Changamoto elimu zishughulikiwe pamoja na mpango wa elimu bure

20Apr 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Changamoto elimu zishughulikiwe pamoja na mpango wa elimu bure

KATIKA kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Rais John Magufuli alitoa ahadi mbalimbali ikiwamo ya elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi kidato cha nne, ili kuwapunguzia mzigo wa ada wazazi na walezi.

Hatua hiyo kwa namna moja ama nyingine itakuwa imesaidia kwa kiasi kikubwa ingawa kuna changamoto ambazo zinatakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili elimu iweze kutolewa katika mazingira, ambayo ni rafiki kwa wanafunzi.

Ninasema hivyo kutokana na ripoti ya mwaka 2015/2016 iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ikibaini uhaba mkubwa wa samani na miundombinu katika shule za msingi nchini.

Kwamba choo kinachotakiwa kutumiwa na wanafunzi 25 wa kiume ama 20 wa kike, kwa sasa kinatumiwa na wanafunzi 57.

Mbali na hilo, ripoti ya CAG ikaonyesha kwamba wakati kuna wanafunzi milioni 8.34 kwa shule za msingi za serikali nchini, kuna madarasa 108,448 tu badala ya 208,540.

CAG akasema kuwa, hiyo ni sawa na wastani wa wanafunzi 77 badala ya 40 katika darasa moja na kwamba licha ya serikali kufanya kampeni kubwa ya utengenezaji wa madawati, ukaguzi wake umebaini wanafunzi milioni 1.1 hawana madawati.

Akafafanua kuwa hiyo ni sawa na asilimia 13 ya mahitaji na kwamba wakati upatikanaji wa madawati ukiimarika kutoka upungufu wa asilimia 24 mwaka 2015 hadi asilimia 13 mwaka jana, hali ni mbaya kwenye changamoto ya vyoo na madarasa.

Kwa ujumla ripoti hiyo ina mengi, lakini nigusie kwa hayo machache ambayo kimsingi yana uzito wake kwenye sekta ya elimu, kwani kama nilivyosema awali, elimu inapaswa kupatikana katika mazingira yaliyo bora.

Ninaamini kwamba, uamuzi wa Serikali wa kutoa elimu bure kwenye ngazi hiyo ulipokelewa vyema na baadhi ya Watanzania na hasa wenye kipato cha chini.

Hata hivyo, kuna umuhimu basi kwa changamoto hizi zilizotajwa na CAG kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Wanafunzi wakikaa kwenye madawati inakuwa ni rahisi kwao kusoma vizuri na wakiwa na vyoo vya kutosha na visafi wanaweza kuwa salama kiafya.

Kimsingi mjadala huu unasema kwamba haitakuwa ni vizuri elimu ikatolewa bure katika mazingira yasiyo bora.

Mwaka 2003, Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kikishirikiana na HakiElimu, walifanya utafiti wa maisha na mazingira ya kazi ya walimu katika wilaya saba nchini ili kupata mawazo na mtazamo wa walimu juu ya hali ya maisha na kazi ya ualimu.

Utafiti huo uliangalia nyanja mbalimbali zinazoweza kuchangia kuboresha ama kudidimiza hali ya maisha na kazi ya walimu.

Hii ilikuwa pamoja na mzigo wa kazi ya ufundishaji, uwiano wa wanafunzi kwa mwalimu mmoja na maendeleo yake.

Baada ya utafiti huo ulibainika kwamba ubora wa mazingira ya maeneo wanayoishi walimu, ni kivutio kikubwa na motisha katika utendaji mzima wa kazi za walimu na ulibaini kwamba shule zenye mazingira mazuri zina maendeleo ya kuridhisha katika taaluma ikilinganishwa na zile zisizo na mazingira ya kuridhisha.

Hivyo elimu bure inabidi iambatane na kuwapo kwa madawati ya kutosha katika shule zote, vyoo vya kutosha kwa wanafunzi, lakini pia motisha kwa walimu ni muhimu ili kuwaongezea moyo wa kufundisha.

Ninaamini hayo na mengine yakifanyika, maana ya kuwapo kwa elimu bure nchini itaonekana, kwani kwenye sekta ya elimu kuna changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wadau wake.

Lengo lisiwe upatikanaji wa elimu kwa watu wengi, bali kinachotakiwa kuzingatiwa ni ubora wa hiyo elimu wanayopewa wanafunzi ili wakiingia kwenye soko la ajira wapambane.

Kila mmoja wetu atimize wajibu wake pale anapotakiwa kwani lengo siyo kuhitaji elimu bure tu bali ipatikane katika mazingira rafiki kwa mwanafunzi kuliko ilivyo sasa, huku baadhi ya shule zikiwa hazina madawati na vyoo vya kutosha.