Jeshi la Zimamoto na Uokoaji fanyieni kazi ripoti ya CAG

20Apr 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji fanyieni kazi ripoti ya CAG

MOJA ya kazi nzuri zilizofanyika mwaka huu toka serikalini kuhusiana na udhibiti wa jumla wa matumizi ya rasilimali za nchi katika dhana nzima ya kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi, ni ripoti iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Ninasema hivyo kwa sababu ripoti yake imegusa maeneo mengi yaliyo chini ya serikali kuu, serikali za mitaa na mamlaka za umma bila kusahau vyombo vingine kama vile idara zinazojitegemea pamoja na wakala mbalimbali za serikali.

Kama ilivyoanishwa kwenye Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008, CAG amepewa mamlaka ya kufanya ukaguzi ili kubainisha ufanisi wa rasilimali za nchi zinazoelekezwa serikali kuu, serikali za mtaa, mamlaka na wakala mbalimbali za serikali.

Amepewa mamlaka hayo ya kisheria kama mkono ama macho ya wananchi ya kuona jinsi ofisi za umma zinavyotumia fedha za walipa kodi zinazoelekezwa kwao.

Kimsingi pale ofisi za umma zinapopata fedha za wananchi katika dhana nzima ya kutekeleza wajibu na majukumu yanayoangukia kwenye maeneo yao, inatarajiwa zitatumie fedha hizo kama ilivyokusudiwa.

Lakini si hilo tu, bali vilevile inatarajiwa kwamba ofisi za umma zitahakikisha thamani ya fedha ilitolewa chini ya mamlaka zao, inalingana na kazi zilizofanyika .

Kwa hali hiyo, sheria hiyo inampa mamlaka CAG ya kuuliza, kuchunguza, kupeleleza na kutoa ripoti kadri anavyoona inafaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupitia kwake kwa Bunge na hivyo wananchi wote kwa ujumla, juu ya namna fedha zao zinavyotumika na ofisi za umma.

Lakini si hivyo tu, bali hata namna serikali kuu, serikali za mitaa, mamlaka na wakala za serikali zinavyotimiza majukumu yanayowaangukia.

Muungwana amesema kuwa ripoti ya CAG ya mwaka huu, ni moja ya kazi nzuri zilizofanyika kwa sababu imegusa mpaka maeneo mengine ambayo huko nyuma hayakuwahi kuguswa pamoja na umuhimu wake katika ustawi mzima wa wananchi.

Moja ya maeneo yaliyofikiwa na CAG katika ripoti yake aliyoitoa Machi, mwaka huu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (FRF).

Hili lina jukumu la kuhakikisha miongoni mwa mambo mengine kuzuia na kupunguza viwango vya vifo vitokanavyo na matukio ya moto.

Lakini pia lina jukumu la kuhakikisha kuwa linazuia na kupunguza majeruhi na uharibifu wa mali za wananchi zitokanazo na matukio ya moto, mafuriko, tetemeko la nchi, ajali za barabarani na majanga mengine.

Sasa kilichomvutia Muungwana kuiangazia ripoti ya CAG kuhusiana na jeshi hili ni mojawapo ya mapungufu yaliyobainishwa ya jeshi hilo.

Ripoti ya CAG imebainisha kwamba, kwa muda wa kipindi cha miaka mitano iliyoangaziwa na ripoti hiyo, yaani kutoka Mwaka wa Fedha wa 2011/12 hadi 2015/16, jeshi hilo halikufanya ukaguzi wa kutosha wa uwapo wa vifaa vya usalama wa moto kwenye majengo ya umma.

Hili ni tatzio kwa sababu janga la moto kwenye majengo ya umma limekuwa likitokea mara kwa mara na kusababisha upotevu wa maisha ya watu, mali, huku gharama za matengenezo ya kurejesha tena majengo hayo katika hali yake ya kawaida zikiwa ni za juu.

Ripoti ya CAG imeainisha kwamba jeshi hilo halikufanya ukaguzi wa kutosha ili kubaini uwapo wa vifaa vya usalama wa moto na kwa hali hiyo, halikuwa kwenye nafasi ya kubaini kama wenye majengo hawakuwa wakizingatia hitaji hilo.

Tulonge inaona hii ni changamoto kwa jeshi hilo sasa kujipanga na kuhakikisha suala la vifaa vya usalama wa moto kweli vipo kwenye majengo ya umma na vinafanya kazi inavyotakiwa.