Kelele za muziki barabarani, mitaani zidhibitiwe

16Apr 2017
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Kelele za muziki barabarani, mitaani zidhibitiwe

UCHAFUZI wa mazingira sio kutupa taka ovyo au kutiririsha maji machafu barabarani, bali hata kelele zinazosababishwa na sauti kubwa za muziki au matangazo.

Kelele nyingi mitaani na barabarani husababishwa na magari ya matangazo na wauzaji wa kanda katika maduka na wanaotembeza mitaani.

Wanaosababisha kelele hizo mara nyingi wanakuwa hawawajali wenzao ili mradi wanatekeleza matakwa yao.

Inaeleweka kuwa biashara ni matangazo, lakini matangazo hayo yasiwe kero kwa watu wengine kwa sababu kuna watu wagonjwa wanaposikia kelele hizo zinawaathiri na kuwaongezea ugonjwa zaidi au hata kupoteza maisha.

Mkuu wa mkoa mmoja wa Dar es Salaam (miaka iliyopita), aliwahi kupiga marufuku kelele zinazosababishwa na magari ya matangazo na wauza kanda za muziki na kuagiza atakayekamatwa kuchukuliwa hatua.

Hata hivyo, agizo hilo lilitekelezwa kwa siku chache na hali ikarejea kama kawaida, mitaani na barabarani.

Kanuni mpya ya Mazingira itakayodhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na makelele yanayosababishwa na shughuli mbalimbali katika jamii, ilizinduliwa mwaka 2015 .
Kanuni hiyo ilitangazwa katika Gazeti la Serikali tangu Januari 30, 2015, kulingana na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2014.

Hata hivyo, kanuni mpya za kudhibiti kelele, hazitadhibiti kelele zitokanazo na ving`ora vya magari ya Polisi, magari ya zimamoto, magari ya kubebea wagonjwa pamoja na mizinga wakati wa magwaride katika sherehe za kitaifa.

Kanuni hizo zimeundwa kuitikia wito wa malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali waliokuwa wakilalamikia serikali kuhusu uchafuzi mkubwa wa mazingira unaotokana na kelele katika kumbi za starehe, uchimbaji wa madini pamoja na mitetemo inayosabishwa na minara ya simu.

Kufuatia kanuni hizo mpya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), lilianza kuzitumia ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa kelele na mitetemo.

Kwa kuanzia liliagiza mtu akitaka kufanya sherehe mtaani, kupiga muziki kwa kelele, kuendesha ngoma za kukesha atapaswa kulipa Sh. milioni 10. Aidha, kumbi za starehe za usiku zitakazopiga kelele, zitapaswa kulipa kiasi hicho.

Aidha, watakaohusika na kelele za migodini za kutumia baruti, kupasua miamba zilizo zaidi ya matakwa ya Sheria ya mazingira ya kelele na mitetemo, watapaswa kulipa Shilingi milioni tano ili kupata kibali.

Uchafuzi wa mazingira, unaosababishwa na kelele na mitetemo, umekuwa ukifanyika bila kujali Sheria za nchi na kufuatia kanuni hizo mpya sasa watakaokiuka watashughulikiwa.

Kanuni zimeweka vigezo na tozo maalumu la kuanzia Shilingi milioni tano hadi Sh. milioni 10, kulingana na eneo na aina ya kelele na mtetemo. Mambo mengine ambayo kanuni zimeweka ni faini kwa kila kanuni itakayovunjwa.

Kwa mujibu wa NEMC, mtu mwenye kutaka kufanya sherehe mtaani, itakayohusisha kelele zitakazosumbua jamii pamoja na majirani, ikiwamo muziki, ibada za makanisani zinazozidi matakwa ya kisheria ya uanzishwaji wa makanisa hayo katika jamii, atapaswa kulipa Sh. milioni 10 ndipo aruhusiwe kuendelea na shughuli yake.

Ruhusa inayo lipiwa pia ina muda na viwango vyake, kila muda husika unapoisha, kelele zinapaswa kupunguzwa ama kuzimwa. Hii inahusisha pia baa na kumbi za starehe za usiku.

Kila mtu anayeishi Tanzania atakuwa na haki ya kuwa na mazingira safi, salama na ya kiafya. Haki hii itahusisha kila raia kutumia vitu vya umma au sehemu mbalimbali za mazingira, kwa madhumuni ya burudani, elimu, afya, ibada, utamaduni na uchumi.

Mtu yeyote, pale haki iliyoelezwa imetishiwa kutokana na kitendo au kutotimiza wajibu ambako kunaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu au mazingira, anaweza kufungua mashtaka dhidi ya mtu ambaye kitendo chake au kutotimiza wajibu kwake kunaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu au mazingira.

Mashtaka yaliyoelezwa yanaweza kuzuia, kukomesha, kusitisha au kutotekelezwa kwa shughuli yoyote, ambayo inaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu au mazingira.

Aidha, yanaweza kumlazimisha ofisa yeyote wa umma achukue hatua za kuzuia au kusimamisha shughuli yoyote au kutotekeleza wajibu, ambako kunaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu au mazingira, kuamuru kuwa shughuli yoyote inayoendelea au kutotekeleza wajibu kunakoendelea kufanyiwe ukaguzi au upelembaji wa mazingira, kumtaka mtu ambaye shughuli yake au kutotekeleza wajibu kwake kunaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu au mazingira, achukue hatua za kuhifadhi mazingira au maisha ya binadamu na kuwalazimisha watu wanaoharibu mazingira kurekebisha uharibifu huo kwa kiwango cha kuyarejesha mazingira katika hali ilivyokuwa kabla ya kuharibiwa.

Vile vile kuelekeza kumlipa fidia kwa mwathirika kutokana na madhara au kutotimiza wajibu, pamoja na gharama zilizosababishwa na kukosa matumizi yenye manufaa kutokana na shughuli iliyosababisha madhara kwa afya ya binadamu au mazingira.
[email protected]; Simu: 0774 466 571