Jukumu la kulinda miundombinu ni la wote

12Jan 2017
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Mjadala
Jukumu la kulinda miundombinu ni la wote

JUKUMU kubwa la Serikali ni kuhakikisha inakuwepo miundombinu imara ikiwemo barabara, shule, zahanati na mengineyo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za kuzalisha mali na kuinua pato la Taifa.

Utekelezaji huo unaweza kufanyika kwa kutumia fedha za makusanyo ya ndani zinazotokana na vyanzo mbalimbali zikiwemo kodi zinazokusanywa na nyongeza za fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo.

Mwaka wa fedha 2016/17 sekta ya miundombinu inayojumuisha barabara, reli, nyumba, bandari, viwanja vya ndege, mawasiliano, Serikali ilitenga zaidi ya Sh.trilioni mbili ili kuhakikisha kuwa miundombinu inayojengwa katika maeneo mbalimbali ni imara na bora.

Serikali ya Rais Dk.John Magufuli ilipoingia madarakani ilitenga Sh. bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa inayotarajiwa kurahisisha usafiri wa reli nchini na kuunganisha vyema nchi jirani.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa aliwahi kubainisha kuwa, katika uboreshaji, ujenzi na ukarabati, Serikali inategemea kujenga reli mpya ya kisasa inayojulikana kama ‘Standard Gauge’.

Licha ya ujenzi huo, pia serikali ina mipango mbalimbali inayolenga kupunguza msongamano wa magari hasa jijini Dar es Salaam ikiwa pamoja na kuimarisha usafiri wa treni zaidi ya moja ili kurahisisha usafiri toka sehemu moja kwenda nyingine na kuchangia kusukuma kasi ya maendeleo.

Miongoni mwa jitihada zilizofanywa jijini Dar es Salaam ni kuanzisha treni ya kubeba abiria kutoka Stesheni Kuu hadi Ubungo maarufu kama ‘treni ya Mwakyembe’. Treni hiyo, imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wanaoishi maeneo hayo.

Agosti, mwaka jana, Waziri Mbarawa alizindua treni nyingine yenye mabehewa 16 inayofanya safari zake kutoka Stesheni ya Dar es Salaam hadi Pugu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi za Serikali kukabiliana na msongamano wa magari barabarani.

Treni hiyo ilianza safari zake kwa kusafirisha mabehewa 15. Kila behewa lina uwezo wa kubeba abiria 100 na hivyo behewa hizo kwa safari moja hubeba abiria zaidi ya 1400 hivyo kupunguza mabasi zaidi ya 40 ambayo yangelazimika kuwa barabarani yakiwa na wastani wa kubeba watu wasiopungua 50 kwa safari moja.

Licha ya kuanzishwa treni hiyo, Kampuni ya Reli (TRL) ambao ndio waendeshaji wa huduma hiyo, wamekuwa wakifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazokabili treni hiyo, ikiwemo upungufu wa mabehewa kwani mahitaji ya wanaoutegemea usafiri huo ni makubwa, ukilinganisha na wingi wa abiria.

Changamoto nyingine ni ya feni na ukatishaji wa tiketi ambao umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu na uongozi wa TRL.

Pamoja na Serikali utekelezaji huo wa ahadi zake kwa kuzindua treni hiyo, kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakirudisha nyuma jitihada hizo kwa kuhujumu miundombinu iliyowekezwa kwa fedha nyingi.

Waziri Mbarawa aliwahi kubainisha kuwa tangu huduma hiyo ianze kutolewa kumeripotiwa matukio ya uhujumu wa miundombinu ya reli likiwemo la kurusha mawe kwenye vioo vya madirisha ya treni hiyo.

Alitaja baadhi ya matukio kuwa ni Oktoba 28, mwaka jana katika eneo la Gongo la Mboto, lilirushwa tena jiwe wakati treni ikifanya moja ya safari zake za kila siku na huku tukio lingine la namna hiyo lilitokea Novemba 24, mwaka jana katika eneo la Karakata.

Katika hali ya kawaida usafiri unaotumiwa na wakazi zaidi ya 17,000 kila siku kutoka sehemu moja kuelekea sehemu nyingine na kuwarahisisha shughuli zao unapodhihirika kuwepo wananchi wachache wanaohujumu miundombinu hiyo kwa mtazamo wa kawaida hawana nia njema na maendeleo yanayofanywa na serikali yao.

Ni muhimu vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kufanya sehemu yao katika kuhakikisha usalama wa abiria na miundombinu inakuwepo na wananchi wana sehemu ya kufanya ili kuhakikisha kuwa usalama unakuwepo.

Si jambo la busara kuendelea kuihujumu miundombinu hiyo, kwani kwa kufanya hivyo, tunaifanya serikali iendelee kutumia fedha nyingi katika ukarabati wa miundombinu wakati fedha hizo zingetumika katika kuendeleza miundombinu hiyo na kuifanya kuwa bora zaidi.

Unapohujumu miundombinu kwa kurusha mawe kwenye mabehewa na kupasua vioo vya madirisha ya treni hiyo fikiria wananchi wanaotumia usafiri huo uwezekano wa wa kupata majeraha kwa sababu ya hujuma zao pia ikifika sehemu ikasimamisha huduma hiyo ili kukarabati mabehewa yaliyohujumiwa na kusababisha kero ya usafiri kwa wananchi wanaotumia usafiri huo, itakua si jambo jema na wananchi hawa hawatakuwa wametendewa haki.

Serikali ina nia ya dhati kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo na kuwa na miundombinu itakayowawezesha kufika mahala popote kwa usafiri ulio rahisi.

Wananchi wanaoishi pembezoni ya reli wana wajibu wa kulinda miundombinu na kutokubaliana na mwananchi yoyote wanayemuona akihujumu miundombinu iwe kwa kurusha mawe hata wakati mwingine kuhamisha kokoto au namna yoyote ile ya uhujumu.

Kila mwananchi akumbuke kuwa, miundombinu hii inatengenezwa kwa kutumia kodi za wananchi na kwa sasa nguvu kubwa imeelekezwa kutatua changamoto zilizojitokeza tangu kuanzishwa kwa usafiri huo.