedha zake, lakini na faida itokanayo na riba inayolipwa.

Ukiachana na dhamana za serikali, kuna kampuni binafsi ambazo pia ziliruhusiwa kuuza hatifungani zake.

La msingi la kuzingatia hapa ni kuwa, eneo unalowekeza fedha yako, lina faida zaidi.

Nasema hivyo kwa sababu, kuna sehemu ambazo watu hufikiri kwa kuwekeza fedha zao huko zinakuwa salama na zitawapatia faida, lakini ukweli wanapoteza fedha zao tu.

Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na kuweka fedha benki ukiamini unapata riba kubwa zaidi, kununua vitu vya matumizi kama magari ya kutembelea, ukiamini kwamba ukiwa na magari mengi ya kutembelea ni mali zinazokuzalishia, kumbe patupu.

Hivyo ni bora basi ukachagua maeneo salama na yenye faida ya kutosha kama niliyoyaeleza hapo juu, kwa ustawi wako.