Madereva jifunzeni kupitia yanayojiri Usalama Barabarani

21Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mjadala
Madereva jifunzeni kupitia yanayojiri Usalama Barabarani

JUZI usiku nilikuwa katika eneo la Kinondoni Mkwajuni, majira ya saa tano usiku. Wakati nasubiri daladala barabarani, nilishuhudia bajaji moja ikipita barabarani ‘imebana kushoto’ na nyuma yake ikifuata gari moja, nadhani ilikuwa ama Mitsubishi Pajero au Toyota VX, ambayo ilikuwa ina kasi kubwa.

Ndani ya muda mfupi, nilisikia mlipuko mkubwa wa sauti bajaji ile ikigongwa kwa nyuma na ikarushwa mbele na kupinduka kwa staili ya ‘samasoti’ huku gari la mgongaji likiongeza mwendo na kukimbia kwa kasi kubwa kuelekea Magomeni, ikizingatiwa barabara ilikuwa wazi Ni ndani ya dakika kadhaa za ‘kufumba na kufumbua’ alishatoweka eneo la tukio .

Kama ilivyo kawaida ya wakazi wa Dar es Salaam, wengi walikusanyika, wakiwamo vibaka kuwashuhudia majeruhi. Waliofika mwanzo walianza kwa msaada wa kuinyanyua ile bajaji iliyokuwa mguu juu, kichwa chini. Baada ya hapo kilichofuata wote walibaki kuwa washangaaji pasipo msaada wa ziada kuwawaisha hospitali, majeruhi watatu na mizigo yao. Hao ni abiria kinamama wawili na dereva aliyelala huku akionyesha kulalamika sana kwa maumivi, damu zinamtoka sikioni.

Naam! Hii ndio salama na tafsiri ya ubaya wa ajali za barabarani zinazopigiwa kampeni kupunguzwa, fedha nyingi zinatumiwa na serikali, viongozi kuumua kichwa na kadhalika.

Hapo niliona hali ya majeruhi wakiwa wachache, lakini kutokana na uhalisia wa ajali zilivyo, huwa ni mbaya sana. Inahusisjha mabasi na malori makubwa katika barabara kuu za safari ndefu na huwa zinahusu vifo vya papo kwa hapo, majeruhi na vifo vya umati na kadhalika.

Japo ni la simanzi lakini nituime hili kama mfano wa kukumbushana madhila ya ajali hizi zinavyotuumiza. Hilo ni la wanafunzi wengi waliokufa kwa mpigo katika ajali ya mkoani Arusha, hata ikazua simanzi ya kitaifa.

Pia ilitumika pesa nyingi (hata kama ya wafadhili), kutibu majeruhi waliopelekwa nje ya nchi kutibiwa. Tusiende mbali na simulizi na mifano hiyo, kwani yote imebeba simanzi na si busara kuifufua kila mara na kwa kina. Naamini hapo kwanza sote tuko sawa!

Binafsi, bado namkumbuka sana Inspekta Jenerali wa Polisi aliyestaafu, Saidi Mwema, katika hatua zake za awali kabisa madarakani alipotoa tathmini yake ya kwanza ya kazi, alieleza kuridhishwa na tathmini ya namna kazi iliyofanyika kitaifa katika kupambana na majambazi na majukumu mengine ya kipolisi.

Mwema aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoani Dar es Salaam, kiongozi wa Polisi wa kimataifa –Interpol na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, kabla ya kupewa nafasi hiyo ya juu kitaifa, hakuficha eneo ambalo alidhani bado kuna ‘makinikia’ katika tija ya ofisi yake, kwamba ni Usalama Barabarani.

Mahali alilalamika sana kutokana na hali halisi, takwimu za matukio ya ajali za barabarani kutoonyesha mwenendo mzuri.

Pengine alichokisema Afande Mwema kina ukweli kabisa, kwani hata ikitathminiwa kwa kina hadi hali ya leo ajali ya barabarani ni mithili ya donda ndugu, kwamba hata ikitokea inapungua, basi ni nafuu ya kipindi kifupi.

Ukweli huo unaakisiwa hata na kinachoendelea katika ushuhuda wetu wa kila siku barabarani kwamba, bado ajali ni kila mara na inatokea katika kila pande ya nchi Mashariki, Kusini, Magharibi na Kaskazini, licha ya wana- usalama barabarani kijitahidi ikiwamo maboresho ya vifaa vyao vya kazi.

Najua kuna juhudi nyingi sana zimechukuliwa kuwakabili madereva wazembe. Hapa kuna mambo kama vile kuwekwa bidii na maboresho katika Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, ambazo zinafanyika kimkoa na kitaifa, mwaka huu kitaifa ilifanyika mkoani Kilmanjaro.

Ajali zinaua sana na tuna ushuhuda mwingi wa vilio. Ila inapotokea tunapanda katika mabasi huwa napata tabu kuwaona madereva hasa wa daladala wakiendesha kwa kasi kubwa na ushindani wa kugombea abiria wachache wenye nauli za Shilingi 400 kila mmoja, pamoja na kuwepo udhibiti mkubwa kutoka kwa wachapa kazi askari wa usalama barabarani.

 

Inashangaza kuona baadhi ya abiria waadilifu wakiwakemea, wapo wanaowapinga kuwaunga mkono madereva wanaochochewa na makondakta.

Hicho ndicho kinachowakuta na madereva wa safari ndefu na abiria wakiangukia katika tabia ya kuendesha kwa kasi, katika sababu zisizokuwa na msingi kulinganisha na usalama wao binfasi, pia mali (gari) wanayoitumia.

Nikiwagusia ndugu zangu wa bodaboda, tabia mbaya imejikita zaidi katika kuendesha pikipiki kwa kasi katika mazingira ambayo hayana hata chembe ya hoja chanya, ikiwamo kugombea abiria.

Nitoe wito tu kwa madereva nchini, kwamba suala la kujirekebisha halina kuchelewa. Wajifunze kujitunza kazini kupitia wito mbalimbali katika maadhimisho na operesheni za Usalama Barabarani, abiria nasi tusiwe mbali.