Hatua stahiki kutunza mazingira ziimarishwe kuepuka magonjwa

27Dec 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hatua stahiki kutunza mazingira ziimarishwe kuepuka magonjwa

JUMAMOSI ya mwisho ya kila mwezi, ilitangazwa na serikali kuwa siku maalum ya usafi nchini.

Uamuzi wa kuifanya siku hiyo kuwa ya usafi nchi nzima ulitangazwa mwaka jana na aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina.

Luhaga alisema, serikali iliamua kuifanya siku hiyo kuwa ya usafi wa mazingira katika dhima nzima ya kuhakikisha kunakuwa na utamaduni wa kufanya usafi wa mazingira ili kuepuka magonjwa ya milipuko.

Na akasisitiza kuwa dhamira kuu ya kuwa na utamaduni huo ni ile ya kuepusha vitongoji, vijiji na mitaa yetu kukumbwa na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu.

Akafafanua kwamba, hatua hiyo ililenga kutengeneza utamaduni wa uwajibikaji binafsi wa wananchi kuyatunza mazingira yanayotuzunguka.

Aidha, akaonyesha madhara ya kuwa na mazingira machafu kwa kutoa takwimu za mwaka 2015, zilizoonyesha kwamba takribani watu 12,000 waliugua kipindupindu na miongoni mwao watu 194 waliripotiwa kufariki dunia.

Mbali na kipindupindu, yapo pia magonjwa mengine yaliyo zao la uchafu.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) isemayo kwa tafsiri isiyo rasmi “Kuzuia Magonjwa kwa kuwa na Mazingira Bora’ inataja magonjwa mengine kuwa ni pamoja na malaria, kuhara, maambukizi kwenye mfumo wa upumuaji na majeraha yanayompata mtu pasipo kupangwa.

Magonjwa ya malaria na kuhara yanatajwa kama chanzo kikuu cha vifo vingi vya watoto duniani.

Kwa mujibu wa WHO, magonjwa haya yanaweza kuepukwa kwa kuweka mazingira katika hali ya usafi.

Kwenye tangazo la serikali la kuifanya Jumamosi ya kila mwezi kuwa siku ya usafi, serikali imeweka usimamizi wa usafi siku hiyo kwa viongozi wa ngazi za chini, kwa maana ya viongozi wa vitongoji, vijiji, mitaa hadi kata.

Pamoja na Muungwana kuona kasi kubwa iliyoanza mwanzoni katika harakati za kulitekeleza agizo hili kwenye maeneo ya makazi chini ya usimamizi wa mabalozi, wenyeviti wa serikali za mtaa na wajumbe wao, hali ilivyo sasa si ya kutia moyo.

Kwa nini ninasema hivyo, kwa sababu mazingira kwenye makazi na maeneo wanakofanyia kazi za kujiingizia kipato wananchi bado ni machafu.

Kwa mfano ukipita katika baadhi ya mitaa jijini Dar es Salaam, bado utakuta kuna baadhi ya makazi ni machafu, majani yameachwa bila ya kufyekwa, miti imechanua ovyo, viwanja vya makazi havisafishwi, kuna madimbwi yaliyojaa maji na baadhi ya nyumba hazina mashimo ya kutupa takataka.

Sasa sehemu kama hizi, mbu kuzaliana ndipo mahali pake, kipindupindu ndipo mahali pake, lakini vilevile watoto kukumbwa na ugonjwa wa kuhara wanapochezea maji machafu, ndipo mahali pake.

Aidha, unakuta kwenye baadhi ya makazi kunatiririka maji machafu ya chooni na kusababisha harufu mbaya na kibaya zaidi, wakazi wengine wanaachia maji ya vyooni kutiririka kuelekea kwenye makazi ya wenzao bila kujali.

Na kwa upande wa maeneo ambako kuna shughuli za kujiingizia kipato, kuna mitaro yenye maji machafu na ambayo imejaa rundo la maganda ya matunda.

Sasa hali hii inaendelea kujitokeza pamoja na kuwapo kwa viongozi wa serikali za mitaa na mabalozi ambao ndio kimsingi wasimamizi wa usafi katika maeneo yao.

Muungwana anatoa rai ya kuimarisha mbinu za kusimamia usafi wa mazingira ili kuienzi siku maalum ya usafi iliyotangazwa na serikali.

Mbinu mojawapo ni kwa watendaji wa serikali za mitaa kupita kwenye makazi ya watu wao kila wiki kukagua usafi pamoja na kutoza faini kubwa kwa wananchi ambao makazi yao ama sehemu zao za kazi ni chafu.

Muungwana anaona kuwa hatua hiyo itasaidia kuyafanya mazingira yetu kuwa safi na hivyo kuepukana na magonjwa niliyoyataja hapo juu yasababishwao na uchafu wa mazingira.