Kipaumbele kitolewe bidhaa za mkonge nchini

27Dec 2017
Salome Kitomari
Nipashe
Mjadala
Kipaumbele kitolewe bidhaa za mkonge nchini

ZAO la mkonge lilipata umaarufu miaka ya 1970, kwa kutoa ajira kwa wingi, kuchangia pato la taifa na fedha za kigeni, pia kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Zao hilo liliporomoka baadaye baada ya dunia au wenye ‘misuli’ ya kiuchumi kuja na bidhaa mbadala ya mkonge na hivyo kuiathiri Tanzania ambayo ilikuwa ikizalisha bidhaa za mkonge na kuuza nje ya nchi.

Matumizi ya bidhaa za mkonge kwa soko la ndani yalikuwa madogo, na hivyo zao hilo lilipoyumba katika soko la dunia, ikawa ndiyo mwanzo wa kuyumba kwa uchumi wa mkonge, kama ilivyotokea kwa mazao mengine ya biashara kama kahawa na pamba.

Tofauti na mazao ya kahawa na pamba ambayo yana kipindi cha kukaa shambani pia yanahitaji dawa na huduma nzuri, zao la mkonge linavumilia kwa kiasi kikubwa na linavunwa kwa kipindi chote cha mwaka na halihitaji dawa zozote.

Unapotembea Kariakoo ambako ndiko kuna biashara nyingi utaona kamba zinazotumika kufungia mizigo ni za plastiki, ambapo ingewezekana kutumia za mkonge zinazozalishwa nchini.

Jola moja la kamba ya nje linauzwa Sh. 16,000 na jola moja ya mkonge inayozalishwa nchini inauzwa Sh. 22,000.

Sasa kwa tofauti hiyo ya bei unakuta wafanyabiashara wakizikimbilia kamba za nailoni kwa kuwa ni za bei rahisi zaidi.

Hata hivyo bado kuna nafasi ya kuimarisha zao hilo na kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia kamba zitokanazo na mkonge zinazozalishwa hapa nchini.

Habari njema kwa wakulima na wasimamizi wa zao la mkonge ni ile ya msukumo wa dunia katika kutunza mazingira unaohimiza matumizi ya vifungashio au bidhaa ambazo ni rafiki kwa mazingira.

 

Kwa mfano, singa inayozalishwa Tanga ni kwa ajili ya soko la nje kama Kenya, ambao hununua kwa ajili ya kutengenezea sofa, wakati sofa zinazotengenezwa nchini zinatumia nailoni yaani bidhaa kutoka nje, wakati malighafi inapatikana nchini.

Kitaalamu inaelezwa kuwa nailoni inapoingia ardhini ni ngumu kuoza, tofauti na bidhaa kama ya mkonge ambayo huoza na kuwa mbolea inayorutubisha ardhi, hivyo msukumo mkubwa kwa sasa ni matumizi ya bidhaa za mkonge.

 

Kwa habari njema hizo, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), lenye hisa asilimia 49 kwenye kampuni ya Katani Limited ya mkoani Tanga inayomiliki mashamba matano na viwanda 10 vya bidhaa za mkonge limeamua kuwekeza kwenye zao hilo.

NSSF ilikuwepo kwenye kilimo cha mkonge kinachotumia wakulima wadogo, wa kati na wakubwa, lakini kwa sasa inataka kuingia moja kwa moja kwa maana ya kuingiza mtaji, mikopo na mikakati ya kampuni ambayo itawezesha uzalishaji kufanyika kikamilifu.

 

Nilipata nafasi ya kutembelea kampuni tanzu ya Tancord (1998) Ltd, ambao wanazalisha bidhaa mbalimbali za vifungashio, mikopo, viti, kamba, nyuzi za viatu, mazulia na bidhaa nyingi za nyumbani na ofisini.

Kilichokosekana kwenye kiwanda hicho ni kutangaza na kusambaza kwa wingi bidhaa hizo, ikiwamo serikali yenyewe kukubali kununua bidhaa hizo kwa ajili ya matumizi ya ofisini badala ya kuagiza kutoka nje.

Kwa sasa mahitaji ya vifungashio vya mifuko au magunia ni makubwa sana kwa kuwa watu wanatoka kwenye matumizi ya nailoni na kwenda kwenye matumizi ya mazao ya mkonge.

 

Lakini pia Tanzania inajipanga kuwa nchi ya viwanda, hivyo ni wakati muafaka kwa NSSF kuwekeza katika utengenezaji wa magunia, ambayo yanahitajika sana nchini.

 Kwa mujibu wa wataalamu, zao la mkonge lina faida kuanzia shina lake hadi jani, na hakuna kinachotupwa bali huzalisha umeme wa kuendesha shamba na mitambo, gesi ya kupikia nyumbani, chakula cha mifugo, kilevi, mbolea ambavyo vyote vinahitaji.

Uamuzi wa NSSF umekuja kwa wakati muafaka katika kuimarisha na kuboresha kilimo cha mkonge ambacho kinaajiri wananchi wengi wa kaya za jirani na mashamba na kutoka maeneo mengine.

Jitihada hizo zinastahili kuungwa mkono na sera na sheria za serikali, kwa maana ya kusaidia matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini kutumika nchini, kuliko kutegemea masoko ya nje ambayo wakati mwingine ni ngumu kuwa na maamuzi.

Mfano, Kuna bidhaa za ofini, kamba zinazoweza kutumika bandarini, kutumiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kwenye shughuli zao mbalimbali, lakini si ajabu zinaagizwa toka nje wakati zinaweza kuzalishwa na kuuzwa nchini.

 

Bila kuwasaidia NSSF na Katani Ltd hawawezi kufikia lengo la kuimarisha viwango vya bidhaa hizo, ambavyo vitatoa ajira kwa wingi kupitia mnyororo wa thamani.

 Mungu ibariki Tanzania.