Jamii ikemee kushamiri udhalilishaji watoto

26Nov 2017
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Jamii ikemee kushamiri udhalilishaji watoto

NOVEMBA 25 hadi Desemba 10 kila mwaka dunia inatekeleza kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia. Ni wakati wa kutafakari na kukumbusha jamii kukemea na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake,watoto na makundi yote ya wanyonge .

Kampeni hizo zimezinduliwa Ijumaa wiki hii lakini bado zipo habari mbaya zinazohusu kukithiri unyanyasaji watoto na wanawake nchini.Ni hivi karibuni Shirika lisilo la kiserikali la kupinga ukeketaji wanawake la (AFNET) limebaini kuwapo kwa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto kuanzia miaka saba hadi 11 katika wilaya za Kondoa na Chemba, mkoani Dodoma.

Shirika hilo lenye makao yake mkoani Dodoma linaeleza kuwa watoto hao hufanyiwa udhalilishaji huo ukiwamo wa kulawitiwa wanapokuwa maeneo mbalimbali kama nyumbani, mitaani au shuleni.

Aidha, linasema watoto hao hufanyiwa udhalilishaji huo na ndugu wa karibu wanaoishi nao majumbani mwao.

Vitendo hivi vya udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara na kinachosikitisha wanaowafanyia ni watu ambao wanaaminika kuwa walinzi wa watoto hao.

Pengine kuibuka na kuripotiwa vitendo hivyo kunatokana na elimu inayotolewa na serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu kuwa na uelewa.

Mwanzoni kabla elimu hii haijaenezwa vitendo hivyo vilikuwa vikifanyika na watu kuogopa kuviripoti hasa kwa kuona wanaofanya ni ndugu wenyewe na kuogopo kuleta ugombanishi.

Wazazi wengi wamekuwa na tabia ya kuwaamini ndugu wa karibu kukaa na watoto wao, lakini wanapokuja kugundua wanaowaamini ndio wabaya wao, mtoto anakuwa ameshaharibika.

Kuna umuhimu kwa wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao na kuwachunguza kila wanapokuwa nao ili kubaini mapema na kuchukua hatua.

Kesi nyingi zinazoripotiwa za watoto kuharibiwa utasikia kafanyiwa na baba yake wa kambo, mjomba au msaidizi wa nyumbani.
Katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili, Shirika AFNET kwa kushirikiana na mashirika mengine yanayopinga vitendo vya ukatili, yameamua kukomesha vitendo hivyo kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

“Tatizo la ulawiti limekuwa kubwa maeneo ya vijijini hasa katika wilaya za Kondoa na Chemba, umekuwa ukifanywa kwenye mazingira ya nyumbani na wanapokwenda shuleni,” linasema shirika hilo. Vitendo hivyo vya ukatili haviishii kwa watoto kufanyiwa udhalilishaji huo tu, bali pia kuwaoza watoto wa kike katika umri mdogo.

Mkoa wa Dodoma umebainika kushika nafasi ya nne kwa ndoa za utotoni kitaifa huku ukeketaji ukishika nafasi ya pili.

Aidha, ukeketaji wasichana kwa mkoa huo ni asilimia 51 na pia unashika nafasi ya tano katika vitendo vya ukatili wa kijinsia majumbani, na uwepo wa mimba za utotoni.

Kumekuwapo na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kutokana na uelewa mdogo wa kukabiliana na vitendo hivyo.

Shirika lisilo la kiserikali la Action Aid, ambalo linafadhili maadhimisho siku 16 za kupinga ukatili kwa kushirikiana na wadau wengine, limedhamiria kutokomeza vitendo hivyo kwa kutoa elimu kwa jamii.

Baadhi ya viongozi katika mkoa huo, wanakiri mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa yenye kiwango kikubwa cha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyokwamisha juhudi za wanajamii wa Dodoma kujiletea maendeleo kwa haraka.

Hata hivyo, viongozi kwa kushirikiana na wadau wengine wamejipanga kuchukua hatua ili kufikia Malengo Endelevu ya Kimaendeleo ya Dunia ifikapo 2030.

Aidha, wamejipanga kutekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa kwenye Mpango wa Kitaifa wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa miaka mitano kuanzia mwaka 2017/18 hadi 2021/22.

“Tutatumia maadhimisho ya mwaka huu kuelimisha jamii kuhusu uwepo wa mpango huu ili kila mdau achukue hatua stahiki na kuwezesha ufikiwaji wa malengo yote yaliyoainishwa kwenye mpango kazi ifikapo mwaka 2022.”

Ili kupinga ukatili kwa watoto kuna umuhimu mkubwa kwa wazazi, walezi, walimu, majirani na jamii yote kushirikiana kuvitokomeza vitendo hivyo.

Mtoto wa mwenzako anapofanyiwa vitendo hivyo, halafu usipochukua hatua, ujue na wewe pia ni kati ya watu wanaotakiwa kuchukuliwa hatua.

[email protected]; Simu: 0774 466 571