Dama (kamba) ni iliyo mkononi

11Jul 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Dama (kamba) ni iliyo mkononi

“USIJITIE hamnazo kucheza ngoma utakazo.” Hamnazo ni mtu anayejifanya hafahamu jambo au kujifanya hujali wala huelewi. Maana yake usijitie tabia ya kupuuza ukayafanya uyatakayo.

Methali hii huweza kutumiwa kumkanya mtu anayejitia mwapuza (mtu asiyetia jambo maanani, asiyezingatia jambo) au anayepuuza mambo aambiwayo na kuishia kuyafanya mengine mabaya.

Mwandishi mzuri apaswa kusoma kazi za wenzake. Hapo aweza kulinganisha uandishi wake na wao ili kujua matumizi bora ya maneno. Pia mtiririko wa sentensi zinazoeleweka kwa wasomaji.

Aidha kutambua matumizi ya vidahizo, konsonati, irabu, ngeli, vibadala na visawe. Kadhalika mabano, alama za uelekezi na matumizi ya alama za vituo. Juu ya yote, ni muhimu kusoma vitabu vya Kiswahili na Kamusi mbalimbali zinazofafanua maneno.

Baadhi ya waandishi huwa na mitindo yao ya uandishi inayoweza kuwa msaada mkubwa kwa waandishi chipukizi. Waandishi chipukizi huandika maneno mengi katika sentensi moja na wasomaji kutoelewa maudhui* yake.

*Maudhui ni: i) wazo kuu linaloelezwa katika kazi ya fasihi na ii) wazo linaloelezwa katika maandishi au katika kusema.

‘Uendelezaji’ ni: i) utendaji wa jambo na kulifanya lipige hatua. ii) utamkaji wa herufi moja moja za neno kulingana na tahajia (herufi zinazounda neno kulingana na mfumo wa lugha fulani) yake.

Magazeti, redio na runinga hutumia maneno ya vijiweni badala ya maneno halisi ya Kiswahili. Matangazo yatolewayo na kampuni za simu huwa na maneno ya kihuni au yanayopotosha maana ya maneno.

“Bamba nikubambe, Bamba ubambike” ni tangazo la runinga fulani inayohamasisha watu wanunue king’amuzi chao. Je, neno ‘bamba’ linaakisi (toa picha, dokezo, ishara au fununu kuhusu jambo fulani) maana ya tangazo hilo?

Maana ya ‘bamba’: Gamba la samaki; mfuniko; kitendo cha kufunika kwa kutandaza kitu juu; fumania; kitendo cha maradhi kuathiri mwili mzima; ‘ubamba’ kisu kilicholika sana na kuwa chembamba; bango.

Je, neno ‘bamba’ limetumiwa kwa maana halisi? Tangazo hilo limefikisha ujumbe uliokusudiwa kwa watazamaji wa kituo hicho maarufu nchini?

Kampuni ya Tigo linatangaza “Jaza ujazwe.” Mmoja wa wateja wao amelalamika mitandaoni kuhusu maneno hayo akisema kwao ni matusi na kuitaka kampuni hiyo iondoe maneno hayo.

‘Jaza’ i) malipo anayopewa mtu kwa matendo mema; ii) kitendo cha kuongeza au kutia kitu katika chombo mpaka kijae; pa mtu vitu vingi. ‘Jaza’ pia ‘jazi’ ni kibali alicho nacho mwalimu wa dini cha kuwaombea watu kabla ya shughuli.

Jambo lililofanywa wakati uliopita, husemwa ‘lilifanywa’ au ‘lilifanyika.’ Linapofanywa sasa, husemwa ‘linafanywa’ au ‘linafanyika.’ Kama unafuatilia vipindi vya Bunge, bila shaka umesikia wabunge wakitumia neno ‘nilikuwa.’

Mfano: “Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa jimbo langu wana shida kubwa ya maji, ‘nilikuwa’ naiomba Serikali ituletee maji ili kuepusha hatari inayowakabili kina mama wanaoamka usiku kwenda kutafuta maji …”

Unapokuwa na shida ya wakati uliopo haisemwi ‘nilikuwa’ kwani neno hilo hutumiwa kuelezea jambo la wakati uliopita. Mfano: Nilikuwa mgonjwa, sasa nimepona. Nilikuwa na njaa, sasa nimeshiba, nilikuwa sina kazi sasa nimepata, nilikuwa sijui, sasa nimejua n.k.

Sasa tusome jinsi waandishi wetu wanavyochanganya lugha ya Kiswahili na Kingereza: ‘HOW! AND WHY?’ KURASA MBILI PIGO TAKATIFU. ‘How’ maana yake ni jinsi (gani); namna gani; je; kwa vipi. ‘Why’ ni kwa nini? Mbona? Kwa sababu gani? Kama mwandishi ametumia maneno ya Kiingereza, ameshindwaje kujua maana yake kwa Kiswahili?

Kadhalika katumia maneno ‘pigo takatifu.’ Maana ya ‘Takatifu’ ni –lio takasika na dhambi; Biblia Takatifu, Kurani Takatifu; Maandiko Matakatifu. Kamwe hakuna ‘pigo takatifu!’

Tuondokane na ulimbukeni wa kuthamini Kiingereza na kubeza lugha yetu ya taifa – Kiswahili. Husemwa “Chako ni chako, cha mwenzako si chako.”

‘Nususi’ ni maelezo ya maandishi yanayothibitisha ukweli wa maelezo yaliyosemwa au kuandikwa. Mfano: “Haya ni katika nususi ya mambo.” Pia ni –enye bidii, -lio na juhudi.

Methali: Ajengaye si alalaye. Anayefanya jambo zuri si lazima afaidike yeye; aweza kupata faida mtu mwingine.
[email protected]
0715/0784 33 40 96