Bila sekta binafsi uchumi viwanda mtihani

16Apr 2017
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
NAWAZA KWA SAUTI
Bila sekta binafsi uchumi viwanda mtihani

BENKI ya Dunia (WB) imewasilisha ripoti ya tisa ya Hali ya Uchumi wa Tanzania, yenye kichwa cha habari Fedha iliyo karibu na mada mahususi iliyojadiliwa na wataalamu wa uchumi isemayo upatikanaji wa huduma za fedha kwa wote.

Pamoja na mambo mengi yaliyoelezwa katika ripoti hiyo ya mwaka 2016 iliyotolewa Aprili 11, imesisitiza umuhimu wa serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kuinua uchumi wa Tanzania.

Mkurugenzi wa WB, Bella Bird, amesema ili kuendelea kusisimua ukujaji wa uchumi siku zijazo na kutengeneza tija, Tanzania inahitaji kufungulia uwezo sekta binafsi.

Anaeleza kuwa Tanzania inayoelekea kwenye uchumi wa viwanda, inapaswa kuelewa kuwa maelewano baina ya mamlaka za umma na sekta binafsi ni muhimu.

Anabainisha kuwa ushirikiano huo ni pamoja na kuwa na sera rafiki na katika sekta za kodi na tozo zilizorekebishwa, upatikanaji wa nishati nafuu na muunganisho katika uchukuzi wenye ufanisi ili kuziba pengo la miundombinu.

Pia, uwekezaji katika elimu na ujuzi, upatikanaji wa huduma za fedha, zote zikiwa ni sekta muhimu katika kukua kwa uchumi wa Tanzania.

Watalamu na viongozi mbalimbali ndani na nje wamethibitisha kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi, kwa kuwa ndiyo inayoajiri watu wengi kwa kuwa serikali haiwezi kuajiri Watanzania wote.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa wahitimu 800,000 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka, na wengi hukosa ajira jambo ambalo linaashiria kuwa bado sekta ya umma na binafsi hazijashirikiana vyema katika kuinua uchumi.

Nguvu kazi hiyo ni kubwa lakini inashindwa kujiajiri kutokana na changamoto mbalimbali kama kukosa mikopo ya riba nafuu, na anapofungua biashara mazingira siyo rafiki kumwezesha kufikia malengo yake.

Sekta binafsi inaelezwa kuanza kuporomoka kwa kutokana na kufungwa kwa biashara mbalimbali zaidi ya 2,000, huku makampuni mbalimbali yakipunguza wafanyakazi ambao wanakwenda kuongeza kundi la watu wasio na ajira.

Wakili, Dk. Hawa Sinare ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baodi ya Kahawa nchini (TCB), katika mjadala alieleza jinsi wakulima wanakabiliwa na riba kubwa na anapopata matatizo kwenye shughuli zake riba huongezeka kiasi cha kushindwa kulipika.

Anasema hakuna namna Tanzania inaweza kuendelea iwapo itakiacha kilimo nyuma ambacho kinategemewa na Watanzania asilimia 70 wanaoishi vijijini, lakini hayo yanawezekana iwapo kutakuwa na mazingira rafiki kwa kujiajiri kwenye kilimo.

Mathalani, alitolea mfano wa vijana walioamua kuingia kwenye kilimo baada ya kuhitimu masomo yao walilima nyanya, ambazo zilikosa soko na hawakuweza kusafirisha nje au kuhifadhi kwa ajili ya kuziuza soko litakapokuwa zuri, jambo ambalo linahitaji mabadiliko makubwa.

Vile vile ripoti hiyo imeeleza uwezekezaji katika sekta binafsi mwaka 2001 hadi 2005 ulikuwa asilimia 12.7 na sekta ya umma ikiwa asilimia 31.4, lakini kwa sababu mbalimbali ikiwamo mdororo wa uchumi na ubinafsishaji kulikuwa na mporomoko.

Kadhalika, imeeleza kuporomoka kulianza mwaka 2006 hadi 2010 kwa sekta binafsi kuwa asilimia 2.9 na sekta ya umma asilimia 0.5.

Kwa mwaka 2011 hadi 2015, uwekezaji kwa sekta binafsi umeendelea kuporomoka kufikia asilimia 2.3 na sekta ya umma ikibaki vile vile.

Ili kunusuru hali hii kwa Tanzania inayojipambanua kuwa ya viwanda, ni lazima kuwe na ushirikiano baina ya sekta zote mbili, zikifanya kazi kwa pamoja kuwezesha upatikanaji wa ajira na kukuza uchumi.

Sekta binafsi imepaza sauti mara kwa mara kueleza vikwazo vinavyowakabili kufikia malengo.

Baadhi ya malalamiko hayo ni mazingira yasiyo rafiki kwa wafanyabiashara, ambayo yamechangiwa na mabadiliko ya sheria na sera za biashara bila kuwashirikisha wafanyabiashara wenyewe, urejeshaji wa malipo ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na umeme wa uhakika.