Bakita mnaridhia uchafuzi wa Kiswahili?

29Dec 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Bakita mnaridhia uchafuzi wa Kiswahili?

‘ZALI la Mwanaspoti lampagawisha mshindi’ ni kichwa cha habari kwenye gazeti hilo la michezo. Habari chini ya kichwa hicho iliandikwa:

“ZALI la Mwanaspoti limezidi kuwapa furaha wasomaji wa Mwanaspoti baada ya mshindi wa pili wa tiketi ya ndege ya kwenda kucheki Ligi Kuu ya England (EPL), Abel Jackson kupagawa kwa kushinda tiketi hiyo.”

 

Habari hiyo imetumia neno ‘zali’ mara tano lisilo la Kiswahili (kwa maoni yangu) na lingine ni ‘pagawa’ linalotumiwa mara kwa mara, tofauti na maana yake halisi! Tatizo ni kwamba waandishi wa magazeti ya michezo hutumia maneno mengi ya mitaani kwa dhana kuwa ‘wanapamba’ lugha kumbe wanapotosha!

 

Maana ya ‘pagawa’ ambalo pia huitwa ‘chagawa’ au ‘pagaa’ ni pandwa na pepo, pandwa na shetani, hemkwa. Je, ni kweli Abel Jackson amepandwa na pepo/shetani (pagawa) kwa kushinda tiketi ya kwenda Uingereza kuangalia mechi za Ligi Kuu ya England (EPL)?

 

Je, mwandishi wa habari hiyo amefuatilia kujua kama mshindi amepungwa (tolewa shetani kichwani) ili wasomaji wajue maendeleo yake? Kama upungwaji  hautakamilika mpaka tarehe ya safari, mshindi wa tatu atasafirishwa badala yake? Hii ndio athari ya kutumia maneno ya mitaani!

 

Neno lingine linalopotoshwa kila siku ni ‘hoho’ (aina ya pilipili) ambayo hudhaniwa ni pilipili mboga/tamu kumbe sivyo. Kwa hakika ‘hoho’ ni pilipili nyembamba ndogo inayowasha sana. Jina lingine la pilipili ‘hoho’ ni ‘pilipili kichaa’ kutokana na ukali wake. Aina nyingine ni pilipili doria, pilipilimanga, pilipili mbuzi n.k.

 

Mwandishi wa gazeti maarufu nchini aliandika kwa kirefu jinsi pilipili hoho ilivyo na uwezo wa kupambana na saratani. Ameandika ‘pilipili hoho’ mara tano na ‘hoho’ mara tatu kisha akaeleza tafsiri yake kwa Kiingereza kuwa ‘sweet pepper’ kumbe alijikanganya mwenyewe.

 

‘Sweet’ maana yake ni tamu. Jina lingine la pilipili mboga ni pilipili tamu kama alivyoandika mwandishi (sweet pepper)! Pilipili mboga pia hutumiwa kutengenezea kachumbari na hata inapotafunwa haiwashi. Sidhani kama kuna anayethubutu kutafuna pilipili ‘hoho’ labda mtu aliyepagawa (pandwa na pepo/shetani)!

 

Soma kichwa cha gazeti la michezo: “Tizi la Mrundi lawapagawisha” kikifuatiwa na habari kwamba: “Wachezaji wa Simba wameukubali mzuka wa Kocha mpya msaidizi.”

 

Kwanza neno ‘tizi’ limetoholewa na lile la Kiingereza (practice) ambalo maana yake kwa Kiswahili ni mazoezi. Kwa hiyo badala ya ‘tizi’ ambalo halimo kwenye msamiati wa Kiswahili, mwandishi angeandika ‘mazoezi’au ‘zoezi.’

Hata hivyo kama zoezi la Mrundi

‘limewapandisha wachezaji mashetani’ iweje tena mwandishi aandike kuwa aina yake ya utendaji (kocha) imeonekana kuchangamsha mazoezi ya Simba ambapo wachezaji wanamuona kama mwenzao na wamekuwa wakifanya mazoezi kwa nguvu zaidi?

 

Kwa kutojua maana ya ‘pagawa’ (pandwa na pepo) na ‘mzuka’ (kiumbe kisichoonekana ila hudhaniwa kuwa kinaishi na huweza kumtokea mtu; pepo) mwandishi katumia maneno hayo kwa raha zake kumbe anapotosha!   

 

“Omog awafanyia kitu mbaya Mtibwa Sugar.” Habari chini ya kichwa hicho imeandikwa:

 

“Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog ameichungulia ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara akagundua kwamba wanalingana pointi na Mtibwa Sugar na sasa ameamua kushusha jeshi lake lote kuwakabili wakata miwa hao katika mchezo utakaochezwa leo Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.”

 

‘Kitu mbaya’ si Kiswahili sahihi bali husemwa ‘kitu kibaya.’ Habari hiyo yenye paragrafu saba hakuna hata moja inayoeleza jinsi Omog alivyowafanyia Mtibwa Sugar kitu kibaya ila kwa mwandishi, Omog kushusha jeshi lake mazoezini kwa maandalizi ya kuikabili Mtibwa ni ‘kitu kibaya!’

 

“Kocha Mrundi mwenye mizuka atua Simba” ni kichwa kilichoandikwa kwa herufi kubwa katika mistari mitano ukurasa wa mbele wa  gazeti la michezo. Niliposoma kichwa hicho, nikajiuliza: iweje Simba imwajiri kocha mwenye mizuka (mapepo)?

 

    

‘Bwana’ ni jina la heshima linalotumiwa kwa mwanamume; hababi. Mwanamume aliyeoa mwanamke; mume.

 

Mwanamume ambaye amemwajiri  mtu; mwajiri. Kidini ni Mwenyezi Mungu, Mola, Muumba. Neno hilo pia ni kihisishi cha kumgutusha mtu au kumfanya awe makini: Bwana!

 

Hata hivyo siku hizi neno ‘bwana’ limefanyiwa ‘marekebisho’ na wachafuzi wa lugha kwa kuliandika ‘bana,’ ‘bhana’au ‘buana!’

 

Mwandishi kaandika hivi: “Watu buana! Kitendo cha mwanamitindo Hamisa Mobeto kuposti ujumbe katika peji yake ya Instagram kwa kuandika maneno ya kumpa pole mwigizaji wa filamu Lulu kwa janga alilolipata la kufungwa jela miaka miwili eti wanasema Hamisa anajikosha ili kutaka kuyarudisha majeshi kwa Majizo ambaye anadaiwa kutoka na Lulu baada ya kumtema Hamisa.” (Maneno 51 katika sentensi moja! Kwa nini?).

 

Kwa nini waandishi wa magazeti ya michezo hubadili maneno ya Kiswahili na kuyapa maana tofauti? Hujasikia vijana wakisalimiana: “Mambo ni aje” kama jirani zetu?

Methali: Werevu mwingi mbele giza

[email protected]

0715 334 096 / 0622 750 243