Madereva na makondakta wa daladala, nidhamu bado tatizo

14Jul 2017
Janja Omary
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Madereva na makondakta wa daladala, nidhamu bado tatizo

ABIRIA ambaye kimsingi ni mfalme katika usafiri wa umma au maarufu kama daladala. Hivyo, hapaswi kubugudhiwa pindi anapokuwa safarini.

Nimeamua kulisema hilo, kwani mara nyingi wahudumu hao huwa marafiki na kukubembeleza pale anapotaka kupanda. Abiria anabembelezwa kwa vigezo na vishawishi vingi, ili awe sehemu mojawapo ya wateja.

Pindi abiria huyo akiingia ndani ya himaya ya kondakta kwa kupanda ndani ya gari na safari yake ikaanza, wasifu huo unabadilika. Vivyo hivyo, anaposhuka, anageuka kuanza kukutana na kero ya kondakta na thamani yake kama abiria mlipa nauli inakwisha papo hapo.

Hapo ndipo kero ya dereva na kondakta na dereva wake wakiwa na haraka isiyo na maana inajionyesha, pale abiria anafika mwisho wa safari na kimsingi ndiyo mkataba wa nauli ulivyo.

Napenda niseme kuwa kondakta  bora  ni  yule anayemheshimu abiria wake, kabla  na baada ya kupanda gari na katika nafasi yake akiwa msaidizi mkuu wa  dereva, anapaswa   kuzingatia hilo kama wajibu  wake wa msingi kazini.

Kwa tafsiri, kondakta ni nani? Ni yule anayekuwa kiunganishi  kati ya gari  na abiria, pia anayeshawishi  abiria kulitumia gari  husika, ili abria atoe  nauli inayozaa mengi, kama vile kipato cha mmiliki wa gari.

Hicho, ndicho kinachozaa malipo kwa wafanyakazi wa chombo cha usafiri, kuhudumia matengenezo na huduma nyinginezo, kama vile malazi na usafi na inazalisha tozo zote za kiserikali dhidi ya chombo hicho, iwe leseni, kodi ya mapato au mauzo na kadhalika.

Je, ni mara ngapi mwananchi umekumbana na kauli chafu  zinazotoka kinywani mwa kondakta? Imekuwa kawaida kwa makondakta wetu nchini, wanawatolea abiria kauli za fedheha na zenye ukakasi kwa abiria, jambo linalowakera watumiaji daladala.

Inafahamika  wazi  kuwa,  wajibu wa kondakta ni kuwa na tabia njema na kauli nzuri, sambamba na kumsikiliza mteja  kwa kutumia busara, kwani ni muhimu kwa kila kitu endapo abiria atapungukiwa nauli na kauli chafu si suluhisho la kukupa nauli  aliyopungukiwa.

Ni vyema huruma na busara zitumike kumfikiria abiria na siyo kumtolea kauli chafu, kwani kufanya hivyo kutamsaidia abiria afurahie safari na si vinginevyo, kwani tunakubali kondakta anafanya makusanyo halali kutoka kwa abiria wake.

Nimeamua kulikemea suala hilo, nikiamini wapo watu watakaoniunga mkono katika hili, kuhakikisha vitendo hivyo vinapungua, kwani ni vya kizamani sana na dunia ya sasa imepiga hatua, hivyo hatupaswi kuwa nyuma.

Nitoe pole kwa abiria wanaokumbwa na madhila hayo na ni changamoto ya kauli chafu kama itapungua mapendekezo. Ushauri uliopo ni kwamba, ipo haja ya makondakta kupata mafunzo, japo ya muda mfupi na wahitimu wapatiwe vyeti maalum, itakayowasaidia kulinda nidhamu zao kazini.

Kuna kero kama ya mavazi, ikiwa makondakta na madereva hawazuiliwi kuvaa vizuri, jambo ambalo katika uhalisia inaonekana wameshindwa kabisa kuitekeleza.

Ni pendekezo linaloweza kuonekana gumu, pia kutoungwa mkono na wadau husika, lakini ukweli bado ipo palepale kwamba ni moja ya nguzo muhimu katika kujenga nidhamu miongoni mwao.

Katika miji mikubwa kama ya Dar es Salaam, unapozungumzia usafiri kwa wananchi wakazi wa Dar es Salaam, iko wazi katika suala la usafiri wao, mtazamo unaishia katika matumizi ya daladala kila kona, jambo linalofanya kuwepo umuhimu mkubwa wa kuwa na nidhamu ya wahudumu wa daladala na kwa nafasi ya pekee, ninazungumzia makondakta na madereva.